loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM apania kutengeneza mabilionea watanzania

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amesema ndoto yake ni kutengeneza uchumi wa Tanzania, utakaovutia watanzania wenyewe kuwa wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali na kuwa mabilionea.

Amesema huu ni wakati wa Tanzania kutoka kwenye mawazo ya kuwa na uchumi tegemezi, na pia kutoka kwenye mawazo ya kubebwa na kutegemea fedha za kuletewa.

“Tunataka uchumi wa Watanzania, tunataka mabilionea Watanzania,” alieleza jana Rais Magufuli, alipohutubia mkutano wake wa mkubwa kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Alitumia muda mwingi wa hotuba yake hiyo ya kuanza rasmi awamu ya tatu ya kampeni, kuelezea Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Akielezea Ilani hiyo, Rais Magufuli alisema ilani hiyo yenye kurasa 303, imelenga kuendeleza juhudi za kujenga taifa kwa kujitegemea na kutumia rasilimali zilizopo.

Aliwaambia maelfu ya wananchi kuwa Tanzania ni nchi tajiri kwa sababu imejaliwa rasilimali za kila aina kama vile gesi, misitu, madini, malikale, wanyama na hifadhi, ardhi yenye rutuba, mito, mabwawa, maziwa na bahari. Pia inafursa za kijiografia kibiashara, ambazo endapo zitatumiwa vizuri, itajikwamua zaidi kiuchumi.

Akirejea ilani hiyo kuanzia ukurasa wa tisa hadi 124, alisema imeeleza kuwa Serikali ya CCM itaendeleza juhudi za kuleta mapinduzi ya uchumi na maendeleo ya watu wa kada mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, madereva, wavuvi na wafanyakazi.

“Mfano miaka mitano ijayo tutakuza uchumi kwa wastani usiopungua asilimia nane. Miaka mitano iliyopita tumetoka kwenye uchumi wa kutupwa hadi tumeingia kwenye uchumi wa kati,” alieleza Rais Magufuli, anayeomba muhula wa pili wa miaka mitano.

Alisema wakati dunia nzima watu hawaendi kazini, hawaendi shambani, madukani, sokoni, kampuni na maofisi yamefungwa na watu wakifunika mdomo kwa sababu ya corona, Tanzania kwa uwezo wa Mungu ilijipanga vyema na kuingia yenyewe kwenye uchumi wa kati.

“Kama mtaichagua CCM, uchumi wa sasa unaokua kwa asilimia saba utakuwa asilimia nane.Na hili lipo kwenye ilani hii ambayo ndio mkataba wa serikali na wananchi,” alieleza.

Alisema ilani hiyo imeeleza katika eneo la ajira kuwa miaka mitano ijayo, serikali itamwaga ajira milioni nane, ambapo miaka mitano iliyopita ilitoa ajira zaidi ya milioni sita.

Alieleza namna ajira zitakavyotengenezwa kuwa ni kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa zahanati, hospitali, vituo vya afya, barabara, miradi mikubwa kama Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji.

“Tumejenga vituo vya afya 487, ajira zilipatikana kwa waliokuwa wanajenga, wanaopeleka saruji, misumari, kokoto, lakini pia tulinunua ndege 11 hii nayo ni ajira kwani marubani zaidi ya 500 waliajiriwa. Tumejenga barabara zaidi ya kilometa 3,000 makandarasi zaidi ya 8,500 waliajiri watu, hizo zote ni ajira,” alifafanua Rais Magufuli.

Alisema miradi mikubwa ya maendeleo kama SGR, tayari ilishatoa ajira zaidi ya 10,000 na Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ajira zaidi ya 10,000. Viwanda vilianzishwa zaidi ya 8,844 zote ni ajira, alieleza.

Alisema kwa mujibu wa ilani hiyo, pia watafanya mageuzi kwenye sheria, kanuni, kodi na tozo kwa kuzingatia muongozo wa kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Alisema wamepanga kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha, kwa kuanzisha programu maalumu na kuhamasisha vijana, wanawake na makundi mengine, kujiunga kwenye makundi na kupatiwa elimu ya ujasiriamali ili wajiajiri au kuajiriwa.

Alisema ili kuhakikisha hilo, Ilani hiyo imeweka mpango wa kuanzisha programu au mifuko zaidi ya 20 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, ambayo baadhi yake ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi za Nordic (NDF).

Alisema pia ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa maendeleo ya watu, kupitia Ilani hiyo ya CCM, wamejipanga kutoa ajira nyingi kwa wananchi kupitia viwanda na sekta nyingine.

“Viwanda ni sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kutengeneza ajira na kuinua pato la wananchi. Tunataka hata Ulanzi ukauzwe hadi Afrika Kusini, mbona Amarula inaletwa huku,” alisema na kuongeza kuwa watajenga ukanda wa viwanda ili viwanda vingi vizalishwe.

Alisema lengo la mpango huo ni kuongeza kasi ya ukuaji uchumi wa nchi, ambapo kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 za Afrika zenye uchumi unaokua kwa kasi.

Alisema katika kuendeleza uchumi wa viwanda, lazima nchi iwena bandari pamoja na bandari kavu, ndio maana katika kipindi cha kwanza Serikali ya Awamu ya Tano ilitumia Sh trilioni 1.5 kufufua bandari za Mtwara na Tanga.

Alisema kwa upande wa kilimo, ilani hiyo imelenga utekelezaji katika kuongeza tija na uzalishaji ili kujihakikishia usalama wa chakula, lakini pia kutumika kama rasilimali kwa viwanda.

Alisema pia watashughulikia na masuala ya mbolea, mbegu bora, dawa na matrekta vipatikane kwa uhakika na bei ya chini. Pia kuongeza miundombinu ya umwagiliaji na kufikia hekta milioni 1.2 ifikapo mwaka 2025 ili kupunguza utegemezi kwenye mvua.

Alisema pia wataimarisha mifumo ya upatikanaji mitaji, bima na kuhamasisha watu waanzishe viwanda vidogo inavyohudumiwa na sekta ya kilimo.

Katika mifugo kwa mujibu wa ilani hiyo, alisema sekta hiyo itaongezewa eneo la ufugaji kutoka la sasa milioni 2.7 hadi hekta milioni sita kabla ya mwaka 2025. Mifugo yote itapatiwa chanjo na chanjo 13 za kipaumbele zitatolewa bure, huku kila wilaya itakuwa na daktari wa mifugo, kila kata daktari msaidizi na kila kijiji kuwa na josho.

Akielezea uvuvi, alisema wamepanga kujenga bandari za uvuvi kwenye ukanda wa pwani na ajira 30,000 zitapatikana. Zitanunuliwa meli tano za uvuvi na wavuvi wadogo watahamsishwa kujiunga kwenye vikundi, wapate vifaa na mitaji.

Alisema katika madini, hatua zimeanza kuchukuliwa, kuimarisha udhibiti na usimamizi wa uchimbaji mkubwa ili kuinufaisha nchi, ambako ilipitishwa sheria ya kufanya madini ni mali ya Watanzania na si mali ya kuibwa.

“Fedha zinazopatikana kwenye madini ni mabilioni ya fedha hususani pale Mirerani, inatufanya Watanzania tutembee kifua mbele, Tanzania sasa imeanza kujitegemea. Tutaendeleza madini yawe mali ya Watanzania,” alisema.

Alisema katika utalii, ilani hiyo inaelekeza kuongeza watalii kutoka milioni 1.5 wa sasa hadi milioni tano kwa mwaka, na kuongeza mapato kutoka dola za Marekani bilioni 2.6 hadi dola za Marekani bilioni sita.

“Ndio maana tumetangaza mbuga na hifadhi nyingi, lakini pia tumenunua ndege, hii ni kwa sababu jamani watalii hawaji nchini kwetu kwa bajaji wanatumia ndege na nchi kuwa na ndege zake ni kichocheo muhimu cha kuongeza utalii,” alisema.

Alieleza kuwa serikali yake itahakikisha mipango na mikakati yote iliyoanishwa kwenye ilani inafanywa kwa kushirikiana na sekta binafsi ambako katika awamu ya kwanza ya miaka mitano mitaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 14 ilisajiliwa.

Katika miundombinu, alisema katika miaka mitano iliyopita walijenga kilometa 1,716 za barabara za lami, na miaka mitano ijayo wanatarajia kuanza ujenzi wa lami kilometa 6,000, ukarabati mkubwa wa madaraja saba, na madogo 14.

Lakini pia alieleza kuwa wanatarajia kujenga meli mpya na ukarabati wa meli za ziwa Victoria na meli mpya ya kuhudumia bahari ya Hindi itakayoenda hadi visiwa vya Comoro.

“Tutanunua vichwa vya treni 58, behewa 800 za mizigo na mabehewa 37 ya abiria. Injini saba katika reli yaTazara zitakarabatiwa na viwanja vya ndege 16 vitakarabatiwa na ndege tano zitanunuliwa,” alisema mgombea huyo.

Katika afya, aliafanua ilani hiyo inaelekeza kujenga zahanati zaidi, vituo vya afya na kukamilisha kujenga hospitali za wilaya 99 na kuongeza watumishi wa afya.

Aidha, alisema ilani hiyo pia ukurasa unaozungumzia mpango wa ulinzi na usalama kwa kuwa kamwe huwezi kuzungumzia maendeleo ya wananchi bila kuzungumzia amani.

Alisema kupitia mpango huo vyombo vya ulinzi na usalama vitaboreshwa na kuongezewa vifaa vya kisasa na mafunzo zaidi yatatolewa.

Mgombea huyo wa CCM alisema pia ilani hiyo inaeleza kuhusu suala la kulinda haki na Katiba, ambapo suala la demokrasia limepewa kipaumbele.

Alisema pamoja na mipango na mikakati hiyo iliyomo kwenye ilani ikiwemo inagusa pia masuala ya burudani, michezo na utamaduni, akipewa ridhaa atatekeleza mengi zaidi hata kama hayamo kwenye ilani hiyo.

Alisema mwaka 2015 alipochaguliwa alitekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020, lakini kuna mambo mengine makubwa aliyatekeleza ambayo hakuwepo kwenye ilani hiyo.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni ununuzi wa ndege 11, ujenzi wa Bwawa la Nyerere, ujenzi wa Reli ya Kisasa, kukarabati treni ya Dar es Salaam  hadi Arusha na kukarabati meli zaidi ya tano Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

“Haya yaliyomo kwenye ilani ya uchaguzi yenye kurasa 303 tutafanya zaidi. Nataka muamini kwa sababu tuna uzoefu wa kufanya zaidi. Tupeni nafasi tukafanye maajabu nchi nzima,” alisema.

Aidha, katika mkutano huo, Mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Mizengo Pinda alieleza mbele ya mgombea huyo mikakati ya ushindi katika mkoa huo, na alimhakikishia kuwa safari hii chama hicho kinapata ushindi asilimia 100 mkoani humo kwa ubunge na udiwani

Watanzania 4,247 wamepata ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi