loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanaofanya siasa nyumba za ibada wakemewa

KAMATI ya Amani Tanzania imelaani na kukema tabia ya baadhi ya viongozi wa dini nchini kutumia nyumba za ibada kufanya kampeni kwa baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa na kudai kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani kama itaendelea kufumbiwa macho.

Wakizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, kamati hiyo inayoongozwa na viongozi wa dini mbalimbali, walisema umefika wakati kwa viongozi wa makanisa na misikiti wanaofanya hivyo kuchagua jambo moja kati ya kuendelea na suala la kuhubiri dini au kwenda katika majukwaa na kufanya siasa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema haipendezi kuona baadhi ya viongozi wa dini wanaacha majukumu yao ya kuwaongoza waumini wao katika masuala ya kidini na kugeukia siasa ndani ya nyumba za ibada ambamo ndani yake kuna waumini wenye itakadi ya vyama tofauti.

“Hili ni suala linalopaswa kukemewa kwa nguvu zote, haipendezi kuona kiongozi wa dini anasimama mbele ya wananchi wake na kuacha kabisa kufanya jukumu lake la kuhubiri neno la Mungu na kuanza kuzungumza siasa, huu siyo utaratibu uliowekwa hata kwa mujibu wa sheria zetu za nchi, wanaofanya hivyo wanapaswa kuacha mara moja,” alisema Shehe Alhad.

Alisema kama kiongozi yeyote anajiona ana mapenzi ya kufanya siasa, hakuna mtu anayemzuia kufanya hivyo lakini anapaswa kutoka katika kazi ya kuwatumikia kiimani waumini wake na kwenda majukwaani, mahali ambapo ndiyo kwenye wigo mpana wa kufanya kitu hicho anachokipenda.

Hatua ya kamati hiyo imekuja kutokana na uwepo wa baadhi ya viongozi hao wa kidini kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo na kiislam kuonekana kuhubiri siasa ndani ya nyumba za ibada, hivyo kuwaacha na hali ya sintofahamu waumini wao wanaokuwa ndani ya nyumba hizo kwa ajili ya kusikiliza neno la Mungu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia Kiongozi wa Taasisi ya Wapo Mission International, Askofu Silvester Gamanywa alisema umefika wakati kwa viongozi wenzao wa kiroho wenye tabia hiyo kubadilika na kuachana na tabia hiyo.

Alisema wakati huu ambao Taifa linaendelea na mchakato wa kampeni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Oktoba 28 Mwaka huu, ni vyema wao kama viongozi wa kiroho wakawa mstari wa mbele kusimamia amani ya nchi badala ya kutengeneza njia za kuibomoa.

Askofu Gamanywa alisema kuna hatari kubwa ya kutengeneza matabaka kwa waumini hasa kwa vitendo vya kuhubiri siasa ndani ya makanisa na misikiti na kusisitiza kuwa wao kama viongozi wanapaswa kuwaongoza waumini wao kuitambua amani na kuisimamia, siyo kueneza siasa makanisani na katika nyumba zingine za ibada.

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi