loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utendaji serikalini unavutia mashirika kimataifa kupinga ukatili wa kijinsia

TANZANIA ni Miongoni mwa nchi ambazo Serikali yake chini ya Rais John Magufuli imefanya kazi kubwa ya kuwakomboa wanawake na wasichana dhidi ya ukatili wa kijinsia katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020.

Hali hii imeyafanya mataifa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo.

Dhamira ya kuwathamini wanawake imeonekana wazi kwani kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, nafasi ya makamu wa rais wa nchi imeshikiliwa na mwanamke, Samia Suluhu Hassan anayeonesha uwezo mkubwa kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Katika kipindi hiki, Tanzania ilizindua kampeni maalumu kupinga ukatili wa kijinsia na kuandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto unaolenga kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022. 

Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008), Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998).

Serikali inasisitiza kuwa, utekelezaji wa mpango huo utachangia katika utekelezaji wa mipango na mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto.

Mwaka 2018, serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ilielekeza wakuu wa mikoa kusimamia uanzishwaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa Uratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto sambamba na kutenga bajeti maalumu.

Waziri mkuu akaongeza kuwa, watu wenye ulemavu wana mahitaji maalumu na ni miongoni mwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Anaaelekeza Jeshi la Polisi kuboresha Dawati la Jinsia ili lishughulikie kikamilifu masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu. Sasa linaitwa Dawati la Polisi la Jinsia, Watoto na Watu wenye Ulemavu.

Kwa Mujibu wa Majaliwa, ukatili wa kijinsia ni hali ya kutenda vitendo viovu, vinavyodhalilisha, vinavyotesa, vinavyonyanyasa, vinavyokandamiza, visivyojali haki za kuishi kwa binadamu ama awe wa kiume au kike.

Ukatili wa kijinsia huja katika taswira nyingi. “Aidha, kwa uchache tunapozungumzia ukatili wa kijinsia tunamaanisha vitendo kama vile, vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi, lugha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na kunyimwa fursa za kushiriki shughuli za kiuchumi.”

“Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji unaofanywa na mtu dhidi ya mtu mwingine bila kujali umri, maumbile, kabila, rangi, dini au mtazamo wa kisiasa. Unahusisha kumpiga mwanamke au mwanamme, kumnyima mtoto elimu, kulawiti mtoto wa kike au kiume, kumbagua mtu katika mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi wanaohusika.”

Septemba 29, 2020, Dunia imeshuhudia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia usawa wa kijinsia na wanawake (UN Women) na Mfuko wa Umoja wa Mataifa kuhusu wa Idadi ya Watu (UNFPA) kupitia ufadhili wa  shirika la KOICA,  wamezindua  mradi  wa “Tuufikie Usawa  wa Jinsia Kupitia Kuwawezesha Wanawake na Wasichana.”

Mradi huu utakaogharimu takribani Sh bilioni 11.5, utatekelezwa katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na Msalala mkoani Shinyanga kwa miaka mitatu kuanzia Oktoba 2020 hadi Septemba 2023.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi, anasema mradi unalenga kuwawezesha wanawake na wasichana katika mikoa ya Singida na Shinyanga kujikwamua kiuchumi na kijamii ili kufikia usawa wa kijinsia.

Anawataka watendaji wa serikali watakaotekeleza mradi huo kuwa makini ili kutimiza malengo ya mradi.

Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, serikali chini ya Rais John Magufuli, itawachukulia hatua kali watendaji ambao hawataendana na kasi na ufanisi unaokusudiwa kwa kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Anasema katika mkoani Singida, mradi huu utanufaisha Wilaya ya Ikungi kwa kutekeleza malengo makuu mawili ambayo ni kuwawezesha wanawake na wasichana kiuchumi kupitia zao la alizeti na mbogamboga, pamoja na kuimarisha na kuunga mkono juhudi za serikali kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu, akiwa ziarani wilayani Ikungi hivi karibuni, alisema kazi nzuri zinazofanywa na Rais Magufuli katika nyanja mbalimbali ndizo zinazoyafanya jumuiya za kimataifa kuunga mkono kwa kutoa misaada kupitia miradi mbalimbali.

Anasema Serikali imedhamiria kuwakomboa wanawake nchini kwa kuwainua kiuchumi, watakuwa wanaliwezesha taifa zima.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa KOICA Tanzania, Jieun Mo, walengwa wasio wa moja kwa moja takribani wakazi 40,000 kutoka wilayani Ikungi na Msalala na walengwa  wa moja  kwa moja 2350 katika wilaya hizo watanufaika na mradi huu. Wanaume na wanawake 6000 wa Wilaya ya Ikungi watanufaika kwenye eneo la mwingiliano wa hati za ardhi.

Mo ameainisha kuwa, shughuli za mradi katika kuwaweza wanawake kwenye eneo la uchumi zitajikiza zaidi kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana wakulima ili watumie njia nzuri za kilimo na hali ya hewa katika uzalishaji wa alizeti na kilimo cha bustani, kukuza uuzaji wa pamoja, ujuzi wa ujasiriamali na wakala wa uchumi wa wanawake na kuimarisha usalama wa ardhi na umiliki.

Anasema shughuli hizo zitatekelezeka kupitia kuunda vikundi vya uzalishaji wa kilimo cha bustani kwa wanawake, kuunganisha wanunuzi wa vikundi vya wakulima vya wanawake, kusaidia ujenzi wa ghala kubwa la alizeti na kituo cha ukusanyaji kilimo cha bustani.

Hili litalenga kuboresha uuzaji wa pamoja na utunzaji baada ya kuvuna, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kutoa mafunzo ya ujasiriamali na ufikiaji wa habari za kifedha na kufuatilia ushauri wa usimamizi wa biashara na fedha na kukuza umiliki wa ardhi pekee na wa pamoja  wa wanawake kupitia utoaji wa hati za hakimiliki za kimila za makazi.

Mwakilishi wa UN Women, Hodan Addou, anaishukuru Tanzania kwa ushirikiano wake kuhakikisha mradi huu hatimaye unaanza kutekelezwa. Anasema shirika hilo linaunga mkono juhudi za Serikali za kumkomboa mwanamke ili kuondokana na unyanyasaji wa kijinsia.

Addou anasisitiza kuwa mradi utasaidia uwezeshaji kijamii kwa kuwawezesha wanawake kusimamia haki zao, kujenga ujuzi wa ujasiriamali wa wanawake na wasichana kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha mifumo ya kuzuia.

Aidha, utawezesha kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kupitia kuanzisha na kuandaa vifaa katika madawati matatu ya Polisi ya Jinsia na Watoto, kuanzisha vituo vitatu vya huduma za dharura katika vituo vya wilaya, kuunda nafasi salama ya umma, kujenga uwezo wa nambari ya msaada ya watoto kitaifa, kuunda na kuimarisha klabu za wasichana na kuunda kamati za ulinzi na usalam kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania, Zlatan Milisic, anaipongeza Tanzania kwa kuwa na mradi huo akisema unaendana na Malengo ya Naendeleo Endelevu ya 2030 hususani lengo Namba 5 linalohusu kuendeleza wanawake katika nyanja mbalimbali.

Milisic anaongeza kuwa, mwaka 2020 ni muhimu kwani Azimio la Wanawake la Beijing, linaelekea kutimiza miaka 25.

Anasema malengo hayo endelevu ya 2030 yameeleza kuwa, kufikia maendeleo ya nchi kumtambua mwanamke ni jitihada muhimu kuharakisha na kutimiza malengo yote ya maendeleo.

Mwakilishi mkazi huyo anaihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kufanya kazi kwa karibu ili kuhakikisha wanawake wanakuwa chachu ya maendeleo nchini.

Mwakilishi wa UNFPA, Dk Winfred, anasema uzinduzi wa mradi umelenga kutokomeza aina zote za unyanyasaji wa kijinsia na kuimarisha usawa katika jamii ikiwa ni pamoja na kuimarisha maisha ya wanawake.

Anasisitiza kuwa, kitovu cha matatizo ya kijinsia ni hasa mila na desturi potofu zinazomtazama mwanamke kwa kumdharirisha, hivyo juhudi za makusudi zinatakiwa kufanywa ili kutokomeza unyanyasaji huo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk Anjelina Lutambi, anasema programu hii ya pamoja kati ya UN Women, UNFPA na Halmashauri ya Ikungi inasaidia juhudi za serikali kuoanisha Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) II, Mpango Mkakati wa Kutokomeza Ukatili dhidi  ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC 2017/18-2021/22) na Sheria ya Ardhi ya Kijiji ili kuendeleza usawa wa kijinsia.

Mwandishi ni Ofisa Habari wa Mkoa wa Singida.

OKTOBA 28, 2020 ni siku muhimu na ya kihistoria katika ...

foto
Mwandishi: John Mapepele, Singida

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi