loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DAYNES FIRE: Msanii anayeamini kukata tamaa ni anguko la mafanikio

JINA lake halisi la kuzaliwa ni Zawadi Daudi, lakini kutokana na umaarufu wake kisanaa, wasanii wenzake walimbatiza jina na kumuita ‘Dayness’ jina ambalo lilitokana na Daudi, jina halisi la baba yake mzazi mwenyeji wa Babati mkoani Manyara.

Daynes anasema haikuwa rahisi kwake kufika mahali alipo sasa hasa kutokana na uhalisia wa maisha ya wazazi wake kuwa ya hali ya chini tangu kipindi alipozaliwa jambo lililomfanya kufikia hatua hadi kukosa fursa ya kutimiza ndoto zake za elimu ya juu kutokana na sababu ambazo hata hivyo hakutaka kuziweka wazi kwa sasa.

Anasema katika kipindi cha makuzi yake alikuwa miongoni mwa watoto wa kike waliokuwa wakipendwa sana katika mtaa waliokuwa wakiishi na hiyo ni kutokana na haiba ya upole na heshima aliyokuwa nayo kitu anachodai kwamba kilikuwa kikiwapendeza watu wengi wa mtaa wake sambamba na wazazi wake.

Msanii huyo ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto 11, nane wa kike na watatu wa kiume wa familia ya Daudi Adiya na kkewe Victoria Saria, anasema kwake suala la kuigiza ndiyo lilikuwa katika moyo wake tangu akiwa mtoto kutokana na mapenzi yake ya kutazama sana filamu na tamthilia mbalimbali zilizokuwa zikionyeshwa katika luninga na kanda mbalimbali.

“Namshukuru Mungu katika kuhangaika hangaika hapa na pale maisha yalinifanya kuja mjini ili pamoja na mambo mengine niweze kutimiza ndoto zangu ya sanaa ya uigizaji, nikiamini kuwa nilikuwa na uwezo wa kutosha kama ambavyo wasanii waliokuwa wakitamba kipindi hicho walikuwa wakifanya,” anasema Dayness.

Anasema alipofika jijini Dar es Salaam, mwanzoni alikutana na changamoto mbalimbali ikizingatia kuwa yeye ni ‘mtoto wa kike’ kitu anachodai kuwa wakati fulani kilitaka kumfanya akate tamaa na kurudi nyuma lakini akasisitiza kuwa kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda ndipo alieendelea kuyaozoea mazingira hayo na kuamua kusongambele.

“Unajua sisi wanawake huwa tunakutana na vikwazo vingi sana ambavyo kama hutokuwa makini unaweza kujikuta unashindwa kutimiza malengo yako uliojiwekea kwa sababu ya kukatishwa tamaa, kwangu mimi nilipiga moyo konde na kuamua kupambana sababu nilikuwa najielewa ni kitu gani nakitafuta,”anasema Daynes Fire.

Anasema unapokutana na changamoto unapaswa kuchukulia kama chachu ya kufanya vizuri na kwamba alipokutana nazo hasa alipokuwa akiona wasanii wenzake wa kike wakifanikiwa kitu ambacho kilikuwa kikimpa moyo siku hadi siku na kuongeza juhudi bila kufikiria kurudi nyuma sababu siku zote lengo lake ni kufika mbali zaidi ya alipo sasa.

“Dhamira yangu ni kufika mbali na muziki wangu, siyo Tanzania hii bali ngazi ya dunia kwa sababu hicho ndicho nilichojiwekea moyoni, suala ni malengo tu, nina amini kila mtu anaweza kutimiza ndoto zake kama hili la kujiwekea dhamira ndani ya moyo litafanyika,” anasema.

Daynes anasema rasmi alianza kufanya muziki mwaka 2017 bila kusimamiwa na mtu yoyote, na kudumu hivyo hadi Mwaka 2018 alipopata usimamizi chini ya Kampuni ya ‘CMB Bright’ inayomsimamia hadi sasa huku akikiri wazi kuwa tangu amekuwa chini ya usimamizi huo anaona sasa umefika wakati sahihi wa kufikia yale malengo aliyojiwekea.

Anasema sababu iliyompelekea kuingia katika muziki ni baada ya kuona nafsi yake inamtuma sana kuacha uigizaji na kufanya muziki huku kila wakati akijikuta akiimba nyimbo za wasanii mbalimbali pamoja na kupenda kutazama muziki huo katika luninga tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mapenzi yake makubwa yalikuwa katika kuangalia filamu za uigizaji.

Hata hivyo anasema pamoja na kujikuta hivi sasa ameangukia katika kupenda sana muziki huko nyuma alikuwa mpenzi mkubwa wa kuigiza na kwamba katika kipindi hicho alifanikiwa kucheza filamu mbili ikiwemo ya ‘Safari hatari’ iliyochezwa Mwaka 2015 na kufanya vizuri na baadaye ilichukuliwa na moja kituo cha utangazaji cha Azam na kupewa jina la ‘Wazee wa Mjini.’

Anasema Mwaka 2014 ndiyo mwaka ambao alicheza filamu yake ya kwanza ambayo hata hivyo anadai kuwa haikuweza kufanya vizuri sokoni tofauti na Wazee wa Mjini anayosema kwa kiasi kikubwa ndiyo iliweza kumtambulisha katika jamii na kumfanya aanze kujulikana.

Daynes anasma baada ya kucheza filamu mwaka 2015 na kumfanya aanze kujulikana katika jamii akaona kuwa ni wakati wake kubadilisha upepo na kuhama kutoka katika sanaa hiyo ya uigizaji na kuingia katika sanaa ya muziki na anasisitiza kuwa mara baada ya wazo hilo kumjia alijikuta taratibu anapoteza mapenzi yake na sanaa ya uigizaji.

“Niliona umefika wakati sasa wa kujaribu kufanya kitu kingine, kwa kuwa tayari nilishafanya katika uigizaji na sikupata kile nilichokihitaji nikaona vyema kuingia upande wa pili wa sanaa ya muziki na kama ilivyokuwa upande wa uigizaji nilikuwa na mapenzi napo,” anasisitiza Dayness Fire.

Anasema katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 2015 hadi 2016, aliamua kutulia ili kufanya tathimini ya sanaa hiyo ya muziki akihofia kuingia ‘kichwa kichwa’ kwa kuwa aliamini kila kitu ni lazima kwanza kujipanga kabla ya kuanza kukifanyia kazi ambapo alifanya hivyo hadi mwaka 2017 alipoamua kuanza rasmi muziki wake.

Daynes Fire anasema baada ya kuanza kufanya muziki akiwa mwenyewe bila ya uongozi alifanikiwakutoa nyimbo tatu ya kwanza ukiitwa Rejea, wa pili ‘Daynes Fire’ na wimbo wa tatu unaitwa ‘Ana mapepe’ na akiwa chini ya uongozi wa Kampuni yake ya CBM na tayari mpaka sasa ameshatoa nyimbo nne ambazo ni Dawa, Gape, Mwaa na ‘Do it’ uliotoka hivi karibu.

“Nyimbo nyingine nyingi zinakuja hivi karibuni lakini zilizopo unaweza kuzipata katika akaunti mbalimbali ikiwemo You- Tube, ukiandika CBM Bright unakutana na nyimbo nilizozifanya nikiwa chini ya uongozi, lakini ukiandika ‘Daynes Fire’ utakuta nyimbo nilizozifanya zile nilizozifanya nikiwa mwenyewe bila ya uongozi,” anasema Daynes .

Aidha Daynes anasema nyimbo zake zote zilizotanguliwa ukiwemo huo mpya unaotamba katika vituo mbalimbali vya redio ndani na nje ya nchi pamoja na mitando ya kijamii ni kama mawingu tu na kudai kuwa mvua ya mambo mazuri na matamu kutoka kwake yanakuja kutokana na kuwa chini ya uongozi unaotambua vyema thamani ya muziki.

Mbali na muziki Dayness hupendela mambo mbalimbali ikiwemo kutazama filamu, tamthilia, kusoma vitabu pamoja na kuogelea lakini zaidi kuona wanawake wenzake wakipambana kutafuta maendeleo.

“Wanawake hakuna kukata tamaa hata kama kuna watu wanawakwamisha katika hatua mbalimbali mnazopitia,” anasema.

Kwa mujibu wa Daynes, katika maisha kukata tamaa ni marufuku na kuongeza kama yeye angekuwa mtu wa kukata tamaa asingeweza kufika mahali alipo sasa kwa kuwa alikutana na mambo mengi ya ajabu lakini alipambana na kuyashinda hadi kufika hapo alipo sasa.

Anasema kutokana na changamoto alizozipitia yeye kama mwanamke hadi kufika mahali alipo sasa hayupo tayari kuona wasichana wenye nia ya kufanya muziki au kuigiza wakipitia changamoto kama hizo na kuahidi kutumia uwezo wake kupambana ili kuwasaidia waweze kufikia au kutumiza ndoto zao.

WANAWAKE wamekuwa ni chachu kubwa ya ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi