loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Ukarabati Shule ya Sekondari Mpwayungu wapunguza utoro

UJENZI na ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Sekondari Mpwayungu wilayani Chamwino, umepunguza utoro na kuongeza ufaulu miongoni mwa wanafunzi.

Akitoa ripoti ya ujenzi na ukarabati wa shule, Mkuu wa shule hiyo, Daniel Makame alisema miundombinu ya shule hiyo imejengwa na kukarabatiwa kwa gharama ya Sh milioni 158.1.

Makame alisema kabla ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo, wanafunzi wengi walikuwa wakiacha masomo. Kwa mfano alisema wanafunzi wa kidato cha tatu, walianza 80 na sasa wamebaki 48.

"Lakini ujenzi na ukarabati wa miundombinu umefanya wanafunzi wengi kubaki shuleni kutokana na kuwa na mazingira wezeshi. Kwa mfano wanafunzi wa kidato cha kwanza walianza 118 hadi sasa wapo kidato cha pili  wapo 102 na wanaendelea na masomo," alisema.

Makame alisema katika kuhamasisha ufaulu, madarasa yaliyokarabatiwa wamepewa kusomea wanafunzi wa madarasa ya mitihani kidato cha pili na nne ili kuwaongezea ari ya kusoma na kuhamasisha ufaulu.

Ujenzi na ukarabati huo uliofanywa kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), ulianza Februari mwaka jana kwa kutumia Sh milioni 101.4 kujenga nyumba mbili kwa pamoja.

"Vilevile shilingi milioni 39 zimetumika kukarabati vyumba vya madarasa na shilingi milioni 6.7 zimetumika kujenga matundu ya vyoo,” alisema.

Pia kutokana na wananchi wenye watoto wanaosoma shule kuhamasishwa kuchangia nguvu zao, wamechangia mchanga, kokoto na mawe kwenye madarasa kwa gharama ya Sh milioni 6.7 na kwenye matundu ya vyoo ya gharama ya Sh milioni 4.8 na hivyo kufanya mchango wao kuwa jumla ya Sh milioni 11.52.

Makame alisema kamati ya ujenzi iliyokuwa chini yake ilijiongeza, kwani badala ya kukarabati majengo matatu wamekarabati sita na matundu ya vyoo 10, yakiwamo ya wasichana sita na wavulana manne.

Jiwe la msingi la shule hiyo liliwekwa  Novemba 11, 2008 na Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda.

Shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madarasa na vyoo kwa wanafunzi na vilivyokuwapo vilikuwa vimechakaa.

Akizungumza baada ya kukagua ukarabati wa madarasa na vyoo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alipongeza juhudi zilizofanywa na kamati ya ujenzi wa shule kwa kujenga na kukarabati majengo. Alieleza kuwa majengo hayo yamechangia kuongeza ufaulu na mahudhurio ya wanafunzi katika sekondari hiyo.

MKURUGENZI Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Chamwino

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi