loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM apongezwa ujenzi SGR, bwawa la Nyerere

JPM apongezwa ujenzi SGR, bwawa la Nyerere

WADAU wa sekta binafsi nchini wamepongeza ujenzi miundombinu ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere kwa kuwa vitasaidia kuchochea fursa za uwekezaji hususani kwenye viwanda kwenye maeneo mbalimbali.

Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) jijini Dar es Salaam juzi kwa lengo la kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mchango wake kuinua sekta binafsi, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula alisema ujenzi wa miundombinu ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika kuinua uchumi wa taifa.

“Kwa miaka mitano Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imefanya makubwa sana na yenye tija kwa uchumi wa Taifa, tunaamini kama wawekezaji tutatumia kila fursa inayopatikana kufanya uwekezaji kulingana na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali,” alisema Ngalula.

Alisema ujenzi wa SGR na miundombinu mingine likiwemo Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 vitaongeza soko la ajira kwa vijana nchini na hivyo kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa.

“Katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ambayo imechangia upatikanaji wa ajira kwa vijana wa kitanzania na ajira zaidi zitakuja punde ujenzi wa miundombinu hiyo utakapokamilika kwa kuwa wadau wa sekta binafsi watawekeza katika miundombinu hiyo,” alisema Ngalula.

Alisema ujenzi wa reli hiyo utaongeza kiwango cha mizigo itakayosafirishwa kutoka tani milioni tano kwa mwaka kwa sasa na kufikia tani milioni 14 kwa mwaka.

“Ujenzi wa SGR utasaidia kuongeza kiwango cha mizigo itakayosafirishwa kutoka tani milioni tano kwa mwaka kwa sasa hadi tani milioni 14 kwa mwaka pindi ujenzi utakapokamilika,” alisema na kuongeza kuwa hali hiyo itaongeza tija kwenye uchumi na ukuaji wa biashara kwa nchi.

Aidha, ameiomba serikali kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo kama ambavyo imefanya kwa kipindi chote cha miaka mitano ili kujenga uchumi imara na wenye kuleta tija kwa wananchi.

“Katika nchi nyingi zilizoendelea zilifanya hivyo kwa kuweka mazingira rafiki ili wadau wa sekta binafsi waweze kufanya uwekezaji,” alisema bosi huyo wa sekta binafsi nchini.

“Tunaipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri na sisi tunaahidi kuyatumia ili kuongeza ufanisi na kuchochea mageuzi makubwa ya kisekta yanayoazimiwa na Serikali ya Awamu ya Tano,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Chama cha Wafanyabiashara Wadogowadogo (Vibindo Society), Gaston Kikui alisema miaka mitano ya Rais Magufuli kwao ilikuwa na neema kubwa kwa upande wao.

“Rais Magufuli amefanya makubwa hasa kwa kutujali wafanyabiashara ndogondogo kwa kutuletea mfumo wa vitambulisho ambavyo vimetuondolea kero ya kukamatwa na kufukuzwa katika maeneo ya kufanyia biashara zetu na sasa tupo huru,” alisema Kikui.

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda nchini, Michael Haule alisema kupitia vikundi vyao wameweza kupata bima ya afya kwa gharama nafuu.

“Kwa upande wa waendesha bodaboda miaka mitano iliyopita imekuwa yenye manufaa makubwa kwetu kwani serikali imetuwezesha kupata bima ya afya kwa gharama nafuu na tumejiona watu tunaothaminiwa,” alisema.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi