loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Azam yasaka rekodi kwa Mwadui

TIMU ya soka ya Azam FC imesema iwapo itaifunga Mwadui leo katika mchezo wa Ligi Kuu itakuwa imeifikia rekodi ya msimu wa 2015/2016 wa kucheza michezo sita bila kupoteza.

Vinara hao wanaoongoza kwa pointi 15, hawajapoteza mchezo wowote katika michezo mitano waliyocheza, na leo watashuka dimbani katika Uwanja wa Azam Complex kuikaribisha Mwadui.

Msemaji wa Azam FC, Thabit Zakaria alisema wanatamani kuifikia rekodi hiyo kisha baadaye wajipange kuivunja.

“Mara ya mwisho kucheza michezo sita bila kupoteza ilikuwa msimu wa mwaka juzi, naamini kwa namna kikosi chetu kilivyoandaliwa kitafanya vizuri na kufikia rekodi yetu ya zamani kisha tuje tuivunje,”alisema.

Azam FC imekuwa bora katika safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Prince Dube aliyeifungia timu yake mabao matano na kuchangia pasi mbili za mabao.

Katika maandalizi ya mchezo huo, timu hiyo ilicheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar walioshinda mabao 3-1 na Fountain Gate mabao 4-0.

Mabeki wake wawili waliokwenda kuzitumikia timu zao za taifa, Nikolas Wadada kutoka Uganda na Yakubu Mohamed kutoka Ghana walitarajiwa kuwasili jana kujiunga na wenzao.

Aidha, Mwadui ilicheza dhidi ya Yanga na kufungwa bao 1-0, mchezo uliochezwa hivi karibuni katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Kocha wa kikosi hicho, Khalid Adam alisema kupitia mchezo huo ametumia kutazama mapungufu yao kwa lengo la kuyafanyia kazi hivyo, anaamini wachezaji watafanya kazi waliyoelekezwa kupata matokeo mazuri.

Mwadui imecheza michezo mitano, imeshinda miwili na kupoteza mitatu ikiwa na pointi sita. Msimu uliopita timu hizi zilikutana mara mbili na Azam kushinda kila mmoja bao 1-0.

Mchezo mwingine utakaochezwa ni Gwambina dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Gwambina katika michezo mitano imeshinda mmoja, sare moja na kupoteza mitatu huku udhaifu wao ukionekana safu ya ushambuliaji iliyofunga mabao mawili tu na ulinzi iliyoruhusu mabao matano.

Kwa upande wa Mtibwa katika michezo mitano, imeshinda mmoja, sare mbili na kupoteza miwili. Hawa pia, bado safu ya ushambuliaji sio bora ikifunga mabao mawili na pia, safu ya ulinzi imefungwa mabao matatu.

Timu zote zinahitaji matokeo mazuri kujiweka sehemu nzuri. 

KIKOSI cha Yanga chini ya kocha mpya Cedric Kaze kimeendelea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi