loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kero 5 za Muungano zaondolewa rasmi

S ERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zimesaini hati ya makubaliano ya kuondoa hoja tano za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Hoja hizo zilikuwa kwenye orodha ya changamoto za Muungano lakini baada ya kufanyiwa kazi, zimeondolewa huku nyingine sita zikiwa zimeshapatiwa ufumbuzi na zinasubiri ridhaa ya Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ kuondolewa pia.

Hati za makubaliano zilisainiwa jana Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika Ikulu na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alisema, kuondolewa kwa hoja hizo haimaanishi kwamba Muungano una matatizo bali ni utaratibu wa kawaida wa kurekebisha kasoro zilizopo kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuudumisha.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano Na Mazingira), Mussa Azzan Zungu, kikao cha kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya muungano kilichofanyika Dodoma Februari 9 mwaka jana, kiliridhia hoja hizo tano zilizopatiwa ufumbuzi ziondolewe kwenye orodha.

Hoja hizo ni ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda, ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, gharama za kushusha mizigo bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Akifafanua kuhusu hoja ya ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine alisema kulikuwa na hoja kwamba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki haiipi nafasi ya kutosha Zanzibar ya kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na unaohitajika na Taasisi za kimataifa.

Katika hilo, pande mbili zimeandaa mwongozo wa ushirikishwaji wa SMZ kwenye masuala ya kimataifa na kikanda ambao utazingatia ziara za viongozi wa kitaifa, mikutano ya kimataifa, nafasi za masomo ya elimu ya juu nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada au mikopo ya kutekeleza miradi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Changamoto kuhusu ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilihusu nafasi yake katika kuwasilisha miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya kujumuishwa kwenye miradi ya kikanda inayotekelezwa katika jumuiya.

Balozi Sokoine alisema SMZ iliwasilisha miradi minane ya maendeleo kwa ajili ya kujumuishwa kwenye miradi ya kikanda inayotekelezwa na EAC.

Miradi minne kati ya minane ilipewa kipaumbele na kuandaliwa maandiko ya miradi, usanifu na tathmini ya gharama ili iweze kuombewa fedha za utekelezaji.

Miradi hiyo ni pamoja na Uwanja wa Ndege Pemba na Bandari ya Mpigaduri-Maruhubi iliyokuwa inatafutiwa ufadhili chini ya EAC ambayo imepatiwa ufadhili kupitia vyanzo vingine huku taratibu za utafutaji rasilimali kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa Chelezo na Kivuko kati ya Bandari ya Dar es Salaam, Zanzibar, Pemba, Tanga na Mombasa kutoka vyanzo vingine zikiendelea

. Changamoto ya tatu ilikuwa ni gharama za kushusha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayotoka Zanzibar ambayo ilikuwa ni kwamba, gharama ilikuwa kubwa ikilinganishwa na mizigo inayotoka nje ya nchi.

Ilikuwa Sh 4,000 kwa mizigo ya nje ya nchi inayoingia Tanzania Bara na Sh 11,000 kwa mizigo ya Zanzibar. Balozi Sokoine alifafanua kuwa kwa mujibu wa Kitabu cha Ushuru wa Bandari na Malipo cha Aprili 2013 iliyopitishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), viwango vinavyotozwa kwa mizigo inayotoka Zanzibar ni vya chini ikilinganishwa na viwango vinavyotozwa kwa mizigo inayotoka nchi nyingine kuingia Tanzania Bara.

Changamoto ya nne ni utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia iliyohusu namna ya kugawana mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia itakapopatikana.

Baada ya majadiliano, serikali zote mbili ziliamua kumtumia mshauri mwelekezi, kampuni ya AUPEC ya Uingereza ili atoe ushauri wa kitaalamu kuhusu mgawanyo wa mapato ya rasilimali ya aina hiyo kwa nchi zilizoungana ambayo imekamilisha kazi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa SMT na SMZ.

Hata hivyo, hoja nyingine ilijitokeza kuwa suala la mafuta na gesi asilia liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano na baada ya majadiliano,pande zote mbili zilikubaliana kuliondoa suala la utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika orodha ya mambo ya muungano.

Uamuzi huo uliwezesha Sheria ya Mafuta Na 21 ya mwaka 2015 kutungwa na kuipa Zanzibar Mamlaka ya kuanzisha chombo au vyombo vya kusimamia masuala ya mafuta na gesi asilia kwa kutumia Sheria ya Zanzibar ambapo Zanzibar ilitunga Sheria yake ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016.

Changamoto ya mwisho iliyopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kweye orodha ya mambo ya Muungano ni utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Alisema kutokana na hoja hiyo, ndipo Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano kilikutana Februari 9 mwaka jana mjini Dodoma na kupitisha utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano na kuagiza kwamba hoja hiyo iondolewe katika Orodha ya Hoja za Muungano.

 

WAZAZI nchini wameaswa kuisaidia serikali kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi