loader
China yataka uchaguzi wa Tanzania kutoingiliwa

China yataka uchaguzi wa Tanzania kutoingiliwa

SERIKALI ya China imesisitiza msimamo wa nchi hiyo na kuyataka mataifa mengine kutoingilia masuala ya ndani ya nchi mbalimbali duniani, ikisema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kusimamia uchaguzi wake mwenyewe.

Kauli hiyo imetolewa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Zhao Lijian wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari mjini Beijing nchini humo.

“Tunaamini kuwa Serikali ya Tanzania na watu wake wana busara na uwezo wa kuendesha uchaguzi. Tunawaombea uchaguzi uwe salama na wenye mafanikio. Kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine inapaswa kuwa kanuni ya kufuatwa na nchi nyingine duniani. China inazitaka nchi zote kuheshimu kanuni hii na pande zote zinapaswa kuunga mkono uhuru wa nchi za Afrika na kulinda uhuru na uimara wao,” alisema Zhao.

Msemaji huyo wa Serikali ya China aliulizwa kuhusu maoni yake baada ya kuripotiwa kuwa Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wake Oktoba 28, mwaka huu, na kwamba Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania hivi karibuni ulitoa taarifa juu ya uchaguzi huo ikiitaka Serikali ya Tanzania idumishe mchakato wa demokrasia, ikibainisha kuwa haitasita kuchukua hatua kwa watakaobainika kusababisha vurugu au kuvuruga mchakato huo wa demokrasia.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Balozi wa China nchini, Wang Ke kutoa wito kwa mataifa mengine duniani kuheshimiana na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio chochote kile na kueleza kuridhishwa kwake na namna mchakato wa Uchaguzi Mkuu unavyoendelea nchini.

Balozi Wang aliyasema hayo wakati wa mazungumzo yake na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge. Alisema kuwa ni lazima mataifa yote yaendeleze uhusiano mwema miongoni mwao na kutoingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine.

Aidha, alisema kuwa China itaendelea kuheshimu masuala ya ndani ya mataifa yote, Tanzania ikiwamo. Alieleza kuridhika kwake na mchakato wa kampeni za Uchaguzi Mkuu zinavyoendelea nchini na kuwatakia Watanzania kila la heri katika uchaguzi huo.

Katibu Mkuu Balozi Brigedia Ibuge alisema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na China kisiasa, kiuchumi na kijamii ni madhubuti na imara. Alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea pia kuheshimu ushirikiano na mataifa mengine.

Aliishukuru China kwa ushirikiano wake wa kimkakati kwa Tanzania. Alisema uhusiano huo utaendelea kudumishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/cf5d4ac520599bed2edc934b3f611f27.jpg

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi