loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa: Lazima Kisiwa cha Gana kipate umeme

Majaliwa: Lazima Kisiwa cha Gana kipate umeme

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, amesema chama hicho kitapeleka haraka huduma za umeme kwa wananchi wa Kisiwa cha Gana kilichopo Ukerewe, mkoani Mwanza kwani nimuhimu na lazima kwa maendeleo.

Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania, alisema hayo juzi katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kitongoji cha Gana alipomwombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli, mgombea ubunge, Joseph Mkundi na madiwani wa wilaya ya Ukerewe.

Alisema serikali ijayo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020- 2025, itaboresha huduma ya umeme katika visiwa vyote nchini kikiwamo Gana chenye wakazi zaidi ya 3000.

“Mkakati wetu ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata umeme, Ukerewe vijiji 70 tayari vina umeme vimebaki sita ambavyo vitapitiwa na mradi,” alisema Majaliwa.

Alisema asilimia 80 ya vijiji nchini vimepata umeme baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015-2020.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuendeleza na kuimarisha sekta ya nishati ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali.

Mpango wa Serikali ni kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote na maeneo ya pembezoni mwa miji,” alisema Majaliwa.

Alisisitiza kuwa, katika kipindi cha miaka mitano, serikali imepata mafanikio kwa kuzalisha umeme kutoka megawati 1,308 mwaka 2015 hadi 1,602 mwaka 2020 ongezeko ambalo limeifanya nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya umeme.

Alisema upatikanaji wa umeme kwa Tanzania Bara umeongezeka kutoka asilimia 36 mwaka 2015 hadi asilimia 70. Ujenzi wa miradi umepunguza gharama za kuunganisha umeme vijijini kutoka wastani wa Sh 454,000 hadi 27,000.

Kuhusu sekta ya uvuvi, alisema serikali imeondoa kodi katika bidhaa mbalimbali za uvuvi ili kutoa fursa kwa wavuvi kujipatia kipato na kuinua uchumi wa Taifa.

Tayari Serikali imeondoa kodi katika zana na malighafi za uvuvi zikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio.

“Tumedhamiria kuboresha sekta ya uvuvi kwa kuchukua hatua mbalimbali, tumeondoa kodi katika baadhi ya maeneo ili kuhakikisha wavuvi wanapata manufaa kutokana na kazi yao,” alisema Majaliwa.

Alisema chama kupitia Ilani ya CCM, kitaimarisha ulinzi katika Ziwa Victoria kwa kununua boti za ulinzi zitakazowalinda wavuvi wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi.

Katika kuhakikisha wavuvi wanafanya kazi kwa ufanisi, serikali iliimarisha ulinzi kwa kuanzisha kanda kuu tatu katika Ukanda wa Ziwa Victoria, Tanganyika na Pwani.

Pia zimeanzishwa kanda nne ndogo za Ukerewe, Sengerema, Nyumba ya Mungu na Mtera. Wakati huo huo: CCM kimeahidi kujenga kituo cha afya katika Kata ya Irugwa, wilayani Ukerewe ili kuwaondolea wananchi wa kisiwa hicho adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

Hata hivyo, Majaliwa alisema serikali ilishatoa Sh milioni 49.2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo moja la kujifungulia katika zahanati ya Irugwa.

Akizungumzia usafiri wa majini kwa wakazi wa eneo hilo, alisema wanakusudia kujenga vivuko mbalimbali kikiwemo kivuko cha Irugwa, Murtanga, Gana, Kakakuru na Lugezi hadi Kisorya.

Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, chama kinaelekeza serikali ikamilishe ujenzi wa vivuko vipya vinane kikiwemo cha Irugwa - Murutanga (Ukerewe)

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalum

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi