loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bilioni 25.3/- zaboresha  barabara, mitaa Musoma 

Bilioni 25.3/- zaboresha barabara, mitaa Musoma 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Sh bilioni 25.3 zimetumika kuboresha barabara na mitaa ya Manispaa ya Musoma, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya mwaka 2015-2020.

Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Mji wa Musoma katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Mara Sekondari, Kata ya Nyamatare, wilayani Musoma, mkoani Mara.

"Shilingi bilioni 18.7 zimetumika kujenga kilometa 14 za barabara kwa kiwango cha lami na kuweka taa za barabarani kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miji (ULGSP) katika Manispaa ya Musoma na mradi umekamilika. Tunataka taa ziwake ili usiku uwe mchana, na mchana uwe mchana,"alisema Majaliwa.

Alisema kupitia fedha za matengenezo kutoka mfuko wa barabara Sh bilioni 6.6 zilitumika kufungua barabara mpya, kufanya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya sehemu korofi na kwamba miradi yote imekamilika.

Katika mkutano huo, Majaliwa alimuombea kura mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli, mgombea ubunge Musoma Mjini, Vedasto Manyinyi, mgombea udiwani wa kata ya Nyamatare, Masumbuko Magesa na wagombea wengine wa udiwani kwenye manispaa hiyo.

"Ninawasihi wana Musoma msisite kumpigia kura Dk John Magufuli hata kama wewe ni mpenzi wa chama kingine kwa sababu yeye ndiye mleta maendeleo kwa nchi yetu," alisema.

Alisema, kwa kutekeleza ilani ya CCM: "Kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani" ilitekelezwa kwa lengo la kumpunguzia mama kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

"Ili kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwenye mji wa Musoma, Sh bilioni 46 zilitolewa kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji safi katika Manispaa ya Musoma ambao tayari umeanza kutoa huduma."

Alisema Sh bilioni 18 zimetolewa kwa mradi wa kusambaza maji katika manispaa ya Musoma na vijiji vitatu vya Musoma Vijijini na Butiama.

Alitaja kazi zilizofanyika kuwa ni pamoja na ujenzi wa tangi la Bharima lenye ujazo wa lita milioni tatu; ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (Booster station) na ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kwenda kwenye tangi la Bharima (Rising main) lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 1.56.

 Alizitaja kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni ulazaji wa bomba la kusafirisha maji kutoka kwenye tangi la Bharima kwenda kwa wananchi lenye kipenyo cha milimita 450 na urefu wa kilomita 7.058; ufungaji wa pampu tatu zenye uwezo wa kusukuma mita za ujazo 175 kwa saa; ununuzi wa mabomba ya kusambaza maji kilomita 44.3 na ununuzi wa vifaa vya kutendea kazi.  

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Musoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi