loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM afunga kazi Dar

JPM afunga kazi Dar

 

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amewashukuru wananchi wa Dar es Salaam kwa kumuunga mkono katika mikutano yake ya kampeni, na kueleza kuwa ana deni kubwa kwao.

 

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Rais Magufuli alifanya mkutano wa kampeni Oktoba 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya majimbo ya Temeke, Mbagala na Kigamboni.

 

Oktoba 12, mwaka huu alifanya kampeni Kinyerezi kwa ajli ya majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea, juzi alifanya mkutano Viwanja vya Barafu Mburahati kwa majimbo ya Ubungo na Kibamba, na jana alihitimisha kampeni zake katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa majimbo ya Kawe na Kinondoni kweney Viwanja vya Tanganyika Packers Kawe.

 

Katika mikutano hiyo yote, wananchi walijitokeza kwa wingi bila kujali jua wala mvua hali iliyomfanya kuwashukuru kwa kumuunga mkono na kuahidi kufanya makubwa baada ya kushinda uchaguzi.

 

“Leo nahitimisha kampeni zangu katika Mkoa wa Dar es Salaam hapa Kawe, nawashukuru sana wananchi wa Dar es Salaam kwa kuniunga mkono, nina deni kubwa kwenu, asanteni sana Dar es Salaam kwa mapenzi makubwa mliyoyaonesha kwangu,” alisema Rais Magufuli.

 

Baada ya kuwashukuru, aliwataka wananchi wa Jimbo la Kawe wasifanye tena makosa kwa kuchagua upinzani, bali wampe kura zote mgombea ubunge wa CCM, Askofu Josephat Gwajima na madiwani wote wa CCM.

 

Alisema anatambua kuna kampeni za ubaguzi wa kidini unaofanywa na wapinzani wao mitandaoni, hivyo akawataka wawapuuze wanaofanya kampeni za ubaguzi na badala yake wamchague Askofu Gwajima.

 

“Kawe mmechelewa sana, mwaka 2015 niliwaomba mumchague Kippi Warioba, lakini mlinyima kura, kwa hiyo sasa naomba msirudie makosa, fanyeni mabadiliko ya kweli kwa kumtoa aliyekuwepo nileteeni Askofu Gwajima,” alisema Rais Magufuli mbele ya maelfu ya waliohudhuria mkutano wake.

 

Alisema kitendo cha wananchi wa Kawe kumchagua mbunge wa upinzani kumewafanya wakose miradi mingi ya maendeleo kwa kuwa mbunge waliyemchagua alishindwa kuwatumikia.

 

Rais Magufuli aliwaahidi wananchi wa Kawe kuzifanyia kazi kero zote ambazo Askofu Gwajima alizitaja ikiwamo kutoa eneo kwa mafundi gereji Geita, kuboresha bandari ya Mbweni, wachimbaji mchanga wadogo Kawe, mafuriko Chasimba na Boko, zahanati Bunju, miundombinu ya barabara na mambo mengine mengi.

 

Pia aliwataka wananchi wa Kinondoni kumchagua Tarimba Abbas kwani anafaa pamoja na madiwani wote wa CCM, lakini pia akaomba wananchi wote wa Dar es Salaam wakipe ushindi wa kishindo CCM.

 

Kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa, Rais Magufuli aliomba kura kwa wananchi wote wa mikoa ambako hakuweza kufika na badala yake aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa.

 

“Nilitamani kufika mikoa yote ya Tanzania, lakini niwaombe Watanzania mtambue kuwa mimi ni binadamu nisingeweza kufika kila mahali, lakini pia pamoja na kufanya kampeni, nina majukumu pia ya kutekeleza ya kitaifa, ndiyo maana nimewatuma wasaidizi wangu,” alieleza Rais Magufuli.

 

Alisema kwenye baadhi ya mikoa ukiwemo Katavi na Rukwa amemtuma Mkaamu wa Rais na kwa mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pemba atamtuma Majaliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema mkutano wa jana pia ulikuwa ni mkutano wa kuzindua awamu ya sita na ya mwisho ya kampeni za CCM.

 

Dk Bashiru alisema awamu ya sita ni ya lala salama na kuwataka wanaCCM wote kufanya kampeni za kishindo ili kujihakikishia ushindi wa kishindo.

 

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi