loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kwa nini Levina alijiua?

WAKATI kesho ni siku ya mtoto wa kike duniani, Kauli mbiu ya kitaifa inasema: ‘Tumuwezeshe Mtoto wa Kike; Kujenga Taifa lenye Usawa.’

Maadhimisho ya  Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike yanalenga  kutambua, kuthamini  na kuwezesha utekelezaji wa haki za msingi za mtoto huyo na kumlinda dhidi ya ukatili.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (Unicef), wasichana milioni 131 duniani wanaopaswa kusoma, hawasomi shule.

Aidha msichana mmoja kati ya watatu ikilinganishwa na mvulana mmoja kati ya sita wenye umri kuanzia maiak 15 hadi 29 hawana kazi na wala hawakupata masomo huku wasichana milioni 15  wa umri wa miaka 15 hadi 19 wanalazimishwa kuwa na mahusiano ya kingono au kulazimishwa ndoa za utotoni

Wakati dunia inaadhimisha siku hiyo ya mtoto wa kike, tukumbuke tukio lililowahi kutokea hapa nchini mwaka 1990 ambapo mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Levina Mukasa alipojiua kutokana na ukatili aliofanyiwa.

Watu wengi walifikiri kuwa alifanya hivyo kwa sababu alikuwa na matatizo kwao na kuwa masomo yalikuwa yanamshinda. Hata hivyo, waliposikia kwamba alifanya hivyo kutokana na unyanyaswaji wa kijinsia uliofanywa na wanafunzi wawili wa Kitivo cha Uhandisi pamoja na kikundi kilichojukana kama “Punch”, baadhi walikasirika wakati wengine walicheka tu.

Marehemu Levina Mukasa, alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza aliyekuwa akisomea shahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kulingana na maelezo ya waliokuwa wakimfahamu wanasema alikuwa mkimya mwenye msaada na ambaye wakati wote alikuwa tayari kutumia vitu vyake na wenzake. Kila aliposoma wakati wote alishika nafasi ya juu darasani.

Mnamo Februari 7, 1990, Levina alikatisha maisha yake kwa kumeza vidonge vingi vya klorokwini (vinavyotumika kutibu malaria).

Swali linabaki, “kwa nini alifanya hivyo?” Karibu kila mwanafunzi wa kike aliyesoma katika kampasi kuu ya Chuo Kikuu (inayojulikana sana kama Mlimani) atakuwa amenyanyaswa kijinsia katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Wamekuwa wakidhihakiwa, kutishiwa kijinsia au kuvamiwa papo kwa hapo na kubakwa.

PUNCH

Pamoja na hayo lipo kundi la kisirisiri hapo mlimani linajukana sana kama PUNCH, linafikia hata kiwango cha kuchapisha maandishi na michoro michafu kuhusu habari za kimapenzi za sasa au za zamani za muathirika wao.

Madhumuni hasa ya PUNCH ni kuwaweka wanawake chini ya wanaume, kuwafanya wanafunzi bora wa kike washindwe masomo yao na hata kulazimika kukatisha masomo. Inatumiwa pia kuwatishia wasichana wakubali kufanya mapenzi na watu wanaowataka ambao wako katika kundi la PUNCH.

Kumkataa mtu aliyeko kwenye kundi la PUNCH  kunamfanya mhusika“apanchiwe”.

Bahati mbaya, wanawake walio katika kampasi wanaiogopa PUNCH. Wanafungwa na sheria zake kama vile kutokunywa chai ya saa 10.00 katika mgahawa, kutokukaa kwenye ‘high table’, kutokuvaa khanga mgahawani n.k.

Wengine wanafurahia hata kumwona mwanamke mwenzao akipanchiwa. Kutokana na maelezo ya shangazi wa marehemu, Dk V.K. Masanja, ambaye ni mhadhiri wa hapo Mlimani, matatizo ya Levina yalianza wakati wa dansi ya kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza iliyofanyika kwenye hoteli ya Silversands wakati huo alikataa kwenda na mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Kitivo cha Uhandisi aitwaye Mark Victor.

FUJO

Levina alienda dansi hiyo na rafiki zake. Victor alipomuona alimtaka warejee pamoja na akalalamika kwa nini alidhubutu kwenda kwenye dansi na watu wengine wakati alikataa kwenda naye.

Levina alikataa kuondoka naye na Victor akamvuta gauni, rafiki zake walijaribu kumtetea na papo hapo ugomvi ukaanza. Baadhi ya marafiki wa Victor wanaojita “Engineers” [Wahandisi] kundi linalofahamika sana kati ya wanafunzi walimsaidia Victor.

Kundi jingine lijulikanalo kama “insiders” walimsaidia Levina. Hatimaye, baada ya kushindwa wahandisi waliondoka kwenye dansi, lakini huo haukuwa mwisho wa matatizo ya Levina.

Waliporejea kwenye dansi mgogoro mwingine ulizuka kati ya Victor na kundi lake na Levina na rafiki zake. Walipofika kwenye mabweni yao, Victor alikuwa akimsubiri ndipo ikawa usiku mzima kutupiana matusi. Asubuhi na mapema Levina alipeleka malalamiko MUWATA [Serikali ya wanafunzi] uongozi ambao ulisulihisha tatizo hilo. Victor aliomba radhi na akadai kuwa alikuwa amelewa.

Siku iliyofuatia, tukio la Silversands lilipanchiwa. Michoro ya Punch haikumwonyesha jina lake lakini kwa kutoa namba yake yakusajiliwa ilidhihirisha kuwa michoro inayofuatia angekuwemo.

Baadhi ya wanafunzi wa kiume walimwendea Levina na kumwambia kuwa walikuwa kwenye kundi la PUNCH. Walimtishia kumpanchi iwapo angekataa kufanya nao mapenzi. Aliwakatalia na akakosa raha sana. Mmojawapo wa wanafunzi hao alikuwa Omari Sarota, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Uhandisi.

Dk Masanja alisema kuwa yeye (Levina) ndiye alimweleza yaliyotokea. Dk Masanja alisema kuwa alimweleza Levina kuhusu uzoefu wake na mambo ya PUNCH alipokuwa mwanafunzi na jinsi alivyoweza kuyapuuza. Alisema kuwa Levina alionyesha kupata ujasiri na akafikiria kuwa mambo yamekwisha.

Marafiki wa Levina waliambiwa kuwa wangepanchiwa iwapo wangeonekana wakiandamana naye. Alitengwa. Maelezo machafu yalitolewa na maandishi yaliandikwa dhidi ya jina lake katika kila orodha ya majina ambamo majina yake yalikuwemo.

Usiku wa Februari 3, mwaka huo muda wa saa 7.30 wakati Levina alipokuwa kitandani akijisomea alisikia mlango ukigongwa. Kabla hajajibu, mlango ulifunguliwa na Omari Saroti aliingia kwa nguvu chumbani. Walipigana. Levina alimng’ata mkono naye alimpiga ngumi za mashavuni na kwenye matiti. Levina alikimbia akiwa amevaa gauni ya kulalia tu na akajificha kwenye kichaka kilichoko nje ya bweni wakati Saroti akiwa bado anamnyemelea. Aligonga nyumbani kwa mlinzi, ambaye alimsindikiza hadi chumbani kwake na akasubiri kwa muda nje.

Madhumuni hasa ya PUNCH   kuwadhalilisha wanawake

Inasemekana kuwa Saroti alitaka kumbaka, wakati wengine wanasema alimbaka. Wanasema Levina alikataa tu kusema. Hata hivyo Saroti alikuwa amemtishia Levina kuwa angembaka na kumwibia vitu vyake. Asubuhi iliyofuatia, mlinzi alisema kuwa alizungumza na saroti na akasema alikuwa “amelewa” wakati huo.

Levina pia alimwona meneja wa bweni, ambaye alizungumza na Saroti. Alisema kuwa Saroti alimwambia kuwa alifunguliwa mlango na Modesta mwenzake Levina ambaye walikuwa wakiishi naye chumba kimoja. Modesta, alikanusha madai hayo kwani yeye ameoloewa na kila mwisho wa juma huwa nyumbani na familia yake.

Dk Masanja alisema alimpa barua Levina na kumwelekeza kwa Mshauri wa wanafunzi, Dk Biswalo ambaye alikuwa akienda kwenye Mkutano wa Baraza hivyo naye alimuelekeza kwa Mama Rajabu.

Waliitisha jalada la Meneja wa bweni/Mlinzi lakini halikuwa na chochote. Levina alifariki jioni ya Februari  7, 1990. Inaonekana kuwa kundi la Punch ni mabingwa wa vita vya kisaikolojia na wamefanikiwa lengo lao kinyume cha matarajio yao kwa kumkatisha tamaa Levina mpaka akaona kuwa maisha yake hayana maana tena.

Zaidi ya hayo utu wake ulikuwa umedhalilishwa na jitihada za Saroti za kutaka kumbaka maana katika jamii ya Kitanzania inaaminika kuwa mwanamke akibakwa amependa mwenyewe.

Kutokana na Punch kuwalazimisha marafiki wa Levina wamtenga, kumdhihaki mbele ya kadamnasi, kumdhalilisha na kumuonea, kutokana na malalamiko yake kutoshughulikiwa na MUWATA kwa kumwambia kuwa hakuna awezaye kushindana na Punch, wakati wengine walikuwa wakimcheka tuu anavyolalamika na rafiki zake wakimuepuka, yote haya yamemfanya alazimike kukata maisha yake kwani aliamini jamii nzima ilikuwa dhidi yake.

Punch ilifanikiwa kuondoa umoja kati ya wanawake. Saroti alifanikiwa kumkosanisha Levina na Modesta, mtu pekee ambaye ndiye alikuwa akimwamini, kwa kudai kuwa yeye ndiye alimpa ufunguo.

Ukweli ni kwamba funguo zote za Hall 7 alimokuwa akiishi Levina  ziliweza kufungua angalau milango mitano, wakati katika Hall 3 bweni lingine la wanawake ufunguo mmoja unafungua milango yote ya gorofa hiyo. Walimfuatafuata na kumgongea mlango usiku wa manane, walimtupia maneno machafu na kumtishia mlangoni pake, walifanya aonekane kama ‘mwenda wazimu’ na asiyefaa.

Mkutano wa dharura wa wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu, wahadhiri, wafanyakazi na wakazi wengine kwenye kampasi uliotishwa Februari 9 ulikubaliana kuwa wanawake walilaumu uongozi kwa kukataa kuchukua hatua za kinidhamu wakati mambo kama hayo yalipotokea.

Wanasema iliendelea hivyo hadi kufikia hatua ya kuwakatisha tamaa wahathirika wasichukue hatua za kisherivna kushindwa kutoa ushauri unaofaa kwa wanafunzi.

Levina Shujaa

Walisema kuwa Serikali ya wanafunzi [MUWATA] imekuwa kimya ikiangalia tu na mara nyingine ilishirikiana na waovu hao.

Walisema kuwa wanafunzi wa kike ambao walijaribu kupata msaada kutoka MUWATA walijikuta katika matatizo makubwa zaidi, maana walihubiriwa kuhusu ukubwa na uwezo wa Punch.

Zaidi ya hayo wanawake walisema kuwa jumuiya ya wanafunzi wanaichukulia michoro ya matusi ya Punch kama burudani muhimu na wanafunzi wanaoonewa wametumbukia kutokana na mgawanyo na mbinu za utawala za Punch, wakati wasomi na uongozi wamekaa kimya wakihofia visasi kutoka kwa Punch ambayo ilikuwa, inatikisa jamii nzima.

Wanawake walikubaliana kuwa, Levina “asipotee hivi hivi, sisi tumtangaze shujaa ambaye hatimaye ameikomesha Punch”.

Hata hivyo wanaume wanaposikia haya wanacheka. Wanauliza, “kwa nini mmuite Levina shujaa? Alikuwa malaya! Alikula fedha za watu! Mlitaka ale tu halafu asilipe? Kwani yeye ni wa kwanza kujiua! Ni mpumbavu. Alikuwa mdhaifu.

Alikuwa mjamzito! Unyanyaswaji wa kijinsia ni jambo la kawaida, wanawake pia wanayanyasa kijinsia. Mwanafunzi mmoja alirukwa na akili kwa sababu alikataliwa na msichana.” hayo ni baadhi ya maelezo yanayotolewa na wanaume wetu ndani na nje ya kampasi.

Hati zenye kuonyesha uso wa levina zilikuwa zimebandikwa fuvu la Punch.

Aliyekuwa Waziri wa nchi asiye na Wizara Maalum, Getrude Mongella, alipozungumza kwenye mgahawa baada ya kunywa chai katika ‘high table’ alilaani unyanywasaji wa kijinsia huko Mlimani na kusema ni sawa na kitu kilichokuwa kinachemka na sasa kimepasuka baada ya kufikia kikomo.

Mapambano ndiyo kwanza yameanza.

Walakini mapambano hayo lazima yaenezwe katika asasi kwanza yameanza, yaenezwe  katika asasi zote za elimu ya juu na sehemu za kazi. Lazima kuwepo na mapambano ya kitaifa dhidi ya uovu huu, Levina ni mwakilishi tu, lakini wapo wengi wanaopitia magumu na machungu kama ya Levina. Jamii ipaze sauti!

 

Makala hii iliandikwa na Chemi Che-Mponda

katika gazeti la Dailynews 1991

NAIBU Waziri wa Nchi Ofi si ya Waziri Mkuu anayeshughulikia ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi