loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mradi kuleta matumaini mapya kilimo cha bustani

KILIMO cha mazoea kinachotokana na kurithi namna walivyolima mababu kinatajwa kuwa chanzo cha kuendelea kwa ugumu wa maisha kwa baadhi ya wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Wakati maeneo mengine wakiwekeza nguvu katika kilimo cha matunda, maua na mboga, mikoa hii bado inajikita kwenye mazao hasa mahindi, ulezi na maharage.

Yapo pia mazao ya biashara ambayo yamekuwa yakilimwa kama mibuni na chai.

Hata hivyo, kuna maeneo machache mno ambayo kinaendelezwa kilimo cha bustani na pengine ndio sababu ya mikoa hiyo kuongoza kwa tatizo la utapiamlo na udumavu licha ya kuwa wazalishaji wakubwa wa chakula.

Tafsiri ya hili ni kwamba wananchi hawa wakiwemo watoto hulazimika kula vyakula vya aina moja katika kipindi cha mwaka mzima kwa kuwa ndivyo vinapatikana kwa wingi.

Kutokana na kulima mazao haya ya aina moja, soko la uhakika kwa mazao yao wakati mwingine limekuwa la kusuasua na hivyo kulazimika kuyarundika ndani wakisubiri soko.

Hapo ndipo kuna wakati utakuta familia ikilazimika kuishi muda mwingi kwa kula mahindi ya kuchoma, kuchemsha au kukaanga. Hata hivyo, mabadiliko yanaweza kupatikana kupitia elimu mbalimbali zinazoendelea kutolewa na wadau wakisaidiana na Serikali.

Ni katika muktadha huo, wananchi, hususani vijana katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kuchangamkia fursa ya uwanja mkubwa wa ndege wa Songwe kwa kuwekeza katika kilimo cha mazao ya bustani.

Hii ni kulenga kwamba kipindi ndege kubwa za mizigo zitakapoanza kutua na kupeleka mazao nje ya nchi wawe pia na kitu cha kuuza nje.

Ofisa Kilimo Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Merius Nzalawahe anatoa ushauri huo alipofunga mafunzo ya wiki mbili ya mbinu bora za kilimo cha mazao ya bustani kwa watoa huduma binafsi 50 kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi (LSPs).

Mafunzo hayo yaliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI-Uyole) kwa kushirikiana na Chuo cha kilimo Tengeru (HORTI Tengeru).

Watoa huduma hao binafsi ni miongoni mwa watoa huduma 100 watakaopewa mafunzo hayo ambao nao watatumika kutoa elimu na kuwaongoza wakulima wa kilimo cha mazao ya bustani kwenye maeneo yao kupitia mradi wa kilimo bora cha mboga na matunda (Kibowavi).

Mradi huo umeandaliwa na Shirika la Helvetas Tanzania kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya.

Nzalawahe anasema wakati serikali ikiendelea na jitihada za kuuimarisha uwanja wa Songwe ili ndege kubwa na za kimataifa ziutumie si wakati wa wakazi wa mikoa hiyo kubweteka bali waige utaalamu kutoka kwa wenzao wa ukanda wa Kaskazini.

Anasema wakulima katika kanda hiyo wanaoutumia vyena uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kusafirisha mazao ya mboga, matunda na maua kwenda nje ya nchi na kujipatia kipato kikubwa.

Anawataka wananchi kuchangamkia fursa za miradi yenye kutoa utaalamu wa kilimo cha mazao ya bustani ili kuwajengea msingi wa kuanza kujikita kwenye mazao hayo aliyosema yana faida kubwa kiuchumi zaidi ya yale ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele kwa muda mrefu.

“Ni muhimu mkatambua kuwa mazao ya bustani yana faida kubwa zaidi ya yale ambayo kwa miaka mingi tumekuwa tukiyahangaikia mpaka tukayawekea na Bodi.

Utasikia kuna bodi ya zao la chai, kahawa, pamba na kadhalika. Lakini kwa sasa mazao hayo faida yake hauwezi kulinganisha na ya bustani. Huku unatumia eneo dogo kwa kipato kikubwa.

“Hatusemi mkakate mibuni au chai na kulima bustani… Nayo yana umuhimu wake. Lakini tambueni wenzenu wa Kaskazini wameendelea kwa kutumia kilimo cha bustani na uwepo wa uwanja wa KIA.

Sasa kama serikali imewajengea miundombinu kama uwanja wa Songwe kwa nini tuendelee kuishi maisha magumu?” Anahoji Nzalawahe.

Ofisa kilimo mkuu huyo anawataka wahitimu wa mafunzo hayo kutokuwa wachoyo watakapokuwa kwenye maeneo yao bali waisambaze elimu waliyoipata ili jamii yote inayowazunguka iweze kunufaika na kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Anataja uwepo wa mazingira rafiki kwa kilimo ikiwemo ardhi yenye rutuba na yenye kutosheleza, hali ya hewa nzuri na maji kuwa chachu ya kuwezesha mpango mkakati wa kilimo cha bustani kunafanikiwa kwenye mikoa ambayo mradi wa Kibowavi utatekelezwa kwa miaka minne.

“Sisi Tanzania tuna bahati kubwa... Tuna hali ya hewa inayoruhusu kulima mwaka mzima. Tuna ardhi inayofaa siyo mpaka uhangaike kama mataifa mengine ambayo ardhi yake mpaka uihangaikie sana katika kuirutubisha ndipo mmea uote.

Tunayo maji karibia katika kila eneo. Tanzania tunao uwezo wa kuzalisha mazao yote yanayozalishwa duniani,” anasema. Anaendelea: “Niliwahi kwenda hapo Njombe nikakuta kuna mkulima mmoja ametelekeza shamba lake la matufaa.

Yaani pamoja na kutolipalilia wala kupiga dawa lakini yamepamba kwelikweli.” Anasema kwa wakulima wa tifaa wa Afrika Kusini wanalazimika kuchimba mashimo makubwa, kuweka mbolea na dawa kwenye udongo na wengine wanalazimika kununua udongo mbali ndipo waweze kupanda mche. “

Tuna hali ya hewa nzuri mpaka watu wanaacha nchi zao kuja kuzalisha huku kwa kuwa makwao kulima mazao kama maua pia ni gharama kubwa mno ikilinganishwa na hapa kwetu,” anaongeza.

Anawataka pia watanzania kutambua kuwa faida za kilimo cha bustani zipo kiuchumi na kiafya. Anasema katika mwaka wa fedha uliopita mazao hayo yalikuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa ukilinganisha na mazao mengine.

“Lakini pia tunaambiwa mazao yote ya bustani yana viinilishe vingi. Ukizungumzia matunda, viungo kama nyanya, vitunguu, karoti, mboga na vingine vingi vyote ni muhimu kwenye mwili wa binadami kiafya.

Na ndiyo sababu soko la dunia halijawahi kutoshelezwa na mazao ya bustani kwa kuwa yana mahitaji ni makubwa na si nchi zote zinaweza kuyazalisha,” anasema.

Jukwaa la Lishe Tanzania, limekuwa likisema kwamba Watanzania wengi hawana shida ya virutubisho vya protini na wanga katika miili yao bali vitamini mbalimbali na madini, vitu vinavyopatikana kwa wingi kwenye matunda na mboga.

Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi wa Mradi wa Kibowavi kutoka Shirika la Helvetas, Daniel Kalimbiya anasema Umoja wa Ulaya unagharamia kwa asilimia 90 mradi huo.

Kalimbiya anawataka wahitimu hao kwenda kutoa elimu waliyoyapata kwa wakulima katika maeneo yao ili kuondokana na kilimo cha mazoea.

“Mkawafundishe pia wananchi kutambua kuwa hata lishe bora si kula tu mboga za majani kila siku. Wajifunze pia kufuga mifugo kama kuku, bata na sungura ili viwasaidie kuboresha milo yao wakati wakiendelea na shughuli za bustani.

“Tunategemea wewe uliyejifunza ukawe chanzo cha mabadiliko na siyo utakaowafundisha wabadilike wewe ubaki palepale. Yaani unahimiza kilimo cha bustani katio wewe mwenewe hauna,” anasisitiza.

Mkurugenzi huyo anasema pamoja na kuwafuatilia kwa karibu ili kujionea watakayokuwa wanayafanya kwenye vikundi vyao, shirika kupitia mradi huo litakuwa linatoa ruzuku kwa vikundi vitakavyokuwa vinafanya vizuri ili kutoa motisha kwa wqengine.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Mboga, Matunda na Maua Arusha (HORTI- Tengeru), Juma Shekidele anasema yapo mafanikio makubwa waliyoyapata wakazi wa mikoa ya Kaskazini hususani Arusha na Kilimanjaro kupitia kilimo cha bustani.

Hii anasema ilichagizwa na uwepo wa chuo cha Tengeru ambacho kimekuwa kikiibua wataalamu wanaoshirikiana na wakulima kuzalisha kwa tija. “Matarajio yetu ni kuona mikoa hii ya Nyanda za Juu Kusini na yenyewe inaanza kuneemeka sasa baada ya mradi huu.

Sisi Tengeru tuko tayari kushirikiana na wakulima mikoa ya huku kama tunavyofanya kule kwetu. Kwa kuwa tuna uzoefu msisite kututumia kama mlivyotutumia kwenye mafunzo haya. Sisi tuna uzoefu wa zaidi ya miaka arobaini,” anasema Shekidele.

Dk Ndabhemeye Miengera ni Mratibu wa Utafiti na Ubunifu TARI-Uyole.

Anasema hatua ya mradi huu kuwapa kipaumbele vijana inaufanya kuwa endelevu zaidi kwa kuwa vijana wanao muda mrefu wa kuitumikia jamii.

Ushiriki wa wanawake pia anasema una tija kwa kuwa ni kundi ambalo mara nyingi linapojifunza elimu husambaa zaidi na mafanikio huonekana tofauti na ukiwafundisha wanaume pekee.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Benard Ntui kutoka mkoani Songwe anasema: “Tumejifunza vitu vingi na tuna deni la kulipa kwa jamii na deni hilo kila mmoja atalilipa kwa nafasi yake. Tunakwenda kushiriki kuinua vijana na wanawake kiuchumi.

Kwa pamoja tunaweza kwani tayari hapa pia tumeanzisha msingi wa mawasiliano kati yetu washiriki, wakufunzi na wadau wengine.”

Mradi wa Kibowavi unatarajiwa kuwafikia wakulima wadogo 75,000 katika kaya 15,000. Mhitimu wa mafunzo ya wiki mbili juu ya mbinu bora za kilimo cha mazao ya bustani kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe na Katavi akipokea cheti.

KESHOKUTWA Watanzania wanapiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Wagombea waliokuwa ...

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi