loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Agizo la JPM kumaliza mgogoro viwanja Kyebitembe latekelezwa

MGOGORO wa viwanja katika Mtaa wa Kyebitembe uliopo katika Kata ya Nshambya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera uliodumu kwa zaidi ya miaka 22 sasa umemalizwa.

Mgogoro huo ulisababisha kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani na sasa umemalizika baada ya serikali kuingilia kati.

Hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Septemba 16 mwaka huu, akiwa katika mkutano wa kampeni mjini Bukoba.

Rais Magufuli aliiagiza Serikali ya Wilaya Bukoba kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa viwanja Kyebitembe ili kuwawezesha wananchi kuishi kwa uhuru na usalama.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kupitia kwa viongozi wake waliomaliza muda wao wakiwemo maofisa ardhi, walipanga kubomoa nyumba za wananchi 374.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya wanyonge, hivyo haipo tayari kuona wananchi wakiteseka na kuhangaika kwa makosa ya wataalamu waliokuwa wanahusika na masuala ya ardhi ambao walikuwa wakiuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja na kusababisha migogoro.

"Mimi nimeletwa Bukoba na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na siyo kuona wananchi wakiteseka, mgogoro huu umedumu kwa miaka 22 na kuna watu wamekuwa wakinufaika na mgogoro huu bila kujali wananchi wanaoumia, kwa hiyo kuanzia sasa nafuta ramani ya zamani ili ichorwe mpya ambayo itaendana na hali halisi ya makazi ilivyo sasa, na kuanzia sasa hakuna kubomoa wala kugusa nyumba yoyote iliyojengwa hata kama ni msingi tu," alisema Kinawiro.

Kinawiro aliongeza kuwa wale wote waliokuwa wakilalamikia viwanja ambavyo tayari viliuzwa na waliouziwa wameshajenga, halmashauri iwatafutie viwanja vingine ndani ya muda mfupi na wale waliokwisha jenga waachwe waendelee na maisha yao.

Pia aliwataka wananchi kwa kushirikiana na kamati ya urasimishaji walioichagua wenyewe wafanye mchakato wa haraka wa kuchanga pesa kwa ajili ya kupimiwa viwanja vyao kwa wakati na kuwawezesha kupata hati ili kila mmoja awe na umiliki unaotambulika kisheria.

Mara baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati   ya Urasimishaji, Fakharudini Nuru,  alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa uamuzi alioufanya na kueleza kuwa migogoro hiyo imekuwa ikiathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na  malumbano baina ya wananchi.

Fakharu alisema kuwa ataendelea kuwahamasisha wananchi wenzake ili waweze kuchanga fedha zitakazowawezesha kupimiwa viwanja vyao na hatimaye kupata hati miliki ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima.

Kaimu Kamishina wa Ardhi, Mkoa wa Kagera, Erick Makundi alisema kuwa baada ya serikali kufuta ramani ya zamani na hati zote zilizokuwepo, amewataka wananchi hao kufuata utaratibu kabla  hawajanunua viwanja wala kuanza ujenzi na kuongeza kuwa endapo watawahi kuchanga pesa za urasimishaji, watapewa kipaumbele cha kupimiwa na suala la kupewa hati miliki halitazidi wiki mbili.

MKURUGENZI Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), ...

foto
Mwandishi: Allawi Kaboyo, Bukoba

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi