loader
Dstv Habarileo  Mobile
Lucy Ngowi

Lucy Ngowi

MCHICHA ni aina nyingine za mboga zinazotumiwa na Watanzania huku aina hii ya mboga ikiwa miongoni mwa zinazopendwa sana na Watanzania.

“Katika mboga, mimi ninapenda sana mchicha, kisha matembele, mlenda (wa bamia), kisamvu na mnavu. Sipendelei sana spinachi kama mume wangu,” anasema Devota Sime, mama lishe na mkazi wa Temeke.

Anasema katika biashara yake ya mama lishe, huwapikia mbogamboga wateja wake lakini mara nyingi huchangaya mchicha na spinachi na wakati mwingine huwaandalia kisamvu.

“Kisamvu huwa ninapikia wateja wangu ninapokuwa na karanga,” anasema Devota.

Mchicha ambao makala haya yanauangazia kwa kina umekuwa ukilimwa tangu miaka ya 6000 na 8000 iliyopita.

Taarifa zilizopo zinaonesha kwamba asili yake ni Amerika ya Kati na Mexico, baadae mchicha ukasambaa India, Nepal, China, Urusi, Ulaya Mashariki, Amerika Kusini na hatimaye ukaufikia Afrika.

Kulinganisha na aina nyingine za mboga kama spinachi, mchicha kwa Watanzania wengi unachukuliwa kama mboga ya asili.

Mchicha upo kwenye familia inayoitwa Amaranthaceae inayojumuisha aina zaidi ya 60.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mikocheni jijini Dar es Salaam, kimeanzisha mradi wa kuendeleza zao hilo ujulikanao kama ‘Mchicha ni Zao la Kushangaza’.

Mradi huo umebuniwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na tasisi ya The World Vegetable Centre ukilenga, siyo tu kuboresha afya za walaji, bali pia usalama wa chakula na kuwaingizia kipato wakulima na wafanyabiashara wa mboga.

Mradi pia unalenga kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora zinazopendwa na wakulima pamoja na walaji.

Ni mradi unaoshirikisha wakulima kutoka wilaya sita za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwenye maeneo ya Bagamoyo, Kigamboni, Kinondoni, Temeke, Ilala na Ubungo. 

Pascal Fabian, mkulima wa mchicha wa Kiluvya, kata ya Kibamba, wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam anasema pamoja na zao hilo kumpatia mahitaji yake na familia, limekuwa na changamoto za hapa na pale, hususani ubora wa mbegu.

Hata hivyo, anasema serikali kupitia watafiti wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mikocheni wamekuwa wakizitatua changamoto hizo kupitia utafiti wa mbegu bora na zenye matokeo chanya.

Fabian anasema pia TARI imekuwa ikimwelekeza yeye na wakulima wenzake mbinu bora za kilimo pamoja na kuongeza thamani katika zao hilo kwa njia mbalimbali.

Fabian anayelima zaidi ya ekari mbili za mchicha katika eneo hilo la Kiluvya, anasema miezi ya Agosti hadi Oktoba kumekuwa na tatizo la soko linalosababisha mafungu ya mchicha wa jumla kuanza kuuzwa kati ya Sh 50 hadi 100, kiasi ambacho anasema ni kidogo ikilinganishwa na nguvu inayotumika.

Lakini anasema pia ugumu wa soko hilo unatokana na wafanyabiashara wa zao la mchicha kutoka mikoa mingine ikiwemo Morogoro, Dodoma na Iringa kuuza mboga zao Dar es Salaam na hivyo kufanya biashara kuwa ya ushindani mkubwa.

Anaomba serikali iwatafutie soko ambalo wataweza kuuza mboga zao kwa bei nzuri, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kupata teknolojia za usindikaji.

Mkulima mwingine, Abdalah Pazi wa Chambezi Bagamoyo mkoani Pwani, ni miongoni mwa waliopata mafunzo ya ulimaji bora wa mchicha kutoka TARI Mikocheni.

Anasema kabla ya mafunzo hayo alikuwa akilima mchicha bila kufuata kanuni bora na kwamba alikuwa akilima kwenye eneo dogo kwa ajili ya matumizi yake ya nyumbani.

Anasema elimu hiyo imemwezesha kulima kisasa mchicha kibiashara na sasa unamsaidia pia kujikimu kimaisha.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Fatuma Latu ambaye alikuwa mgeni rasmi siku hiyo ya wakulima iliyoadhimishwa hivi karibuni, anawapongeza watafiti, maofisa ugani na wakulima ambao wameshiriki kwenye mradi huo wa mchicha tangu mwaka 2018.

Anasema juhudi zinazolenga kuleta mafanikio makubwa kwenye sekta ya kilimo na kuchangia katika kuboresha ajira za wakulima wa mchicha na wafanyabiashara wa mboga huku walaji pia wakipata faida ya miili yao kurutubika.

Anasema mradi huo unaotekelezwa nchini maeneo ya Pwani na Kanda ya Kaskazini umeshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wasindikaji, walaji, wafanyabiashara, wazalishaji mbegu, maofisa ugani na wauzaji wa pembejeo za kilimo.

Wadau wengine waliohusishwa ni maofisa afya, maofisa lishe, walimu, wanafunzi na taasisi zisizo za kiserikali.

Mkurugenzi huyo anaamini mpaka sasa mazao mengi ya asili ukiwemo mchicha hayajapewa kipaumbele cha kutosha kwenye utafiti au mipango mikubwa ya maendeleo ya kilimo nchini.

“Kwa hiyo bado mchicha unahesabika kwenye kundi la mazao yaliyosahaulika,” anasema.

 

Anasema matumizi ya mbogamboga kwa wingi kwa mjamzito na mtoto yanasaidia sana katika kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto.

Kwa mujibu wa Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), udumavu ni hali ya viungo vya mwili vya mtoto, ukiwemo ubongo kutokomaa vyema tangu mimba inapotungwa hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili kutokana na lishe duni aliyopata mama ama mtoto baada ya kuzaliwa.

Mkurugenzi Latu anasema tatizo la udumavu wakati mwingine huchangiwa na elimu ya lishe kuwa duni ama kukosekana kwa mazao muhimu yenye vitamini na madini kwa wingi ikiwemo mchicha.

Anasema pamoja na kwamba utapiamlo nchini Tanzania unapungua bado viwango vyake viko juu kulinganisha na viwango vya kimataifa vinavyokubalika.

Anasema viini lishe vyote muhimu vinapatikana kwa wingi na kwa gharama nafuu kwenye zao la mchicha, hivyo ulaji wa mchicha unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa matatizo hayo.

Anasisitiza kuwa ili mlaji aweze kupata viini lishe hivyo kwa kiasi cha kutosha ni lazima mchicha uandaliwe kwa ubora unaotakiwa.

“Aina mbalimbali za mchicha nazo zinatofautiana kwenye viwango vya viinilishe. Pia kuna tofauti kati ya viwango vya viinilishe kati ya mbegu na majani ya mchicha,” anasema.

Anasema tafiti za mradi huo zimelenga kuongeza uzalishaji kupitia upatikanaji wa mbegu bora zenye ukinzani dhidi ya mazingira magumu lakini zinazopendwa na wakulima na walaji.

Vile vile mradi pia unahusika na tafiti za kuboresha mapishi na maandalizi ya mchicha ili uweze kumfikia mlaji ukiwa na viwango vya kutosha vya viinilishe muhimu ambavyo ni Vitamini C, A na madini chuma yanayohusika sana katika utengenezaji wa damu mwilini.

Mratibu wa mradi huo, Dk Ruth Minja kutoka TARI Mikocheni anasema kuna aina mbalimbali za mchicha na kwamba hutofautiana kulingana na rangi za maua na majani.

Anasema kuna mchicha wa zambarau, mwekundu, kijani, mchicha wa majani membamba, majani mapana na kadhalika.

Dk Minja anasema mradi huo uliangalia mchicha kwa namna ya tofauti na ilivyozoeleka, siyo tu kuchuma majani yake na kupika bali kuona mengi yaliyopo kwenye zao hilo.

Anasema kwenye mradi huo waliona jinsi ambavyo majani yake yana virutubisho vingi vinavyohitajika mwilini pamoja na mbegu zake zinaweza kutumika kama lishe bora kwa wagonjwa.

Anasema mchicha ukitumiwa kwa usahihi na walaji una virutubisho vya kutosha katika kupambana na matatizo ya udumavu na upungufu mwingine wa lishe.

Anasema mapishi bora ya mchicha ni yale yanayowezesha uhifadhi wa viinilishe kwa maana ya vitamini na madini vilivyoko ndani yake kwa ajili ya afya ya mlaji.

“Viinilishe, mfano vitamin C na B ni rahisi kupotea kutokana na aina ya mapishi. Hivyo osha mchicha kabla ya kuukatakata kuepuka kupotezea viinilishe kwenye maji. Pia muda unaotumika kuupika unapaswa kuwa mfupi kulingana na ugumu wa majani lakini usizidi dakika 10,” anasema na kuongeza kwamba hata dakika tano zinatosha kuivisha mchicha.

Kuhusu ajira anasema kilimo cha mchicha kibiashara ni ajira tosha kwa sababu watu wanataka kula mchicha kila siku.

Kutokana na faida za mchicha anasema hata majirani zatu wa Kenya nao wanaendesha mradi kama huo. Anasema mradi unafadhiliwa na  serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la maendeleo la BMZ.

“Lakini fedha za ufadhili zinapitishwa kwenye taasisi ya mboga ya kimataifa ya uendelezaji wa mazao ya aina za mboga ambayo makao yake makuu yapo Taiwan,  makao makuu kwa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika yapo mkoani Arusha, Tanzania,” anasema.

Kwa maelezo yake TARI imekuwa ikiendeleza kilimo cha mboga nchini hasa upatikanaji wa mbegu mpya bora.

Anasema baada ya tafiti zilizofanywa na taasisi mbalimbali za Tanzania wakishirikiana na Taasisi ya Mboga ya Kimataifa kuna aina tano za mchicha zilizopasishwa na tume ya udhibiti wa mbegu bora ambazo tayari ziko madukani.

Anataja aina hizo za mbegu kuwa ni madeira 1, Madiira 2, Akeri, Poli na Ngurumo.

“Mchicha ni mojawapo ya mboga zinazolimwa mijini na vijijini na unastawi kwenye aina mbalimbali za udongo na hali ya hewa tofauti. Zao hili hulimwa kwa matumizi ya nyumbani na biashara. Kilimo cha mchicha huchangia usalama wa chakula na lishe bora duniani,” anasema.

Meneja wa TARI Mikocheni na Chambezi, Dk Zuberi Bira anasema kituo hicho ni mojawapo ya vituo 17 vya taasisi hiyo ambacho kina majukumu mawili mojawapo likiwa ni utafiti na uendelezaji wa zao la minazi, pia utafiti wa matumizi ya bayoteknolojia kwa kilimo chenye tija.

Anasema kituo hicho pia kinaruhusiwa kufanya utafiti wowote wa kilimo mbali na majukumu yake ya kitaifa, mfano wanafanya utafiti wa mazao miti ikiwemo miembe, michungwa pamoja na kilimo cha mseto ndani ya shamba la minazi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/21fab22bd857e2c4549664e6967cd3af.jpg

Sehemu kubwa ya ulimwengu wa biashara uli dorora kutokana na ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi