loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Changamoto 5 Muungano Zatatuliwa

SERIKALI imetatua changamoto tano za Muungano na kuwekeana saini hati ya makubaliano kuondoa hoja za muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika Ikulu, Dar es Salaam leo na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluh Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine mbalimbali wa serikali upande wa Zanzibar na Bara.

Akitaja mambo matano yaliyopatiwa ufumbuzi, Makamu wa Rais, Samia amesema ni ushirikishwaji wa SMZ katika masuala ya kimataifa na kikanda ambayo itaiwezesha Zanzibar kujadili matatizo yake kimataifa na ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mengine ni gharama ya kushusha mizigo bandarini ambapo Samia amesema “Suala hili limekuwa likipigiwa kelele muda mrefu, sasa limepatiwa ufumbuzi,”

Changamoto nyingine iliyotafutiwa ufumbuzi ni utafutaji na uchimbaji wa mafuta ya gesi asilia na utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya kushughulikia masuala ya Muungano.

“Kutatuliwa kwa changamoto hizi haimanishi Muungano wetu una matatizo, hata ndani ya nyumba migongano inatokea, na inapotokea migongano haimanishi hakuna mapenzi,” amesema Samia.

Awali akizungumzia hatua hiyo, Waziri wa Mazingira anayeshugulikia Muungano, Mussa Hassan ‘Zungu’ amesema  utiaji saini hati za makubaliano ya ufumbuzi wa changamoto hizo umetokana na muendelezo wa vikao vya kamati ya pamoja kwa ajili ya kushughulikia masuala ya muungano na kuridhia hoja hizo tano za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi, hivyo zinaondolewa katika orodha ya hoja za Muungano.

Kwa upande wa Waziri Mkuu, Majaliwa akizungumza katika hafla hiyo, amesema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imefanikiwa kuonesha dhamira kwa vitendo katika kuimarisha Muungano.

Amesema mafanikio hayo yamechochewa na utendaji kazi wa Samia anayesimamia wizara inayoshughulika na masuala ya Muungano na Mazingira.

 “Kufuta hati hizi, ni kielelezo tosha kwa Serikali ya SMZ na Jamhuri ya Muungano namna zilizojikita katika kutatua changamoto mbalimbali za Muungano kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.”

“Mfano ni kuondolewa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kufuta malimbikizo ya deni lililokuwa limefikia Sh bilioni 22.9  kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco)  kutokana na umeme uliouzwa na Tanesco,” amesema Majaliwa na kuongeza:

“Rais Magufuli alifuta sherehe za Muungano wakati wa Covid-19 na kuelekeza Sh milioni 500 za sherehe hizo ipatiwe Zanzibar,” amesema.

Akihitimisha hotuba yake, Majaliwa alinukuu sehemu ya ujumbe aliotoa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Machi 6, 1997 Accra, Ghana kwamba: “Umoja hautatupatia utajiri lakini utatufanya Waafrika tusipuuzwe na kudharauliwa .”

Amesema Muungano huo ndio chimbuko la umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo,” hivyo basi tukiwa tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu, Nitoe rai wananchi kujitokeza kumpigia kura mgombea urais wa Zanzibar, Dk Hussen Mwinyi na Dk John Magufuli.”

WAZAZI nchini wameaswa kuisaidia serikali kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi