loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wakubaliana kilimo biashara kuongeza masoko na tija

Wakubaliana kilimo biashara kuongeza masoko na tija

WIZARA ya Kilimo imesaini mkataba wa makubaliano na taasisi ya Building Rural Incomes Through Entrepreneurship (Briten) kuhusu kuendeleza sekta ya kilimo kwa kufanya kilimobiashara na kuongeza upatikanaji wa pembejeo na masoko kwa wakulima.

Makubaliano hayo yanahusisha kuimarisha ujuzi wa biashara kwa wakulima wadogo ili kufanya kilimobiashara na kuimarisha uwezo wa kutunza mazao kabla na baada ya mavuno ili kupunguza upotevu na kuongeza tija.

Mkataba huo wa makubaliano umesainiwa juzi baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Briten, Josephine Kaiza, jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa utiaji saini, Kusaya alisema mkataba huo utasaidia wizara kutumia fursa ya kuongeza ujuzi wa wakulima kufanya kilimobiashara, matumizi ya teknolojia na kuwapatia wakulima mbinu bora za kuongeza kipato.

“Eneo lingine la ushirikiano ni kutoa huduma za upatikanaji habari, pembejeo na kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa wakulima wadogo kutumia tafiti na uvumbuzi wa teknolojia mpya za kilimo,” alisema.

Kusaya alieleza mkakati wa wizara kuhakikisha inapima sampuli za udongo katika wilaya zote nchini ili kuwasaidia wakulima na wawekezaji kujua virutubishi gani na aina ipi ya mbolea au zao la kupanda.

Alisema tayari Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Selian cha Arusha kimekusanya sampuli za udongo kutoka kata zote 3,956 za Tanzania Bara ili kujua aina gani ya zao inastahili wapi na mbolea gani ya kutumia ili kuwa na uhakika na kilimo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Briten, Kaiza alisema taasisi yao imebobea katika kutekeleza miradi ya kilimo biashara na kutengeneza ushindani wa kibiashara kwa kuwafundisha wakulima mbinu za uzalishaji bora wa mazao.

Alitaja taasisi hiyo imeongeza muunganiko wa wadau wa sekta ya kilimo kufanya kazi pamoja na kugusa maisha ya wakulima 165,000 katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Taasisi ya Briten imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo kwa takribani miaka 10 na kupitia makubaliano na wizara ya kilimo wataendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Pili wa Ukuzaji Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e6cc2e4c11ca599d9436926d51148167.jpg

Sehemu kubwa ya ulimwengu wa biashara uli dorora kutokana na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi