loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wakandarasi wazawa gesi,  mafuta kuwezeshwa vifaa

Wakandarasi wazawa gesi, mafuta kuwezeshwa vifaa

KERO ya kusuasua kwa wakandarasi wazawa kushiriki miradi mikubwa ya kimkakati nchini kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na mitaji, umepata dawa baada ya Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi nchini (ATOGS), kuingia Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Kampuni ya RentCo Africa kuwawezesha wakandarasi hao kupata vifaa.

Akizungumza jana jijini Dar e Salaam wakati wa kutiliana saini mkataba huo, Mwenyekiti wa ATOGS, Abdulsamad Abdulrahim alisema hiyo ni fursa nzuri kwa wakandarasi wazawa wakiwamo wa mafuta na gesi kuchangamkia zabuni za miradi hiyo na kisha kukopa vifaa vya kazi kwa muda wa mradi na kuvirejesha.

“Mwanzoni wakandarasi wazawa walikuwa wanalia hawana mtaji wala vitendea kazi vya kuingia kwenye zabuni za miradi mikubwa ya mafuta na gesi kwani wakienda benki watu wa benki wanataka dhamana kubwa na uoneshe uwezo wako wa vitendea kazi, sasa kupitia RentCo Africa wakandarasi wanakopeshwa vifaa hivyo kwa muda wa zabuni kisha wanavirudisha,” alisema Abdulrahim.

Alisema fursa hiyo ni kwa wakandarasi mbalimbali wakiwemo wa mafuta na gesi, miundombinu, uhandisi, ulinzi na wengine na kuwataka wale wa mafuta na gesi kuchangamkia zabuni zitolewapo kwenye Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani jijini Tanga.

Alisema mkataba baina ya ATOGS na RentCo Africa ni chachu ya kuwezesha sera ya nchi kuwa miradi yote mikubwa inayopangwa kutekelezwa nchini, asilimia 30 ya mradi inapaswa zabuni zake zifanywe na wakandarasi wazawa.

Hata hivyo, kutokana na changamoto ya mitaji na ukosefu wa nguvu ya kununua vifaa ambavyo ni gharama kubwa, wakandarasi hao wazawa wengi walishindwa kushiriki kutokana na kukosa mtaji na masharti magumu ya benki.

Akizungumzia mkataba huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa RentCo Africa –Ukanda wa Afrika Mashariki, Robert Nyasimi alisema wameingia makubaliano na jumuiya hiyo kwa lengo la kuwasaidia wakandarasi wazawa baada ya kuona wengi hawawezi kushiriki miradi mikubwa kutokana na changamoto ya vifaa.

“Tunafanya kazi na benki mbalimbali za biashara tunatoa vifaa vya kiutendaji na tunawakopesha wakandarasi hao vifaa vya kazi kwa muda wa zabuni kwa maana sio rahisi mkandarasi mzawa akajitosheleza kwa kuwa na vifaa, kwanza ni ghali na mtaji ni mkubwa,” alisema Nyasimi.

Mkurugenzi wa Benki ya Biashara ya Maendeleo (TDB) Ukanda wa Afrika Mashariki, Lloyd Muposhi alisema kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita wameikopesha Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ukiwemo Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

“Lakini swali kubwa ni jinsi gani miradi hii mikubwa inawanufaishaji wakandarasi wazawa, kwa sababu asilimia 80 hadi 90 ya fedha zinazotolewa kutekeleza miradi hiyo barani Afrika zinarudi Ulaya na nchi nyingine za nje, kwa sababu wakandarasi wanatoka huku, lakini kama wakandarasi wazawa watashiriki na hivi sasa wanawezeshwa vifaa na mitaji, fedha nyingi zitabaki Afrika,” alieleza Muposhi.

Meneja Mwandamizi wa Mikopo ya Miradi Mikubwa wa Benki ya CRDB, Focus Mrosso alisema kilio kikubwa cha wakandarasi wazawa ilikuwa ni mtaji na vifaa, na kuwa benki hiyo sasa inawawezesha kupata mitaji baada ya wao kuwa na vifaa.

“Mkandarasi mzawa akiwa na vifaa na amepata zabuni kwenye mradi ya maendeleo nchini, sisi tunamwezesha kwa kuweka mfano mafuta kwenye vifaa hivyo kama ni mashine ya migodi au vijiko vya kutengeneza barabara na tunafanya hivyo ili asikwame wakati akisubiri kulipwa na mwenye mradi,” alisema Mrosso.

Alisema benki hiyo imetenga Sh bilioni 50 kwenye miradi miwili wa SGR na ule wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji na kwamba hadi sasa Sh bilioni 30 zimeshatolewa kwa wakandarasi hao.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/307795a439f2c8b68194fca955b27617.jpg

Sehemu kubwa ya ulimwengu wa biashara uli dorora kutokana na ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi