loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

‘Waandishi fuateni kanuni mpya EPOCA’

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kufanya kazi zao kwa kufuata kanuni mpya, zilizoongezwa kwenye sheria mpya ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA).

Pia wametakiwa kuacha ushabiki wa mambo mbalimbali yanayoweza kuhatarisha usalama ili kusaidia wananchi kupata taarifa zilizofanyiwa kazi na ambazo zipo katika mrengo sahihi.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu  alisema hayo kwenye semina ya siku moja iliyoandaliwa na APC kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa wanahabari mkoani humo.

Alisema ni vyema waandishi wa habari katika shughuli zote wanazozifanya, ziendane na sheria kanuni na taratibu zote walizowekewa ili kuepuka kuingia kwenye migogoro ya kisheria na mamlaka za serikali.

Gwandu alisema APC kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kufanya mazungumzo na mamlaka za kiserikali ili kuondoa kanuni na sheria ambazo zinaonekana kuminya uhuru wa habari, hivyo wakati mazungumzo yakiendelea ni vyema kama wanahabari wakafuata sheria zilizopo kwanza.

Alisema mwandishi anahitajika kupewa elimu na kukumbushwa masuala yanayomgusa moja kwa moja katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.

Ofisa Mawasiliano wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Rolf Kibaja aliwataka wanahabari kuacha mihemko, badala yake waandike habari zenye ulinganifu, mizania na kwa ufasaha sambamba na kujiepusha na maoni yao binafsi.

Kibaja aliwakumbusha waandishi kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ndiyo yenye jukumu la kutoa matokeo ya uchaguzi na si wao kujitwika majukumu ambayo si ya kwako. Alisisitiza endapo kutakuwa na tashwishwi yoyote ni vyema wapate majibu sahihi kutoka kwa tume yenyewe

Aliwasihi wanahabari kuzingatia na kufuata kanuni na maadili maudhui mtandaoni na kuhakikisha habari kabla haijapelekwa kwa walaji, lazima iwe na usawa pande zote mbili ili kuleta tija katika jamii, bila kusahau kuzingatia Kanuni ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 Namba 343.

Makamu Mwenyekiti wa APC, Musa Juma aliwasilisha mada ya usalama wa waandishi kazini na mitandao ya kijamii na kueleza kuwa mitandao ya kijamii ina faida na hasara zake. Aliwataka wanahabari kuacha kuweka taarifa zao muhimu katika mitandao hiyo, kwani ni rahisi mtu yeyote kuwafuatilia na hata kudhurika pia.

Aliwataka kufahamu kuwa kwa miaka ya sasa ni vigumu kuishi bila kutumia intaneti kwa namna moja ama nyingine, lakini intaneti hiyo ina madhara. Alitoa mfano wa kuwapo kwa taarifa za uongo, kichaka cha uhalifu, hurahisisha udanganyifu wa taaluma na ni chanzo cha kusambaa kwa virusi vya kompyuta.

Musa alisema mitandao hiyo ikitumika vizuri, zipo fursa mbalimbali za kufungua milango mipya ya chombo kingine cha habari na  pia imewaleta watu wengi kwa karibu zaidi.

Alisisitiza waandishi wanatakiwa kutambua kuwa maisha yao yana thamani kubwa kuliko kitu chochote kile, hivyo ni vyema waitumia kwa umakini wa hali ya juu.

Aliwataka waandishi wa habari kutawala matumizi yao na kuzingatia kanuni za usalama mitandaoni ili wasiathirike.

MSANII wa Bongo fl eva , Zuwena Mohammed ...

foto
Mwandishi: Veronica Mheta, Arusha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi