loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

CCM yakaba kila kona

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea na kampeni za uchaguzi mkuu kwa kasi ambayo mgombea urais, John Magufuli sambamba na makada wake, wamefika maeneo mbalimbali wakinadi mafanikio na kuahidi kufanya maendeleo ya haraka makubwa zaidi.

Wakati CCM kikitamba kuzunguka kona zote za nchi huku zikiwa zimesalia siku 31 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, wagombea urais wa vyama vingine vya siasa wameonekana kujikongoja wakiwamo baadhi walioishia njiani na wengine kampeni zao zikitarajiwa kuzinduliwa leo.

CCM kila kona Tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipofungua pazia la kampeni, Agosti 26 mwaka huu, CCM kupitia wagombea na makada wake kimeendelea kuzunguka nchini kikiainisha mafanikio na kuahidi mambo mengine makubwa.

Mgombea wa urais, Rais Magufuli, alihitimisha raundi ya pili ya kampeni hivi karibuni baada ya kunadi sera na ilani za chama katika mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora na kuzungumza na wananchi katika vijiji mbalimbali kisha kufanya mikutano.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema juzi kwamba Magufuli alipata mapokezi makubwa katika mikoa yote aliyofanya kampeni ukiwemo wa Kagera, Kigoma, Geita, Singida, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Mwanza.

Awamu ya tatu inaanzia Iringa, Njombe na Mbeya. Katika mikutano, Magufuli ameendelea kunadi mambo mbalimbali aliyotekeleza, kuahidi kufanya mambo mengine makubwa .

Amekuwa akifafanua hoja zinazotolewa na wagombea wa vyama vingine. Sambamba na kampeni, chini ya kofia ya urais, Magufuli ameendelea kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na kutoa maagizo ya utekelezaji kwenye anayobaini mambo kutokwenda vizuri.

Mgombea mwenza, Samia Hassan Suluhu, pia ameendelea kuzungukia mikoa akieleza mambo ambayo serikali ya awamu ya tano imeyatekeleza na ilivyojipanga kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.

Vivyo hivyo kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa. “Tangu tumeanza kampeni tumekuwa tukiwatuma makada waandamizi sehemu mbalimbali, tunaendelea vizuri katika kampeni za majimbo, kata na urais,” alisema wakati akizungumzia mwenendo wa kampeni za CCM tangu walipoanza hadi sasa akisema chama kinawaahidi Watanzania maendeleo ya haraka.

Mbio za upinzani Mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amefanya mikutano Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera, Singida, Kigoma, Geita, Mbeya, Njombe, Katavi na Tabora. Pia mgombea mwenza, Salum Mwalimu anaendelea na mikutano mikoa mingine. Upande wa vyama vingine, ACTWazalendo kimeishia njiani baada ya mgombea wa urais, Bernard Membe kusimamisha kampeni zake hivi karibuni akiwa amepita kwenye mikoa miwili pekee.

Kabla ya kusimamisha kampeni, Membe alifanya mikutano na kuhutubia mkoani Lindi katika jimbo la Lindi mjini, Kilwa Kaskazini katika eneo la Njinjo na mkoani Pwani ambako alihutubia katika eneo la Ikwiriri, jimbo la Rufiji .

Ikiwa zimepita siku 33 tangu kampeni zianze rasmi, kwa upande wa Chama cha ADA-Tadea, mgombea wake wa urais, John Shibuda leo ndipo anazindua kampeni zake wilayani Maswa katika mkoa wa Shinyanga.

Vyama vyasuasua Hivi karibuni, vyama vinne vilisitisha mikutano yake ya kampeni kutokana na kile kilichoelezwa ni kukumbwa na ukata. Vyama hivyo ni NCCR-Mageuzi, Alliance for African Farmers (AAFP), Sauti ya Umma (SAU) na Democratic Party (DP).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, viongozi wa vyama hivyo walikiri kuwa walilazimika kubadilisha ratiba au kusitisha mikutano kutokana na kutafuta fedha. Jumla ya vyama 15 vimesimamisha wagombea wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi