loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

HUSSEIN MWINYI: Mdau wa utalii aliyejikita kwa wanafunzi

KARIBU kila mtu anayefanya shughuli fulani hasa kama ni kazi inayomwingia kipato anakuwa na sababu iliyopelekea kuifanya kazi hiyo.

Sababu hizo zinaweza kuwa ni zile zinazotokana na uzuri wa shughuli husika au hata mateso ambayo ameona yakitokea na ndio maana anaamua kufanya jambo kwa lengo la kuwanusuru wengine.

Hii ni ndio kama ilivyotokea kwa Hussein Mwinyi ambaye amejikuta akiingia katika kazi za utalii na hasa kuhamasisha masuala ya utalii wa ndani kwa wanafunzi.

Mwinyi ni maarufu hasa kwa shule za Dar es Salaam, umaarufu wake unatokana na uwezo wake katika kuimudu sekta ya utalii kwa kuwaunganisha wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari na vituo vya utalii.

Kazi anayoifanya hasa ni kuwachukua wanafunzi hao kutoka kwenye shule hizo na kisha kuwafikisha mbugani au hata kwenye vituo vingine vya utalii vinavyopatikana mjini kupitia kampuni yake ya Loxodanta.

Gazeti hili lilikutana na Mwinyi kwenye Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam iliyopo katikati ya jiji la Dar es Salaam, siku ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.

Alikuwa na wanafunzi takribani 500 na wote walifikishwa katika Makumbusho hayo na Mwinyi ambaye tangu akiwa kijana alikuwa na shauku siku moja kushiriki kuendeleza utalii kwa wanafunzi.

Alivyoanza utalii Mwinyi Mzaliwa wa mkoani Tanga alivutiwa na shughuli za utalii na kaka yake aliyekuwa akiitwa Hassan Mwinyi ambaye hivi sasa ni marehemu.

Anasema kaka yake huyo alikuwa Mkuu wa Kikosi cha kupambana na ujangili mikoa ya Kusini ambaye siku moja alifika Tanga na kumchukua kwenda naye mkoani Mtwara na anaongeza kuwa wakiwa mkoani Mtwara siku moja kaka yake huyo alimchukua na kwenda naye mikoa jirani ya Mtwara akiwa kwenye kazi zake za kukabiliana na majangili.

Akiwa Lindi na kisha kurejea Mtwara alishuhudia wahalifu hao walivyokuwa wakiathiri maliasili za nchi na watuhumiwa hao walikuwa wamekamatwa wakiwa na nyara mbalimbali.

Anasema wengine walikuwa wamekamatwa na nyama za nyati na wanyama wengine ambao hawaruhusiwi kuwindwa huku wengine wakiwa na mikia ya simba na bidhaa nyingine ambazo sio halali kwa wananchi kuwa nazo.

Kwa mujibu wa Mwinyi matukio hayo yalimsukuma kuwaza sana na akajiuliza kama wamekamatwa kwa kuua wananyama je, ni wanyama wangapi tayari watakuwa wameuawa kwa kipindi cha miaka miwili, mitatu hadi mitano.

Anasema hapo alianza kuumiza kichwa kuwaza ni hatua gani anaweza kuchukua kuzuia ujangili huo na wazo lililomjia lilikuwa ni kuanza kuwaandaa watoto kupenda utalii.

Mwinyi anasema alifikiria kumwambia kaka yake wazo lake hilo lakini ilikuwa ni muda ambao sasa anatakiwa kurejea Tanga, alirudi Tanga huku kichwani akiwaza mkakati wake wa kuwashirikisha watoto kupenda utalii na kulinda maliasili ili kuzuia baadaye wasije kushawishika na kushiriki kwenye matukio ya ujangili.

Anasema wakati huo alikuwa ana ari kubwa zaidi ya kupenda utalii, lakini kwa bahati mbaya kaka yake huyo alirejea Tanga na aliaga dunia zikiwa ni siku chache baada ya kurejea mkoani humo.

Mwinyi anasema licha ya kifo hicho cha kaka yake kumuuma, kilimuongezea nguvu na kuchochea wazo lake hilo la kuanza mpango wa kuwahusisha watoto na utalii sambamba na kutamani kuenzi kazi aliyokuwa akifanya kaka yake.

“Yani nilijikuta naanza kupenda utalii na ulinzia wa mali kale, hifadhi na utunzaji wa mazingira, nilikuwa na shauku kubwa pengine hata kushinda kaka yangu ambaye alikuwa ameshatangulia mbele ya haki…nikaona ili kumuenzi ni lazima kwanza nihakikishe wazo langu la kuwahusisha watoto katika masuala ya utalii linafanyiwa kazi na kwa kufanya hivyo niliamini namuenzi kaka yangu,” anabainisha.

Mwinyi anasema aliamua kuanzisha kwanza ofisi ya utalii mkoani Tanga kisha akafungua nyingine Dar es Salaam na alianza na wafanyakazi wawili ambao ni Husna Hussein na Shaban Kimambi.

Anasema wakiwa Tanga waliona kuwa ni vema wakahamia kwanza Dar es Salaam ili wazo lao linafinikiwe kwa urahisi. Mwinyi anaongeza kuwa walianza kupita katika baa, kambi na ofisi mbalimbali kuhamasisha masuala ya utalii hasa wakitafuta wateja watakaotumia huduma zao kwenda kutalii katika mbuga mbalimbali.

Anasema awali ilikuwa ni kazi ngumu kwa kuwa mbinu ya kutafuta watalii katika baa na ofisi mbalimbali ilikuwa ikiwapatia watalii wachache, lakini kwa kuwa lengo lilikuwa kupata fedha kwa ajili kuwaendeleza watoto kupenda utalii wakavumilia.

Mwinyi anasema baada ya muda walipata fedha za kutosha kwenda kwenye shule kadhaa hasa za msingi kufundisha masuala ya uhifadhi wa mazingira, utalii, ulinzi wa mali kale na viumbe baharini.

“Sasa baada ya kusaka fedha kuanzia mwaka 2009 kwa njia ya kupeleka watalii mbugani, tukapata kiasi ambacho tukajipanga kwa lengo la kwenda shuleni kufundisha masuala kadhaa ya uhifadhi na utalii huku lengo likiwa kuwaandaa watoto kuwa walinzi wakubwa wa maliasilia na kupinga ujangili,” anasema.

Kwa mujibu wa Mwinyi alishirikisha wazo lake Wizara ya Elimu na walimpatia shule za kuanzia na hapo ndipo akafungua milango ya kuwapeleka watoto katika mbuga za wanyama kutalii.

“Wakati nilipokuwa najiandaa kuja kufanya kazi za utalii hasa kwa watoto pia nilikuwa nasoma masuala ya utalii, uhifadhi wa mazingira na mali kale tena kupitia mitandao ya kijamii, vitabu na wadau, nilisoma kwa kina tu na ndio maana haikuwa shida kuja kufundisha nikiwa na wenzangu hao,”anasema.

Anaongeza kuwa akiwa na timu yake waliendelea kutoa elimu hadi walipoona ni muda sasa wa kuwapeleka watoto kwenye mbuga za wanyama na wakaanza na mbuga ya Saadani na wanawapeleka pia katika maeneo mengine ya utalii lakini kwa kiasi kidogo cha michango kutoka kwa wazazi.

Mwinyi anasema tangu alipoanza harakati zake hizo mwaka 2009 hadi sasa ameshawafikia zaidi ya wanafunzi 10,000 na kuwasafirisha kutembelea vituo mbalimbali vya utalii nchini.

Anasema kwa kushirikiana na walimu ameendelea kuwaelimisha wanafunzi mambo ambayo yatawawezesha kuepuka kushiriki kwenye uhalifu hasa ujangili.

Moja kati ya kazi zake Gazeti hili lilishuhudia moja kati ya kazi za Mwinyi chini ya kampuni yake hiyo la Loxodanta alipowapeleka wanafunzi zaidi ya 300 kutoka shule sita za Kibasila, Temeke, Olyimpio, Bunge na Movamali kutembelea Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam kujifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na utendaji kazi wa mwasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

Anasema wanafunzi wakitembelea maeneo kama hayo wanaongeza uelewa wa mambo kadhaa vichwani mwao. “Hizi ni harakati nzuri za kukuza utalii wa ndani ya nchi kwa kuwa kama wanafunzi wakianza kutembelea makumbusho haya tangu wakiwa wadogo wanajifunza na watakuwa na mengi ya kusimulia kwa wenzao na kwa kufanya hivyo wanahamasisha utalii wa ndani,” anasema.

Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Mwinyi, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga anasema wanafunzi wanapofika hapo kutalii hujifuza na kupata uelewa wa masuala mengi kuhusiana na utalii.

Anatolea mfano kuwa wanafunzi wanaotembelea Makumbusho hayo wanafundishwa kuhusiana na upendo, amani, uzalendo na uchapaji kazi mambo ambayo Mwalimu Nyerere alikuwa akiyatekeleza kwa vitendo.

Anasema Makumbusho ya Taifa hupokea wanafunzi zaidi ya 500 kila wiki wanaokwenda kujifunza masuala mbalimbali kuhusiana na utalii na utamaduni na ziara iliyofanyika Oktoba 14, mwaka huu ilikuwa maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Mambo anayopenda Mwinyi ambaye ni baba wa watoto wanne anapendelea zaidi kusoma vitabu hasa vinavyoelimisha kuhusiana na masuala ya wanyama, haki ardhi, uhifadhi wa misitu na masuala ya mali kale na asili.

WANAWAKE wamekuwa ni chachu kubwa ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi