loader
Magufuli aapa kulinda amani

Magufuli aapa kulinda amani

RAIS John Magufuli amewaonya Watanzania waepuke vitendo vya vurugu na mauaji, kwa kuwa hayuko tayari kuiacha nchi ikiwa imesambaratika wakati anamaliza muda wake wa uongozi.

Ametoa msimamo huo wa kulinda amani jana wilayani Momba mkoani Songwe katika Halmashauri ya Mji Tunduma kwenye mkutano wa kampeni. Alikuwa anawaomba kura wananchi, wamchague tena awe Rais wa Tanzania kwa miaka mitano mingine.

Awali, mgombea Ubunge Jimbo la Tunduma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), David Silinde alimpa pole Rais Magufuli, CCM na wanaCCM wote kutokana na mauaji ya kada mwenzao Bryan Mollel Agosti 25, mwaka huu.

Silinde alidai waliofanya mauaji hayo ni wanachama wa chama cha siasa nchini, ambao walimpiga kwa kumponda kichwa kwa mawe kijana huyo hadi akapoteza maisha. Alisema viongozi wana wajibu wa kukataa, kupinga na kukemea vitendo hivyo kuendelea kutokea ndani ya nchi hii.

Rais Magufuli aliwaambia wananchi wa Tunduma kuwa pamoja na kuwaomba kura, lakini pia waache mambo ya ubaguzi kwa kuwa yanaifanya Tunduma isiwe sehemu salama.

“Leo tumesimama kuomboleza kifo cha kijana yule, alipondwa kichwa chake, na waliokuwa wanamponda ni vijana wenzake, Watanzania…Baba wa Taifa ameliacha hili Taifa likiwa salama, mimi kama Rais nisingependa niliache Taifa hili likiwa na hali ya ugomvi namna hii,” alisema Rais Magufuli.

“Ndiyo maana nimekuja Tunduma kuwaomba kura, lakini pia nimekuja kuwaonya, na hili mimi nawaambia kwa dhati bila kupepesa, haiwezi ikawa inafikia wakati wa kura tu hizi za siasa, zitugawanye watu kiasi hiki, Tanzania haijafikia mahali hapo, angalieni nchi ambazo hazina amani, mna ushahidi wa kutosha, kuna nchi mpaka leo zinapigana, Tanzania pamekuwa mahali pa salama pa kimbilio la kila mtu, hatuko tayari kuichafua Tanzania kwa kuanzia Tunduma,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka Watanzania wafahamu kwamba siasa si mwisho wa maisha na vyama visiwe sababu ya kuwagawanya.

Alisema wapo wanasiasa waliotoka CCM na leo wanapumulia mashine kwa sababu hata kampeni wameshindwa na waliwajua kuwa hawatafika mbali, hivyo aliwataka vijana kuepuka vitendo vya jazba na mihemuko ya siasa ila wawe wavumilivu.

“Nawaomba sana ndugu zangu wa Tunduma tushikamane, nchi hii iliachwa salama na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, akaja Mzee Mwinyi, akafanya kazi yake kwa uadilifu na kuliacha hili Taifa salama na amani, akaja hayati Mkapa, alitimiza miaka yake kumi ameliacha Taifa hili kwa amani, amekuja Mzee Kikwete, amefanya kazi yake miaka kumi, ameliacha hili Taifa likiwa salama, kamwe asitokee mtu wa kulifanya Taifa hili tuache kuelewana, serikali haijalala, na mimi japo naomba kura hapa lakini mimi ndiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Aliwataka wananchi wa Jimbo la Tunduma, kumchagua Silinde awe mbunge wao na wasifanye makosa kama waliyoyafanya mwaka 2015, kwa kutomchagua mgombea wa CCM.

Alisema serikali imefanya mambo mengi Tunduma na itaendelea kufanya mengi, hivyo wamchague Silinde  ili iwe rahisi kutekeleza hayo yote.

“Nawaomba wana Tunduma mniletee Silinde, halafu mje mniulize maji, na nimeshaanza kuifanya hii miradi hii, tutayatoa maji Ileje,” alisema Rais Magufuli.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/5d304cee970ad44bacdbb8805c740c7e.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi