loader
Uamuzi wa mahakama wapandisha joto la kisiasa

Uamuzi wa mahakama wapandisha joto la kisiasa

MAHAKAMA ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imetupilia mbali kesi ya kuzuia mabadiliko ya Katiba nchini Uganda yanayotoa nafasi kwa Rais Yoweri Museveni kugombea muhula mwingine madarakani.

Hatua hiyo sasa imezidisha joto la kisiasa nchini humo, ambapo wafuasi wa mwanasiasa na mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine wameapa kumuangusha Museveni kupitia sanduku la kura.

Mahakama hiyo yenye makao yake jijini Arusha, Tanzania, wiki iliyopita ilimwondolea pia makosa aliyekuwa Jaji Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe, katika kesi iliyowasilishwa na wakili Male Mabirizi.

Wakili huyo alimfungulia kesi Katureebe kwa madai kuwa amekuwa akifanya kazi zake bila kuzingatia maadili na kuwa na upendeleo.

Katika kesi dhidi ya mabadiliko ya Katiba yanayomwezesha Rais Museveni kugombea tena urais, Mabirizi alidai mchakato mzima wa kubadilisha kifungu 102(b) cha Katiba ya Uganda kilichokuwa kimeweka ukomo wa umri wa miaka 75 kwa wagombea urais nchini humo haukufuata sheria.

Kesi hiyo ilifikishwa katika Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Mei, mwaka jana, kupinga katiba ya Uganda kubatilishwa.

Awali, majaji wanne kati ya watatu wa mahakama ya juu kabisa nchini Uganda walitupilia mbali rufaa ya wakili Mabirizi kwa msingi kwamba, licha ya kuwapo dosari katika mchakato wa kufanyia marekebisho Katiba hiyo, hazikuathiri mchakato mzima.

Aliyekuwa Jaji Mkuu Bert Katurebe, majaji Stella Arach Amoko, Rubby Opio Aweri na Jotham Tumwesigye, waliidhinisha mabadiliko hayo ya Katiba, huku majaji Eldad Mwangusya, Lilian Tibatemwa na Paul Mugamba wakikubaliana na wakili Mabirizi ambaye baada ya kutoridhika na maamuzi hayo alikata rufaa katika Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d4f219b70bd146ffede1f07d08b9991c.jpg

Marekani na Umoja wa mataifa zimelaani vikali mauaji ...

foto
Mwandishi: KAMPALA, Uganda

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi