loader
Dstv Habarileo  Mobile
Miradi ya maji  ya bilioni 58.8/-  yakamilika

Miradi ya maji ya bilioni 58.8/- yakamilika

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekamilisha ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa kwa Sh bilioni 58.8.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa Getrude Mongella mjini Nansio Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wakati akizungumza na wakazi wa mji huo. 

“Shilingi bilioni 58.8 zimetumika kwenye ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji ambapo miradi ya maji katika Mji ya Longido, Sengerema na Nansio-Ukerewe imekamilika,” alisema Majaliwa.

 Majaliwa alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 13 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji zikiwemo Sh bilioni 10.9 za uboreshaji wa huduma ya majisafi mjini Nansio. Alisema wakazi 108,653 wananufaika na mradi huo katika eneo la mji wa Nansio. 

Majaliwa alisema Sh bilioni 2.1 zilitumika kwa uboreshaji huduma ya usafi wa mazingira mjini humo. 

Alisema miradi ya maji na uchimbaji visima ilitekelezwa kwa Sh bilioni 1.3 ukiwemo ukarabati wa mradi wa maji Irugwa, mradi wa maji ya bomba ya Nansore, mradi wa maji wa Muriti/Ihebo, upanuzi wa mradi wa maji wa Chabilungo na upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Kazilankanda.

 Majaliwa amekuwa Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais John Magufuli. Pia, aliwaombea kura mgombea ubunge Jimbo la Ukerewe, Joseph Mkundi na wagombea udiwani wa kata za Wilaya ya Ukerewe.

 Kuhusu uvuvi, Majaliwa alisema katika kutekeleza Ilani ya CCM, serikali iliondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio.

 Kwa sekta ya afya, Majaliwa alisema hospitali ya wilaya hiyo ilipatiwa Sh. milioni 570 kujenga jengo la kisasa la upasuaji (theatre), ujenzi wa duka la dawa, ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti na ukarabati mkubwa wa wodi saba ambazo zote zinatumika. 

 Kwa upande wa umeme, alisema kati ya vijiji 76, vijiji 70 vimepelekewa huduma ya umeme na vijiji sita bado havina umeme, ambavyo ni Kaseni, Busangumugu, Murutilima, Kitanga, Namakwekwe na Muhande.

 Kuhusu elimu, alisema mpango wa elimu bila malipo kuanzia 2015/2016 – 2019/2020 uliwezesha shule za msingi 123 zipatiwe Sh bilioni 3.29 za ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

 Chini ya mpango huo, shule za sekondari 23 zilipatiwa Sh bilioni mbili kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

 Kwa shule za sekondari, alisema Sh milioni 873 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule za Bukongo, Pius Msekwa, Bwisya, Muriti na Lugongo na nyinginezo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Ukerewe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi