loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mashirika, Wakala waagizwa bajeti kielektroniki

NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga  amemuagiza Msajili wa Hazina, kutochambua bajeti yoyote ya mwaka 2021/2022, itakayowasilishwa nje ya mfumo wa uandaaji na uwasilishaji wa bajeti na taarifa za bajeti kielektroniki (PlanRep).

Mary alitoa agizo hilo jana jijini Dodoma wakati wa kufungua mafunzo ya matumizi ya mfumo mpya wa uandaaji na uwasilishaji wa bajeti na taarifa za bajeti kielektroniki (PlanRep) kwa wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma.

Alisema hadi Juni mwaka 2019, serikali ilikuwa imewekeza katika taasisi, mashirika na kampuni zinazomilikiwa na serikali kwa hisa chache zipatazo 266 zenye uwekezaji wa kiasi cha Sh trilioni 59.6 hivyo kuihitaji usimamizi wa karibu kupitia mifumo ya kiletroniki.

“Mashirika haya ni mengi na uwekezaji ni mkubwa unaohitaji usimamizi madhubuti utakaowezesha ongezeko la tija katika ukuzaji wa uchumi na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ili kuwezesha ufanisi katika usimamizi wa mali za umma, ilihitajika mifumo madhubuti ya kielektroniki itakayorahisisha usimamizi wa rasilimali hizo.”alisema Mary

Alisema uwepo wa mifumo hiyo utapunguza upotevu wa mapato, kuimarisha na kuchochea uwajibikaji, kuimarisha uchambuzi wa bajeti na ufuatiliaji na hatimaye kuongeza mapato katika mfuko mkuu wa serikali.

“Hivyo basi, mfumo huu wa PlanRep utakuwa kitendea kazi muhimu cha Ofisi ya Msajili wa Hazina na naamini hata wizara na taasisi nyingine za serikali kuu zitaweza kutumia mfumo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato.”alisema Mary.

Aliwaagiza watendaji wakuu wa wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma wote kusimamia matumizi ya mfumo huo katika taasisi wanazozisimamia.

“Pia nitoe maelekezo mahsusi kwa maafisa masuuli wote wa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhakikisha kuwa, mpango na bajeti kwa mwaka 2021/22 unaandaliwa na kuwasilishwa kupitia mfumo huu wa PlanRep.”

Awali, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina ikishirikiana na Ofisi ya Rais- Tamisemi na Wizara ya Fedha na Mipango ilianzisha mradi wa kusimika mfumo wa PlanRep ili kuhakikisha serikali inanufaika na uwekezaji inaoufanya na taasisi hizi kuchangiza ipasavyo katika ukuaji wa mapato ya serikali.

Alisema kuwa mfumo huo wa bajeti, ulishaanza kutumika na mamlaka za serikali za mitaa tangu mwaka 2017/18, na iliamuliwa kuuboresha ili uweze kutumika na kila taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi