loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Upinzani wapigia chapuo usafiri wa ndege

VYAMA vya siasa vimejinadi vitakavyoboresha usafiri wa anga kwa kuboresha viwanja vya ndege na kuhakikisha shirika la ndege linatoa huduma za ndani na kimataifa hatua inayodhihirisha kuunga mkono hatua ya serikali kununua ndege za kutosha.

Ingawa wagombea wa baadhi ya vyama wamekuwa wakibeza ununuzi wa ndege wakidai kuwa ni maendeleo ya vitu na si watu, ilani zao kuhusu usafiri wa anga pamoja na sekta ya utalii, zinabariki umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya nchi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho mgombea wake wa urais, Tundu Lissu na makada wengine wamekuwa akikosoa hatua ya serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, ilani yake inasema watahakikisha mikoa yote inapata huduma za kibishara za usafiri wa anga.

Kinasema kitahakikisha Tanzania inakuwa na shirika la ndege litakalomilikiwa kwa ubia kati ya sekta binafsi na serikali, litakaloendeshwa kibiashara kwa kuzingatia nguvu ya soko na litakalotoa huduma za usafiri za ndani na kimataifa.

“Hii itajumuisha ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege kwa viwango na ubora wa kimataifa ili kukidhi mahitaji ya sekta ya usafiri wa anga,” inasema sehemu ya ilani ya Chadema.

Kitaboresha viwanja vya ndege na kuweka maeneo maalumu ya kuhifadhi mazao ya mifugo, uvuvi na kilimo kama vile mboga, parachichi na maua kwa ajili ya kusafirisha kwenda nje ya nchi.

Chama cha Wananchi (CUF) kinasema serikali yake itakaribisha wawekezaji kutoa huduma za haraka kati ya mji na mji na kuhakikisha walau kila mkoa unakuwa na kiwanja kimoja cha ndege kinachoweza kuhudumia ndege muda wote bila kujali majira ya mwaka.

Pia kila kanda itakuwa na kiwanja cha ndege kikubwa kimoja kinachoweza kuhudumia ndege zenye ukubwa unaohitaji viwanja vikubwa.

Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta ambazo zimekuwa zikitegemea kwa kiwango kikubwa usafiri wa anga hususani kwa watalii wa nje jambo ambalo bila kuwapo ndege za kutosha, ni vigumu kutekeleza mikakati kama ilivyobainishwa na ilani za vyama ikiwamo ya kuvuta idadi kubwa ya watalii kuja nchini.

Chama cha ACT Wazalendo kinasema kitaanzisha kampeni maalumu ya kufikisha idadi ya watalii milioni tano watakaoingia nchini ifikapo mwaka 2025.

Kinakiri kuwa sekta ya utalii ina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi nchini iwapo itawekewa vivutio vya kutosha na usimamizi shirikishi kati ya sekta binafsi na serikali.

Chadema katika kuzungumzia utalii, kinasema kitaongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini, kufungua vivutio vipya vya utalii vilivyopo nchini na kuwa na ulinzi wa uhakika kwa watalii Kinasema kitaanzisha mchakato wa mashauriano na wadau kupata muafaka kuhusu maboresho ya sheria yatakayowezesha kuvutia watalii wengi kutembelea nchini kwa njia ya matangazo ya kibiashara na kuhakikisha taarifa za maeneo asili yenye vivutio, tamaduni na maeneo ya kihistoria zinawafikia kwa wakati na ufasaha.

CUF kinasema serikali itaimarisha mawasiliano ya aina zote katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ambayo kwa hivi sasa yako kwenye ukanda wa utalii. Kimesema pia kitatafuta wawekezaji zaidi kuwekeza katika huduma za watalii kama vile hoteli, usafirishaji, uandaaji wa ziara.

Kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mgombea wake wa urais, Rais Magufuli, alipohutubia mkutano wa kampeni hivi karibuni mjini Kigoma, alisisitiza kuwa ndege siyo anasa bali zina faida kubwa kwa maendeleo ya watu na uchumi wa nchi.

Alisema ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) unamnufaisha Mtanzania moja kwa moja kwa kuchangia katika shughuli za maendeleo huku akisisitiza kwamba, wanaopinga ununuzi wa ndege hizo wana mawazo yaliyopotoka.

Katika kipindi cha kwanza cha uongozi wake wa miaka mitano, serikali imenunua ndege 11 ambazo kati yake, nane zimeshawasili. Magufuli ameahidi kununua ndege nyingine tano katika kipindi kingine cha miaka mitano. “Hata hizi ndege zimetengeneza ajira… ndiyo maana tumepanga kuendelea kununua ndege zaidi…nchi zenye ndege zake ndizo zinaongoza kwa kuwa na watalii wengi,” alisema.

Akizungumza katika mahojiano na Times FM hivi karibuni, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi, alisema ndege ni ajira na zimeshaingiza zaidi ya ajira 400 za moja kwa moja.

Zimeongeza mapato ya ATCL na serikali kutoka Sh bilioni 2.5 kwa mwezi hadi Sh bilioni 15 kwa mwezi na kodi zaidi zinalipwa zinazokwenda kuhudumia wananchi.

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi