loader
JK: MUME CHADEMA, MKE CCM, SISI WAMOJA

JK: MUME CHADEMA, MKE CCM, SISI WAMOJA

RAIS Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimeliunganisha taifa kwa kujenga na kuimarisha upendo, umoja na uvumilivu kati ya watanzania.

Kikwete amesema hayo kwenye Uwanja wa Zakhiem- Mbagala katika kampeni za kumuombea kura Rais John Magufuli anayewania nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM , pia alimuombea kura mgombea  ubunge wa jimbo la Mbagala, Abdallah Chaurembo pamoja na wagombea wa nafasi za udiwani  wa jimbo hilo.

Kati ya hoja alizogusia kwenye kampeni hiyo ni pamoja na uwezo wa CCM wa kuwaunganisha watanzania  licha ya tofauti zao za kidini, kisiasa na ukabila  huku akibainisha kuwa licha ya kuwa na makabila 120 na vyama vya siasa 19 lakini watanzania wameendelea kuwa wamoja na wanapendana.

Alisema:“Tunashindana , tunapigana vijembe hasa katika kipindi kama hiki cha kampeni, lakini Uchaguzi ukiisha tupo wamoja, mume Chadema, mke CCM, wapo nyumba moja na maisha yanaendelea, hiyo ndio Tanzania,

Pamoja na hayo, nchi yetu imeendelea kuwa na amani, umoja na utulivu kuna nchi sitaki kuzitaja zinahangaika kutafuta amani na utulivu, ukabila unawatafuna, udini unawagawa hivyo basi amani tuliyonayo ni tunu tuitunze.”

Aidha Kikwete aliweka  mbele vipaumbele miradi ya kimkakati  pamoja na kutatua kero zinazowakabili wananchi na kuwataka kumchagua Magufuli ili amalizie kazi aliyoianza ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na hospitali, barabara, usambazaji maji, umeme na huduma nyingine za kijamii.

Amesema Magufuli amekomesha nidhamu mbovu ya watendaji wa umma katika kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kuzuia rushwa.

“Rais Magufuli kapambana na rushwa, mahakama ya mafisadi imeanzishwa ndio maana uchaguzi huu sijasikia mgombea yeyote aliyezungumza rushwa na atakeyechukua kama ajenda atakua ameishiwa,” amesema

 “Tumchague Magufuli aendelee kuongoza nchi yetu, tumpe miaka mitano mingine amalize ngwe yake. CCM ina sera nzuri za kudumisha masilahi ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kiusalama na watu wake. Hakuna chama kingine kinachofanana na CCM mimi sikijui,” amesema Kikwete.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

1 Comments

  • avatar
    Deus Thomas keya
    19/10/2020

    Watanzania tuipe serikali ya CCM ili kuleta maendeleo ya kweli na kusimamia Amani Tanzania

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi