loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mfumo jike unavyotawala maisha ya tembo

S IYO rahisi kuongelea utalii wa Tanzania bila kuwataja wanyamapori wetu wapatikanao kwenye mbuga zetu, hasa wale wa kundi la ‘Big 5’ ambao ndiyo kivutio kikubwa cha wageni nchini kwetu.

Simba, tembo, chui, kifaru na nyati ndiyo wanyama wanaounda kundi la wanyama watano wakubwa na neno hilo liliundwa na wawindaji wakijumuisha wanyama ambao ni wagumu kuwawinda wakiwa mbugani kwa mguu.

Kwa bahati mbaya, tembo ndiye mnyama anayewindwa zaidi na majangili kutokana na uhitaji wa ndovu zake kwenye masoko haramu nje ya nchi na katika muktadha huo, jitihada za dhati zinaendelea kufanywa ili kutokomeza ujangili.

Tanzania ina jumla ya idadi ya tembo wasiopungua 51,000 na umati wote huu unatawaliwa na ufalme wa kike.

Akiwa na uzito usiopungua tani sita ambao ni sawa na uzito wa Toyota Coaster iliyobeba abiria ‘levo siti’, tembo ndiye mnyamapori mkubwa zaidi kuliko wote ardhini na wanapatikana bara la Afrika na Asia tu huku maeneo mengine wakiishi kama mateka au kwa kufugwa kwenye taasisi maalumu.

Tembo wa Afrika ana masikio makubwa kuliko wa Asia na pia ana kichwa cha duara mithili ya yai huku tembo wa Asia akiwa na kichwa kilichokaa kama duara pacha kikielekea kufanana na kopa. Tembo hao wa Asia pia wana manyoya kidogo utosini.

Tembo wa Asia ana mgongo mbonyeo ambao humfanya aweze kutumika na binadamu kama usafiri huku tembo wa Afrika akiwa na mgongo mbinuko. Mara nyingi tembo dume na jike wa Afrika wana ndovu (meno) ila kwa upande wa tembo wa Asia, ni madume pekee ndiyo wenye ndovu.

Afrika tuna tembo wa misituni na wa tambarare ambao ndiyo wenye miili mikubwa zaidi. Wengi wakiwa na urefu wa zaidi ya futi kumi na hivyo kumzidi binadamu kwani binadamu mrefu kuliko wote duniani, Robert Wardlow ana urefu wa futi nane na inchi 11.

Tembo huishi katika koo na ukoo mmoja unaweza kuwa na tembo kuanzia wanane hadi mia moja na idadi kubwa ya wanafamilia wa koo hizi huwa ni majike yaani bibi, mama, shangazi, dada na mawifi na madume wadogo ambao wote huongozwa na tembo jike mzee kuliko wote.

Tembo hubeba ujauzito kwa miezi 22 na huzaa ndama wa tembo mwenye kilo zaidi ya mia.

Tembo anapozaliwa, mama yake humfundisha na humfanyia kila kitu, humlisha, humlinda, humuogesha, humkinga na jua na humsaidia kutembea mpaka atakapoweza kujitegemea na ndiyo maana mara nyingi utaona ndama wa tembo akitembea huwa chini ya tumbo la mama yake.

Kuna tendo la tembo kujipodoa, tendo hili huhusisha tembo kutumia mkonga wake kujimwagia tope na mchanga mgongoni mwake na anaweza pia kumfanyia ndama wake ili kuikinga ngozi yake na jua kali.

Kazi hii ya kulea ndama haifanywi na mama peke yake, kuna mashangazi na madada ambao pia huweka mchango wao kwenye malezi ya huyu kinda ingawa kama ni dume, baada ya kufikia umri wa balehe hutoweka kwenda kujitegemea lakini kama ni jike basi ni nadra sana kuiacha familia yake.

Ndama wa tembo anapokuwa hatarini hupata msaada kutoka kwa kila mmoja aliyepo karibu na humzunguka kuhakikisha yupo sawa. Mshikamano huu wa tembo unafikia hatua ya tembo mmoja kuwa tayari kwa kujitoa maisha yake kuokoa ndama au kuokoa kundi zima.

Bila kutofautiana sana na binadamu, tembo huishi wastani wa miaka hamsini hadi 70 na chakula kikubwa kikiwa ni mimea hususani mizizi, nyasi, majani, maua, matunda na matawi malaini.

Tembo wa wastani hula wastani kilo 150 kwa siku. Mkonga wa tembo una nguvu ya kukata nyasi na matawi ya miti, hutumika pia kama pua, kama mkono wa kulia chakula na hata kunywea maji maana mkonga huo unaweza kubeba hadi lita 14 za maji.

Tembo hunyonyesha ndama wake na pale anapokuwa hanyonyeshi, ndama huwa ananyonya mkonga wake mithili ya mtoto wa binadamu anavyonyonya kidole gumba chake.

Sitosahau Krismasi ya mwaka 2018 nilipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, ambapo mimi na tuliokuwa nao tulikutana na kundi la tembo watatu waliyoziba njia na hivyo tukalazimika kuzima gari na kubaki tukiwashangaa huku tukiwapiga picha lakini zoezi likaanza kuwa gumu pale ambapo mmoja alipolisogelea gari na kuingiza mkonga wake ndani kupitia dirishani, kitendo ambacho kilitufanya abiria wote tuwe masanamu.

Meno ya tembo hutumika pia kama mikono, hutumika kuchimbia mizizi, kuweka alama kwenye miti kama eneo lake la himaya na pia huzitumia kama silaha wakati wa mapambano.

Tembo akipigana hutumia meno hayo, mkonga pamoja na miguu kumkanyaga adui yake pale anapoanguka na anaweza kutumia meno ya upande mmoja vizuri zaidi kulinganisha na upande mwingine kama ilivyo kwa mikono ya binadamu.

Tembo dume MAKALA Watalii wakimtazama tembo. hupandwa na hasira pale anapokuwa katika kipindi cha joto halafu akakosa jike wa kumpanda.

Halikadhalika madume wawili wanaweza kugombania jike mpaka mmojawapo atakapoibuka kidedea. Tembo pia ana tabia ya kukerwa pia na kelele na yale masikio makubwa yanasikia sana.

Tembo ni mnyama mpole lakini upole wake una mwisho, majangili na wanyama wawindaji wanalitambua hili kwamba tembo huwa haukimbii ugomvi, yeye humfuata adui yake na kupambana nae.

Naweza sema tembo ana intelijensia kubwa kuliko wanyama wengi kana kwamba anaweza kutambua muziki, kuhisi huruma, kufurahi, kucheza mchezo atakaofundishwa na ana kumbukumbu nzuri sana.

Tofauti na wanyama wengine, tembo anajitambua akijiona kwenye kioo na hawezi kuhisi kuwa ameona tembo mwingine.

Tembo mwanafamilia anapokufa, tembo huomboleza pamoja kwa hisia na majonzi na maombolezo hayo huongozwa na tembo jike ambao ndiyo waliyo wengi kwenye ukoo, madume hupenda kujiweka mbali na matukio ya kifamilia.

Ndama wa tembo anapompoteza mama yake anabaki kuwa yatima na mashangazi huchukua jukumu zima la kumlea, lakini malezi hayawezi kufanana na ya mama, hivyo nafasi za ndama huyu kutoboa hadi ukubwani zinapungua kwa sababu fisi wanawawinda sana ndama wa tembo wasio na ulinzi mzuri huku ikiaminika kwamba nyama yao ni tamu sana kwa fisi.

 

OKTOBA 28, 2020 ni siku muhimu na ya kihistoria katika ...

foto
Mwandishi: Nasibu Mahinya

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi