loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Corona yasababisha hospitali kufungwa

WIZARA ya Afya imechukua hatua ya kufunga Hospitali ya Wilaya ya Kapchorwa iliyoko Mmashariki mwa Uganda ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Kwa sasa Uganda ina maambukizi zaidi ya 7,000 ya virusi vya corona na vifo vikikaribia 70 kutokana na ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo.

Hospitali ya Wilaya ya Kapchorwa iliyoko mashariki mwa Uganda imefungwa baada ya wafanyakazi 19 kupatikana na maambukizi ya virusi vya corona.

Wizara hiyo imeelezea kuwa, hatua ya kufunga hospitali hiyo ni muhimu ili kuwakinga wananchi wanaokwenda kupata huduma hospitalini hapo wasipate maambukizi hayo.

Hata hivyo, kitengo cha kutoa huduma kwa wajawazito na maabara havijafungwa ili kuendelea kutoa huduma za dharura.

Wakati huohuo, Waziri wa Afya, Jane Ruth Acieng , amesema kuelekea kufunguliwa kwa shule mwezi ujao nchini humo, jitihada zinafanyika kuwapima walimu virusi vya corona.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (ECDC), John Nkengasong, ameyapongeza mataifa ya Afrika kwa kuweza kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Afrika imeshuhudia maambukizi ya corona ya watu milioni 1.4, na vifo 34,000 tangu Machi, mwaka huu. Idadi hiyo ni ndogo kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na martaifa ya mabara ya Ulaya, Asia na Amerika Kaskazini na Kusini ambayo maambukizi na vifo vipo juu.

Mlipuko wa virusi vya corona unaosababisha ugonjwa wa covid-19, kwa mara ya kwanza ulitokea katika mkoa wa Hubei, nchini China, mwishoni mwa mwaka jana.

Ugonjwa wa covid-19 huathiri mfumo wa kupumua wa binadamu na dalili zake ni homa kali na kukohoa ambako baada ya wiki moja muathirika anakabiliwa na tatizo la kupumua na hata kusababisha kifo.

foto
Mwandishi: Kampala

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi