loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Urejelezaji takataka kuongeza malighafi

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema urejelezaji wa takataka na vyuma chakavu utachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa malighafi za viwanda na kupunguza gharama za kuigiza malighafi hizo nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samwel Gwamaka, alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Watanzania wameitikia vizuri biashara ya kuchakata vyuma chakavu na hivyo kuongeza upatikanaji wa malighafi viwandani.

“Mfumo wa urejelezaji wa vyuma chakavu na takataka za aina mbalimbali katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeleta mafanikio makubwa kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja, lakini pia umeongeza kasi ya upatikanaji wa malighafi katika viwanda vyetu vya ndani,”alisema.

Alisema uagizaji wa malighafi kutoka nje ya nchi ni gharama kubwa kwa wenye viwanda na pia, hutumia muda mrefu kufika nchini hali inayozorotesha utendaji kazi na uzalishaji viwandani.

Aidha, Dk Gwamaka alizitaka halmashauri zote nchini kutengeneza utaratibu wa namna ya kukusanya takataka ili kurahisisha ukusanyaji wake pamoja na vyuma chakavu ili kuzirejeleza katika viwanda nchini.

“Vyuma chakavu na baadhi ya takataka ni fursa nzuri kwa wananchi kuwaingizia mapato hususani wanaozikusanya, lakini hata kwa halmashauri kwani zimekuwa zikikukusanya kodi kupitia biashara hiyo. Mwito wangu kwa halmashauri zote nchini, ni kutengeneza utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa takataka hizo.”

“Mfumo wa urejelezaji wa takataka umetusaidia sana kuyafanya mazingira yetu yawe mazuri, lakini pia umepelekea viwanda kupata malighafi muhimu, hali ambayo imechochea kasi ya ukuaji uchumi na kuingia uchumi wa kati,”alisema.

Hata hivyo, Dk Gwamaka amewaonya watu ambao wamekuwa wakiharibu miundombinu ya madaraja, umeme, nyaya za simu na maji kwa ajili ya kuuza vipande kama vyuma chakavu kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi