loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

NEC yathibitisha kumwita Lissu, agoma

WAKATI Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akisema hatarajii kuacha kampeni kuitikia mwito wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa kuwa hana barua ya kuitwa, tume hiyo imethibitisha kumuandikia barua rasmi ya kumtaka afike bila kukosa katika ofisi hizo.

Juzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Willson Mahera alizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha na kumtaka Lissu afike leo mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Maadili kutoa ushahidi wa kauli yake kuwa Rais John Magufuli amekutana na wasimamizi wa majimbo yote ya uchaguzi jijini Dodoma kati ya Septemba 25 na 26 mwaka huu.

Lissu jana katika ukurasa wake wa Twitter aliandika, “Sijapokea malalamiko yoyote juu ya jambo lolote linalohusiana na kampeni za Uchaguzi Mkuu huu kutoka NEC. Sijapokea wito wowote kuhusu jambo lolote linalohusiana na kampeni za Uchaguzi Mkuu huu kutoka NEC. Sitarajii kuacha kampeni ili kuitikia wito wa mitandaoni wa mtu yeyote!”.

Gazeti hili lilizungumza jana kwa simu na Dk Mahera, kutaka kujua ikiwa walitumia utaratibu rasmi wa kiofisi kumwita Lissu.

Dk Mahera alisema utaratibu huo umefuatwa,kwa kuzingatia misingi stahiki, na Lissu amepelekewa barua hiyo, ingawa alisema hana uhakika kuhusu tarehe aliyoandikiwa afike ofisi za NEC kwa kuwa yeye hakuwepo ofisini wakati huo.

Juzi Dk Mahera alinukuliwa na vyombo vya habari, akisema Lissu anapaswa kufika ofisi za tume leo.

“Hatuwezi kujibizana na mtu kwenye mitandao au magazeti, ninachojua ni kwamba utaratibu wa ofisi umechukuliwa. Kama ni kesho (leo) au siku nyingine waliyoona nzuri zaidi sijui maana sipo ofisini, ila najua wamemuandikia barua,” alisema Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi wa NEC.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Dk Mahera alisema Septemba 26, mwaka huu Lissu akiwa Musoma mkoani Mara katika mikutano ya kampeni, alisema Rais Magufuli Septemba 25 na 26, mwaka huu aliitisha kikao Dodoma na kukutana na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote.

Alisema mbali ya hilo, Septemba 25, mwaka huu, Lissu alisambaza taarifa mitandaoni zikisema Rais Magufuli alifanya kikao na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi mjini Dodoma.

Dk Mahera alisema siku zilizotajwa na Lissu, alikuwa katika ziara za kikazi kukagua na kuratibu maandalizi ya uchaguzi katika majimbo ya mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro na mikoa mingine alikopita amekutana na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao ya kazi.

Alisema kutokana na hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa taarifa zilizotolewa na Lissu zina lengo baya kwa nchi na halitakubalika.

Dk Mahera alisema NEC inawasihi wagombea wa vyama vyote kufuata sheria, kanuni na utaratibu wa nchi ili kulinda amani katika kipindi cha kampeni kilichobaki kwa kujali muda wa kampeni, ratiba ya kampeni na kuepuka matusi na kutoa tuhuma zisizo na ushahidi.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi