loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM kumalizia lala salama Kaskazini

JPM kumalizia lala salama Kaskazini

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally ameeleza ratiba ya awamu ya sita ya Mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli, huku akitoa sababu za kwa nini hatakwenda baada ya mikoa kuomba kura.

Dk Bashiru aliwaambia waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam kuwa Rais Magufuli hatakwenda katika baadhi ya mikoa kutokana na ufinyu wa muda na hasa baada ya mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa, kufika katika maeneo ambayo mgombea urais hakufika.

“Mgombea urais asingeweza kufika maeneo yote nchini, lakini ukiunganisha ratiba ya Rais Magufuli, mgombea wa Zanzibar, Mjumbe wa Kamati Kuu Majaliwa, mgombea mwenza Mama Samia, utaona kote tumeenda.

Hivyo mgombea urais akitoka Dar es Salaam anaenda Pwani, Tanga kisha atakwenda Kilimanjaro, ataingia Arusha, Manyara na kisha ataingia Dodoma,” alieleza.

Kutokana na kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa, juzi akiwa kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli aliomba kura kwa wananchi wote wa mikoa ambako hakufika na badala yake aliwakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa.

“Nilitamani kufika mikoa yote ya Tanzania, lakini niwaombe Watanzania mtambue kuwa mimi ni binadamu nisingeweza kufika kila mahali, lakini pia pamoja na kufanya kampeni, nina majukumu pia ya kutekeleza ya kitaifa, ndiyo maana nimewatuma wasaidizi wangu,” alieleza Rais Magufuli.

Alisema kwenye baadhi ya mikoa ukiwemo Katavi na Rukwa amemtuma Mkaamu wa Rais na kwa mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Pemba atamtuma Majaliwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Aidha, Dk Bashiru alisema mpaka jana maeneo yote nchini wamefika. Alisema ugumu unatokana na ukubwa wa nchi na kusimamisha wagombea kuanzia kata hadi taifa na ndio sababu ya wagombea wa CCM kujigawa kwa namna hiyo.

Alisema katika historia ya uchaguzi wa vyama vingi, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, CCM itakwenda kushinda kwa kishindo kikubwa ambacho hakijawahi kutokea kwa kuwa inashindana na vyama dhaifu na vipya.

“Ushindi ni mkubwa sana unajua mwaka huu tumeshindana na vyama dhaifu kuliko wakati wowote, sasa vyama dhaifu hata vikiwa na wagombea wazuri bado utendaji utakuwa dhaifu, ACT ni kipya kimesimamisha wagombea urais Zanzibar na Bara.

“Lakini wa Bara namtafuta sijui yupo wapi, ningekuwa katibu wake mkuu ningekuwa nimeshaenda Polisi, sijui yuko wapi, sasa hao ndio tunaoshindana nao,” alisema Dk Bashiru na kusema hata wanaojikakamua kama Chadema, bado chama hicho ni dhaifu kwa kuwa waliowapa nguvu mwaka 2015, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, sasa wapo CCM.

Dk Bashiru alisema mwaka 2015 wagombea walikimbilia upinzani na kupambana na mteuliwa dirishani, leo wote 40,000 waliowania nafasi mbalimbali ndani ya chama, wapo pamoja kwa nguvu moja hivyo ushindi ni mkubwa.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi