loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

China yatoa msaada wa mil 150/- kudhibiti moto mlima Kilimanjaro

CHINA imetoa msaada wa Sh milioni 150 kudhibiti moto uliozuka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro nchini ambao hata hivyo mpaka sasa umeishadhibitiwa kwa asilimia 95.

Aidha, imeelezwa kuwa moto unaoendelea kuwaka kwa sasa unatoka chini ya ardhi na mpaka sasa watu 300 wanaendelea kudhibiti mito huo mchana na usiku wakati upepo unapovuma na kuuibua katika majani na miti mikavu.

Akikabidhi msaada huo, Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke alisema kati ya fedha hizo Sh milioni 50 zimetolewa na ubalozi huo na Sh milioni 100 zimetolewa na kampuni za ujenzi toka China zinazofanya kazi nchini.

Alisema China wamekuwa wakisaidia Tanzania katika majanga mbalimbali na jambo linaloonesha uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo kati yan chi hizo mbili.

Alisema walisaidia pia wakati wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19).

“Msaada huu ni kusadia kununua vifaa vya kuzima moto kwenye mlima huo mkubwa Afrika ambao ni kivutio cha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani, pamoja na kusaidia kuhifadhi mazingira kutokana na kuteketea kwa viumbe hai katika maeneo ya hifadhi,” alisema Wang.

Akipokea msaada huo, Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) Kanda ya Kaskazini, Herman Bariho alisema moto katika Mlima Kilimanjaro ulianza Oktoba 11 mwaka huu na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na watu zaidi ya 800 walifanikiwa kuudhibiti kwa asilimia 95.

Alisema sababu ya moto bado uchunguzi unaendelea lakini inaelezwa ni kutokana na shughuli za binadamu na sasa moto ulio chini ya ardhi unapopulizwa na upepo unawaka upya katika majani na miti katika uwanda wa juu ambao ni kichocheo cha moto kwa sasa. Alisema watu 300 wanaendelea kuudhibiti usiku na mchana.

Bariho alisema kwa msaada waliopata kutoka ubalozi wa China itasaidia katika kupata vifaa vya kuzimia moto, tochi kwa ajili ya kudhibiti moto usiku na nguo kudhibiti baridi na vifaa vingine kutumika hapo baadaye ikitokea tatizo kama hili.

Bariho alibainisha kuwa athari za moto huo si kubwa sana na zaidi ya katika uharibifu wa mazingira kwani eneo lililoungua ni asilimia tano ya eneo la uhifadhi ambapo mimea kadhaa iliharibika pamoja na wadudu wanaotembea taratibu ambao ni makinda ya ndege, nyoka na wadudu.

"Shughuli za utalii hazijaathirika na zinaendelea kama kawaida, watu wanaendelea kupanda mlima kwani moto si kikwazo cha shughuli za utalii," alisema

Alibainisha kuwa katika kukabiliana na majanga kwa nyakati nyingine zaidi ya mipango waliyonayo ya kila siku wataendelea kuboresha na katika moto huo wamepata funzo la kuhakikisha wanapata helkopta ya kuzima moto juu na pembeni mwa mlima.

Alisema moto huo uliozuka katika hifadhi hiyo Oktoba 11 mwaka huu umeteketeza kilometa za mraba 95.5 sawa na asilimia tano ya eneo lote la hifadhi lenye kilometa 1,700 na ulianzia eneo la Whona ambako ni kituo cha kupumzikia wageni.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

2 Comments

 • avatar
  Isaac Mrithi
  25/10/2020

  Sawa kabisa,na Mungu yupo upande wa tz, shida la moto litapita tu. Asante kwa kutupatia taarifa Theopista.

 • avatar
  Isaac Mrithi
  25/10/2020

  Sawa kabisa,na Mungu yupo upande wa tz, shida la moto litapita tu. Asante kwa kutupatia taarifa Theopista.

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi