loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa aagiza wakulima wapate mbolea kwa wakati

Majaliwa aagiza wakulima wapate mbolea kwa wakati

 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza watendaji serikalini wahakishe mbolea ya bure inayotolewa na kampuni ya YARA Tanzania inawafikia kwa wakati wakulima waliokusudiwa kwa kuzingatia maandalizi ya msimu wa kilimo mwaka 2020/2021.

Alizindua mpango huo jijini Dar es Salaam kuwezesha ugawaji mbolea tani 12,500 ili sekta ya kilimo ipige hatua na kutoa mchango katika kuinua uchumi na kuongeza kipato cha mkulima.

“Nachukua fursa hii kuipongeza kampuni ya YARA kwa kujitoa kwake kuchangia kwenye kukuza sekta ya kilimo kwa kutoa mbolea bure kwa wakulima zaidi 83, 000,” alisema Majaliwa.

Aliagiza watendaji wa serikali washirikiane na YARA kutimiza lengo la kuwafikishia mbolea wakulima kwa wakati.

“Watendaji wasiwe kikwazo katika utekelezaji wa mpango huu ambao una lengo la kuwanufaisha hasa wakulima wadogo ili kuongeza uzalishaji wa mazao nchini,” alisema Majaliwa.

Alitoa wito kwa kampuni nyingine zinazojihusisha na sekta ya kilimo kuiga mfano wa kampuni YARA katika kuiboresha kwa kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima.

“Natumia nafasi hii kuyataka kampuni mengine kujitoa ili kusaidia sekta hususani kwenye swala la pembejeo na zana za kilimo kwa kuwa kilimo ni sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania,” alisema Majaliwa.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema wizara hiyo na mamlaka za uthibiti zimejiridhisha kuwa mbolea ya YARA inafaa kwa matumizi kulingana na mazingira ya nchi yalivyo na hivyo itaongeza uzalishaji wa mahindi na mpunga.

“Taratibu za kufanya ithibati ya mbolea hii zimezingatiwa hivyo tuna imani zitachangia katika kuongeza ubira na uzalishaji wa mazao nchini,” alisema Hasunga na kuongeza;

“Serikali imejipanga kuhakikisha masoko ya mazao yanapatikana ili mkulima aweze kufaidika na shughuli yake jambo litakalo chochea ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla,”

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya YARA Tanzania, Winstone Odhiambo alisema mpango huo ni jitihada za kampuni mama kutoka Norway kuhakikisha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinajitosheleza kwa chakula.

Aina za mbolea zinazosambazwa na kampuni hiyo ni NPK na wakulima wanapaswa kujisajili kupitia namba *149*46*16#.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi