loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Uswisi yaipa Tanzania bil 40/-kukabili malaria

SERIKALI imepokea msaada wa Sh bilioni 39.59 kutoka nchi ya Uswisi kwa ajili ya kugharamia mradi wa uboreshaji wa afya na uimarishaji wa mfumo wa afya na programu ya kutokomeza malaria nchini.

Kiasi hicho cha fedha kinafanya jumla ya Sh bilioni 83.7 ambazo serikali ya Tanzania imezipokea kutoka Uswisi kwa ajili ya miradi hiyo ya afya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alisema fedha hizo zimetolewa bure bila masharti yoyote.

Akizungumza wakati wa kutiliana saini makubaliano ya msaada huo, James alisema fedha hizo zilizotolewa kwa nyakati tofauti ndani ya kipindi hiki cha Oktoba na zitapelekwa moja kwa moja Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema Sh bilioni 24.5 zitapelekwa kwenye wizara hiyo kwa ajili ya mradi wa afya na uboreshaji wa mfumo wa afya na Sh bilioni 15.08 zitapelekwa kwa ajili ya programu ya kutokomeza malaria.

Alisema mbali na mikataba hiyo miwili iliyosainiwa jana, Oktoba 6 Mwaka huu, Serikali ya Tanzania na Uswisi zilisaini mkataba wa msaada wa Sh bilioni 44.01, hivyo kufanya fedha zilizotolewa na taifa hilo kwa Tanzania kufikia Sh bilioni 83.69

"Ikumbukwe kuwa huu ni msaada usio na masharti yoyote kwa nchi yetu, jambo linaloonesha kuwa Tanzania na Uswisi ni marafiki wa kweli wanaoshirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma za jamii," alisema James.

Aliishukuru serikali ya Uswisi kwa msaada huo na kuihakikishia kuwa fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa kusaidia utekelezaji wa sera ya kitaifa ya kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini.

Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chasso, alisema msaada huo ambao siyo wa kwanza kutolewa kwa Tanzania, umelenga kudumisha ushirikiano wa mataifa hayo mawili huku akisisitiza kuwa Uswisi bado itaendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa Tanzania.

Alisema kupitia mipango mbalimbali ya taifa hilo ikiwemo kukabiliana na magonjwa, serikali ya nchi Uswisi iliona vyema kutoa fedha hizo kwa Tanzania ili iweze kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara hiyo, Dk Leonard Subi, alisema fedha hizo zitatumika kama ilivyopangwa huku akiamini kuwa kupitia msaada huo kutaongeza kasi ya kupambana na ugonjwa wa malaria.

Aliishukuru serikali ya Uswiswi kwa msaada huo pamoja na serikali yaTanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kutafuta misaada inayosaidia kupambana na magonjwa mbalimbali jambo ambalo limekuwa na tija kwa jamii.

WENYE ligi yao wameanza kurejea kwenye nafasi zao. ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi