loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tusitukane, tueleze sera -JPM

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amewataka wanachama wa chama hicho kuwa watulivu na kufanya kampeni za kistaarabu, zinazowaeleza watu sera na mikakati ya kuwaletea maendeleo, badala ya matusi.

Alisema hayo jana alipohutubia wananchi katika mikutano mbali mbali ya kampeni, aliyoifanya mkoani Njombe akiwa njiani kwenda mkoani Mbeya.

“Nawaomba CCM tuwe watulivu, tufanye kampeni za ustaarabu, tusitukane mtu yeyote, tuwaeleze watu sera na mikakati ya kuleta maendeleo nchini, hayo ndio watu wa Njombe na Watanzania wanataka kusikia,” alisema Magufuli

Pia, Rais Magufuli aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama, vichunguze mauaji ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Vyuo Vikuu mkoani Iringa, Emmanuel Mlelwa na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Magufuli alisema amehuzunishwa na tukio hilo na aliwapa pole familia na wananchi wa mkoa wa Njombe. “Namuomba Mungu ampumzishe pema peponi na naomba wafiwa muwe na moyo wa uvumilivu.

Naagiza vyombo vya ulinzi na usalama vichunguze hili ili kubaini ukweli na kuwafikisha wahusika wote kwenye vyombo vya sheria” aliagiza.

Jeshi la Polisi limesema watu 120 wakiwamo wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Mlelwa, wamekamatwa kwa tuhuma za matukio mbali mbali ya kihalifu na baadhi yao wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah aliliambia gazeti hili juzi kuwa watu watano wakiwamo viongozi wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanashikiliwa na Polisi juu ya tuhuma za mauaji hayo.

Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Thadeus Mwanyika ambaye ni mgombea udiwani Kata ya Utalingolo (Chadema), George Sanga pia mgombea udiwani Kata ya Ramadhani (Chadema), Optatus Mkwera ambaye ni Katibu Mwenezi Kata ya Ramadhani (Chadema) na Godluck Mfuse ambaye ni dalali wa magari ya mizigo Njombe.

Alisema Mlelwa alipotea Septemba 20, mwaka huu baada ya kutafutwa bila mafanikio na Septemba 24 mwili uliokotwa Kibena na ndugu zake walimtambua Septemba 26.

Katika uchunguzi wa awali, Polisi ilikuta mkanda wa marehemu katika gari Toyota Gaia yenye namba za usajili T457DAB linalodaiwa kuwa ni mali ya mtuhumiwa Sanga.

Katika hatua nyingine, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Liberatus Sabas katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana katika Makao Makuu ya Polisi Dodoma, alisema nchi iko shwari wakati huu wa kampeni na watu wachache wanaofanya uhalifu, wanawashughulikia kwa mujibu wa sheria.

“Mtakumbuka mnamo tarehe 21/09/2020 kulijitokeza tukio la mauaji katika maeneo ya Bwawa la Kibena Estate wilaya na mkoa wa Njombe, ambapo Emmanuel Mlelwa (25), mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, aliuawa na wahalifu ambapo mpaka sasa watu wanne wanashikiliwa huku uchunguzi zaidi ukiendelea,” alisema Sabas.

Alisema katika tukio hilo na mengine yaliyotokea, kwa juhudi za Polisi na ushirikiano wa wananchi, watuhumiwa 120 wamekamatwa na baadhi wamefikishwa mahakamani na wengine ziko katika hatua za mwisho ili wafikishwe kortini.

Sabas alisema pamoja na hatua hiyo, changamoto wanazokutana nazo ni baadhi ya wagombea kutofuata ratiba ya kampeni iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema jambo ambalo ni kosa kulingana na kanuni za maadili. Alisisitiza kuwa kamwe Polisi haitamuonea muhali mtu yeyote, atakayekwenda kinyume na sheria za nchi.

“Aidha, Jeshi la Polisi linalaani vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wagombea na wafuasi wao kwa kutoa lugha za matusi, uzushi na uongo na kashfa kwa wagombea wengine ikiwa ni pamoja na kupandikiza chuki kwa wananchi ili waone serikali haitendi haki pamoja na kuchana bendera na picha za wagombea wengine,” alisema Sabas.

WASIMAMIZI wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi,wameonywa kujiepusha na ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi