loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maendeleo awamu ya tano yameimarisha muungano, amani Z’bar

TANGU kuanzishwa kwa siasa za ushindani wa vyama vingi mwaka 1992, Zanzibar hapakuwahi kuwa na utulivu wa kisiasa kwa muda mrefu sana.

Kila uchaguzi mkuu ulifuatiwa na mikwaruzano na kusababisha mpasuko wa kisiasa wa muda mrefu kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kilichokuwa chama kikuu cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF).

Kwa wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar watakumbuka kati ya mwaka 1995 na 2005 iliibuka misemo ya ngangari na ngunguri au jino kwa jino ikiashiria utayari wa wanasiasa hawa wa upinzani kupambana na vyombo vya dola visiwani humo.

Katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo, mambo mengi yalifanyika ikiwemo kupitisha Katiba inayoruhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 tulishuhudia Zanzibar ikiunda SUK ikiongozwa na Rais Ali Mohamed Shein (CCM), pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, kutoka CUF na Makamu wa Pili wa Rais kutoka CCM. 

Hata hivyo, wasomaji wa makala haya watakumbuka kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 ulifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na baadae kutangaza uchaguzi wa marudio mwaka 2016.

Chama cha Wananchi (CUF) kilisusia uchaguzi huo kikidai kuwa walipokonywa ushindi wa rais na hali hii ikaleta sintofahamu kubwa juu ya hali ya kisiasa visiwani humo.

Wachambuzi wa mambo wakatabiri kuwa muhula wa 2016-2020 ungekuwa ni kipindi cha mpasuko mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar na uwezekano wa kuwepo vurugu za mara kwa mara. La hasha haikuwa hivyo!

Zanzibar iliendelea kubaki tulivu hata sasa, na makala haya inajaribu kufafanua kuwa, utulivu huu ni kwa hisani ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John Magufuli kwa kushirikiana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuwekeza katika maendeleo ya watu.

Hata hivyo, mvutano wa kisiasa baina ya pande zinazohasimiana visiwani Zanzibar una uhusiano wa moja kwa moja na uimara wa Muungano wenyewe.

Lakini katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Rais Magufuli na Rais Shein walifanya kazi ya ziada kuhamisha mawazo na fikra za Wazanzibari kutoka kufikiria vurugu na mpasuko wa kisiasa ili wafikirie maendeleo.

Marais hawa hawakutaka kuona jamii ya Watanzania wanajikita kwenye siasa za ngunguri na ngangari wakati tuna kazi kubwa ya kusukuma maendelo ya nchi.

Na katika kuongoza mabadiliko haya ya kifikra, Rais Magufuli aliiweka Wizara ya Muungano chini ya kiongozi hodari Mzanzibari, Mama Samia Suluhu, ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Busara na uthabiti wa Mama Samia Suluhu ni moja ya mambo yaliyoimarisha muungano wetu na kupunguza migogoro ya kisiasa visiwani Zanzibar.

Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar, uliofanyika mwaka 1964, una historia ya kipekee na unaheshimika kama tunu ya taifa hili kwa pande zote mbili kwa kuwa uliwaunganisha wananchi ambao wana historia ndefu ya udugu.  Lakini hata hivyo, muungano huu umekuwa na kero zake mahusisi na za jumla jumla. 

Moja ya mambo ambayo Serikali ya Rais Magufuli aliyapa kipaumbale ni kushughulikia kero za Muungano. Vikao takribani 83 vimekaa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapunduzi Zanzibar (SMZ) kati ya mwaka 2015- 2020.

Katika kipindi hiki jumla ya kero 18 zilijadiliwa na kero 11 kati ya hizo zilipatiwa ufumbuzi. Nitajaribu kufafanua kwa nini kero hizi zinazolenga maendeleo ya Zanzibar zilituliza kabisa siasa za vurugu visiwani humo.

Moja ya kero hizo ni kuipa Zanzibar mamlaka ya kushughulikia mafuta na gesi wao wenyewe. Mchakato huu ulihusisha kutungwa kwa sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 ya SJMT ambayo ilifuta sheria ya zamani ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta Sura ya 328 na kutungwa kwa Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 ya Zanzibar.

Lakini pia Serikali iliondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye umeme unaouzwa na Tanesco kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO), jambo ambalo liliwapa Wazanzibari unafuu wa kununua umeme. Lakini pia SJMT ilifuta deni la Shilingi bilioni 22.9 ambalo Tanesco walikuwa wanadai kwa shirika la ZECO.

Majadiliano hayo pia yalipelekea kupitishwa kwa mwongozo wa ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kikanda na kimataifa, zikiwemo ziara za viongozi wa kitaifa katika mikutano ya kimataifa.

Lakini pia majadilino haya yameweka mwongozo juu ya nafasi ya masomo ya elimu ya juu nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada au mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Katika kutatua kero ndogo ndogo za Muungano, vyombo vya moto vilivyosajiliwa Tanzania Bara yakiwamo magari na namba zake ni ruhusa kutumika Zanzibar na utaratibu kama huo kutumika kwa magari yaliyosajiliwa Zanzibar na kutumika upande wa Tanzania Bara.

Mfumo wa ulipaji kodi ya ongezeko la thamani (VAT), umebadilika, bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kuingia soko la Zanzibar, zitalipiwa Zanzibar badala ya Tanzania Bara na utaratibu kama huo utumika kwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kulipiwa Tanzania Bara.

Kabla ya mabadiliko hayo, Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa wakala wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na ilikusanya kodi ya VAT kwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara na kuingizwa Zanzibar.

Katika kuhakikisha SMZ inakimbiza miradi mbalimbali visiwani humo, Serikali hiyo iliendelea kupata asilimia 4.5 ya fedha za misaada ya kibajeti.

Takwimu zinaonyesha kuwa fedha zilizotolewa katika kipindi cha 2015 2020 ni shilingi bilioni 174.1, ambapo kati ya pesa hizo shilingi bilioni 6.8 ni za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo.

Vilevile shilingi bilioni 105 zilitokana na kodi ya mshahara (PAYE), wakati shilingi bilioni 27.2 ni msaada wa kibajeti na shilingi bilioni 35.1 ni gawiwo la faida ya Benki Kuu ya Tanzania. Pesa hizi ziliisaidia Zanzibar kutekeleza miradi yake ya maendeleo.

Lakini pia katika kipindi kigumu cha corona, SJMT ilitoa shilingi milioni 500 kwa SMZ ili waweze kupambana na mlipuko wa janga hilo la corona.

Pesa hizi zilitokana na busara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Magufuli kufuta sherehe za Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar zilizokuwa zifanyike tarehe 26 Aprili 2020 na kuamuru pesa hizo zitumiwe na Serikali ya Zanzibar kukabiliana na dharura hiyo.

Hatua hii pia inatafsiriwa kama nia nzuri ya kiongozi huyu wa kitaifa kujenga mahusiano mazuri baina ya pande zote mbili za Muungano.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bado una changamoto zake hasa katika masuala ya fedha na uchukuzi, lakini tulichojifunza kutokana na utekeleazaji Sera za CCM kwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuwa Wanzanzibari wanataka maendeleo na siyo vurugu za kisiasa.

Lakini pia Muungano wetu utaendelea kubaki imara pale ambapo pande zote mbili zinashuhudia dhahiri jitihada za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Wasomaji wa makala haya bila shaka watagundua kuwa, katika kipindi chote hicho cha utelekelazji wa Ilani ya CCM chini ya uongozi wa awamu ya tano, wananchi wa Zanzibar walikuwa watulivu sana ili kuipa serikali yao fursa ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Na hivyo basi, Serikali hizi mbili zilitumia muda huo kushughulikia kero zilizodumu muda mrefu baina ya pande zote mbili kwa ufanisi mkubwa.

Ni matumaini yangu kama mchambuzi kuwa miaka mitano ijayo, Wazanzibari wataamua kumpa tena kura Rais Magufuli ili amalize kazi aliyoianza ya kutatua kero na kuleta utulivu wa kisiasa visiwani humo.

Migogoro ya kisiasa kamwe haijawahi kuwa mtaji kwa mwananchi wa kawaida na katika tathmini hii tunashawishika kusema kuwa Wazanzibari watachagua maendeleo na siyo siasa za ngangari na ngunguri.

Rais Magufuli ameonyesha mfano wa namna ya kuachana na siasa za migogoro zinazofanywa kama mtaji na baadhi ya wanasiasa na badala yake alisisitiza kusimamia maendeleo ya nchi yetu Tanzania.

Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Jamii na mchangiaji katika gazeti hili.

 

KESHOKUTWA Watanzania wanapiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Wagombea waliokuwa ...

foto
Mwandishi: Dk Richard Mbunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi