loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mgombea urais Ada Tadea kufuata nyayo za Shein

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib amesema akichaguliwa kuwa rais, anakusudia kufuata nyayo za Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ambayo lengo lake kubwa ni kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.

Khatib alisema hayo wakati akizindua kampeni za chama chake katika Viwanja vya Magaeni Sogea Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema miradi yote muhimu iliyobaki, ambayo imesimamiwa na Rais Shein anakusudia kuimaliza ili kuunga mkono kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.

‘’Nikichaguliwa kuwa rais wa Zanzibar nakusudia kutekeleza miradi yote muhimu ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri iliyopo Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na nitajenga Uwanja wa Ndege wa Karume uliopo Pemba ili kuruhusu kuweza kutua ndege kubwa na kuongeza idadi ya watalii,’’ alisema.

Khatib ambaye ni Waziri asiye na Wizara Maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) alimshukuru Dk Shein kwa kumteua katika baraza la mawaziri na hivyo kupata uzoefu wa hali ya juu wa uongozi.

‘’Namshukuru Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa kuniteua kuingia katika Baraza la Mawaziri na hivyo kupata uzoefu mkubwa wa uongozi,’’ alisema.

Aidha, alisema akichaguliwa kuwa rais anakusudia kufufua eneo la viwanda vidogo vidogo lililopo Amani, kwa ajili ya kuzalisha ajira nyingi za vijana na kurudisha enzi ya Zanzibar ya kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Kwa mfano, alisema katika miaka ya 1980, Zanzibar ilikuwa maarufu kwa kuwa na viwanda vidogo vya aina mbalimbali ikiwemo masufuria, sabuni, waya za umeme, mafuta ya nazi na bidhaa nyingine za kusafirisha nje ya nchi.

‘’Mimi nilibahatika kufanya kazi katika shirika la viwanda vidogo vilivyopo Amani, tulikuwa tukizalisha bidhaa mbalimbali na kuifanya Zanzibar kusafirisha nje ya nchi,’’ alisema.

Mapema, Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Ada Tadea, Hassan Kijogoo alisema wanakusudia kuifanya Zanzibar kuwa lango kuu la uchumi, kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali hadi katika visiwa vya Ngazija.

‘’Tukichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano chini ya mgombea John Shibuda tunakusudia kuifanya Zanzibar kuwa lango kuu la kiuchumi kwa kutumia fursa ziliopo nchi jirani, ikiwemo Comoro na Mombasa, Kenya’’ alisema

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi