loader
Magufuli kutekeleza  ahadi zote Pemba

Magufuli kutekeleza ahadi zote Pemba

 

MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amewahakikishia wananchi wa kisiwa cha Pemba kuwa ahadi zote kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho 2020-2025 kuhusu miradi na mipango ya maendeleo kisiwani humo zitatekelezwa.

 

Magufuli amesema kama mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi atachaguliwa kuongoza visiwa hivyo atashirikiana nae kutekeleza ahadi hizo.

 Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa kisiwa cha Pemba kupitia simu aliyompigia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni.

Mgombea huyo wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipiga simu wakati Majaliwa akiwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Mchangamdogo Kambini, jimbo la Kojani, Kaskazini Pemba.

Aliahidi kuwa atafanya kazi kwa karibu na kumpa ushirikiano Dk Mwinyi endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ili kuleta maendeleo haraka katika visiwa vya Unguja na Pemba.

 

"Nimemtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa afanye kazi ya kuniombea kura mimi John Joseph Magufuli, mtanipa lakini? (aliuliza hadhira iliyohudhuria mkutano huo na kujibiwa ‘Ndiooo), la pili nataka nimuombee kura Mheshimiwa Mwinyi awe Rais wa Zanzibar na wawakilishi na madiwani hapo Pemba muwape wote wa kutoka CCM. Ninataka niwahakikishie changamoto zenu mlizonazo za maji, ajira na masuala mbalimbali zitashughulikiwa msipoteze kura zenu muniletee Dk Mwinyi," alisema.

 

Magufuli alimtaka Majaliwa ampelekee orodha ya miradi na mipango ya maendeleo iliyotajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 na mambo yote ambayo Dk Mwinyi ameyatolea ahadi katika mkutano huo.

 Aliwasihi wananchi wa Pemba wasifanye makosa katika uchaguzi ujao, bali wawachague wagombea wa CCM katika nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani.

Kwa upande wake, Majaliwa aliwapongeza wananchi wa Pemba kwa kuonesha kuwa wamebadilika, wamechoka kudanganywa na wapo tayari kuipigia kura CCM.

 

Aliwaomba wapigakura wamchague Dk Mwinyi kwa kuwa ni muadilifu na ameahidi kuunda serikali itakayowatumikia wananchi kwa kukusanya na kusimamia mapato na mali za serikali kwa manufaa yao.

 "Nawasihi sana ndugu zangu tumchague Dk Mwinyi ili aweze kupambana na wala rushwa na mafisadi, akiunganisha nguvu zake na Serikali ya Muungano wa Tanzania ataweza kuifanya Zanzibar ipae kiuchumi," alisema Majaliwa.

Aliwasihi wananchi wasikubali kutumika vibaya kipindi hiki cha uchaguzi na kuchagua viongozi wasioaminika kwa sababu tu za ushabiki wa kisiasa.

Naye Dk Mwinyi alitaja faida za Muungano kuwa ni pamoja na amani na utulivu na kwamba ili Zanzibar waendelee kuwa na amani lazima uendelee kuwapo.

 

"Juhudi zote na mipango mizuri ya maendeleo na maisha bora kwa Wazanzibar hazitafanikiwa kama amani itatoweka," alisema Dk Mwinyi.

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Idd aliwahakikishia Wazanzibari kuwa serikali itaimarisha ulinzi siku ya uchaguzi Oktoba 28, mwaka huu.

Aliwasihi wananchi wasikubali kudanganywa na wanasiasa wasioitakia mema Zanzibar wanaowachochea waende kupiga kura siku ya Oktoba 27 ambayo ni maalumu kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama na wasimamizi wa uchaguzi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/88f3e646872ef3cd135b058b4c39112a.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi