loader
Dstv Habarileo  Mobile
TBS yataka wauza vipodozi kuzingatia ubora

TBS yataka wauza vipodozi kuzingatia ubora

WAFANYABIASHARA wa vipodozi nchini wamehimizwa kuzingatia orodha ya vipodozi vinavyofaa na kuruhusiwa kutumika katika soko la Tanzania ili kulinda usalama wa afya za watumiaji na mitaji yao.

Ofisa Udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mbumi Mwampeta, alisema hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ukaguzi uliofanyika sokoni katika maduka yanayouza vipodozi.

Alisema wafanyabiashara hao wakijenga utamaduni wa kutembelea tovuti ya TBS mara kwa mara, watapata orodha ya aina ya vipodozi vinavyoruhusiwa katika soko nchini hali itakayowawezesha mitaji yao kuwa salama bila kuathiri afya za wateja wao ambao ni watumiaji.

Alisema katika ukaguzi walioufanya katika maduka kadhaa yaliyopo Magomeni katika Wilaya ya Kinondoni kuangalia ubora na usalama wa bidhaa za vipodozi, waligundua kuwapo sokoni baadhi ya bidhaa zisizoruhusiwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Tumegundua pia kwamba, kuna bidhaa ambazo maelezo yake kwenye lebo hayaelezi tarehe ya kutengenezwa, tarehe ya kumalizika muda wa matumizi na taarifa nyingine,” alisema Mwampeta.

Akaongeza: “Tumegundua pia kuwapo matumizi ya lugha zisizotakiwa kwenye soko letu la Afrika Mashariki kwa sababu hazieleweki kwa mtumiaji wa kawaida.”

Alizitaja lugha zinazopaswa kuwapo kwenye lebo kueleza bidhaa husika kwa nchi za Afrika Mashariki ni Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa. “Lakini pia ukishakuwa na lugha nyingine ni uamuzi wake mzalishaji, lakini ni lazima ziwepo lugha zinazohitajika soko letu la Afrika Mashariki, hasa hapa Tanzania ni Kiingereza na Kiswahili,” alisema Mwampeta.

Alishauri wafanyabiashara kutembelea tovuti ya TBS inayoonesha vipodozi visivyotakiwa kuwapo soko.

Aliwashauri waingizaji wa bidhaa za vipodozi na vyakula kufika TBS kwa kuvisajili kwa ajili ya usalama wake na kwamba, wauzaji wadogo wanaponunua kwa wauzaji wakubwa, wadai kuonesha cheti cha usajili wa hiyo bidhaa kutoka TBS.

Kuhusu vipodozi vilivyokamatwa baada ya kubainika havifai katika soko la Tanzania, Mwampeta alisema hatua inayofuata ni kuviharibu kwa kuzingatia miongozo na sheria zilizopo. Ofisa Masoko wa TBS, Deborah Haule, alisema katika ukaguzi huo, walikamata sampuli mbalimbali za vipodozi takribani kilo 100 vikiwemo vilivyoisha muda wa matumizi na vyenye viambata sumu.

Alipoulizwa shirika linafanya nini ili kuwezesha wafanyabiashara kuondokana na vipodozi hivyo, Haule alisema: “Kwanza tunatoa elimu, lakini pia tunaendelea na programu za elimu kwa watumiaji na tunaenda hadi katika shule mbalimbali kufanya mafunzo ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari.”

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c00187142dc5c14f3adba8942a95d56a.jpg

Sehemu kubwa ya ulimwengu wa biashara uli dorora kutokana na ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi