loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM: Kubinafsisha ndege,  treni na meli ni dhambi

JPM: Kubinafsisha ndege, treni na meli ni dhambi

RAIS John Magufuli amewataka viongozi wa serikali waliopo na wale watakaokuja baada yake, kuacha tabia ya kubinafsisha vitu vya msingi katika nchi kama ilivyofanyika kwa Shirika la Ndege (ATCL), Shirika la Reli (TRC) na meli zilizoachwa na Baba wa Taifa kwani hiyo ni dhambi kubwa.

Akizindua safari za treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga-Moshi hadi Arusha, Magufuli alisema huduma zinazotolewa na mashirika ya umma ni msaada mkubwa kwa wananchi wanyonge.

Katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Arusha, Magufuli alisema reli hiyo ilikufa kwa miaka 30 iliyopita kabla ya serikali yake kuamua kuifufua tena jambo ambalo alisema taifa lilikuwa limefikia mahali pabaya na hilo liwe fundisho kwa Watanzania na vizazi vijavyo kwamba kubinafsisha reli, ndege na meli ni dhambi kubwa.

“Ninyi ndugu zangu wana Arusha na Watanzania mnafahamu hali ya reli ilikuwa imefikia wapi, kijana aliyezaliwa miaka 30 iliyopita hakufanikiwa kuona treni hapa Arusha au Moshi au Tanga, maana yake tulikuwa tumefikia mahali pabaya.

“Na huu ni ukweli na siwezi kuuficha, na hili liwe fundisho kwetu sisi Watanzania na vizazi vinavyokuja baadaye, kwamba kubinafsisha ndege, treni na meli ni dhambi kubwa,” alisema Rais Magufuli.

Alisisitiza, “ Lakini niwaombe viongozi wenzangu serikalini, hili liwe fundisho kwetu, tusikubali tena kubinafsisha binafsisha vitu ambavyo ni vya msingi katika nchi, tulibinafsisha ndege zote zikaisha na tumekuja kuanza upya, tukabinafsisha treni tumekuja kuanza upya.”

“Tulikuwa na meli ambazo ziliachwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, nazo hazipo, sasa hili liwe fundisho, mimi sitakuwa Rais wa maisha, lakini natoa ujumbe wangu kwa wale watakaokuja katika maisha ya leo na baadaye, hili liwe fundisho.”

Magufuli alisema hata katika nchi zilizoendelea hawajabinafsisha mashirika yao ya reli bali yanabaki kuwa ndani ya serikali na yanapobaki kuwa ndani ya serikali inakuwa rahisi kufikisha huduma kwa wananchi wanyonge.

Hata hivyo, Rais Magufuli alifurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Bodi ya TRC na uongozi wa TRC kwa kazi nzuri waliyofanya ya kukarabati reli hiyo, mabehewa na vichwa vya treni jambo lilosaidia kurejeshwa kwa usafiri kati ya Dar es Salaam-Tanga-Moshi na Arusha.

Alisema miundombinu ya usafiri ni kichocheo kikubwa kwa ustawi wa shughuli za kiuchumi na uzalishaji ikiwemo viwanda, biashara, kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii na uchimbaji madini. Alisema ukosefu au ubovu wa miundombinu ya usafiri ni kikwazo kikubwa kwa ustawi wa shughuli hizo.

“Tafiti zinaonesha kwamba ukosefu au ubovu wa miundombinu ya usafiri, unapunguza pato la nchi za Afrika kwa asilimia 2 na kuongeza bei ya bidhaa kwa asilimia 40, hili shirika la reli tulilibinafsisha, wakawa wanachukua mabehewa yetu na vichwa wanapeleka huko na matokeo yake pakawa hakuna chochote, lakini pia watendaji wakawa wanastaafishwa na wafanyakazi wakawa wanaachishwa kazi,” alisema Magufuli na kuongeza

TRC imefanya maajabu

“Ndiyo maana nawashukuru sana watendaji wa TRC kwa sababu niliwaeleza kwamba ni lazima sasa tufanye mabadiliko, tuachane na yule aliyekuwa mbia wetu, tujipange sisi Watanzania, tumezoea mno vya dezo, vya kudanganywa, hakuna vya bure duniani, ndiyo maana nasema kwa dhati watendaji wa TRC mmefanya maajabu kwa ajili ya taifa hili, Munga awabariki.”

Magufuli alisema anajua kwamba Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa anapigwa vita lakini chini ya utawala wake atahakikisha anawalinda watendaji wazuri.

Alisema kuna wakati uongozi wa TRC ulimuomba Sh bilioni tano kwa ajili ya kufufua mabehewa kwa kuwa wataalamu wazawa wapo wakiwemo wastaafu, pia walifanya ukarabati wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, lakini pia wamenunua vichwa vipya 11 kutoka Marekani, wamekarabati mabehewa ya mizigo 347 na ya abiria 20 kwa kutumia wataalamu Watanzania.

Rais Magufuli alisema hatua hiyo ya TRC imeongeza uwezo wao wa kusafirisha mizigo kutoka tani 186,963 hadi tani 425,787 mwaka 2019/20 pamoja na kuongeza idadi ya abiria kwenye treni inayofanya safari zake ndani ya Jiji la Dar es Salaam kutoka abiria 1,020,070 mwaka 2014/15 hadi kufikia abiria 6,070,030 mwaka 2019/20 na kutoa ajira mpya 374.

“Sambamba na hili, hivi sasa mnasimamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma takribani kilometa 700 kwa gharama ya Sh trilioni 7.026 itakayotumia umeme na kusafiri kwa mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa na kubeba tani nyingi za mizigo kwa wakati mmoja,” alisema.

Alisema pia serikali imeshatangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa kipande cha Mwanza-Isaka. “Lakini pia hivi karibuni mtaanza ujenzi wa reli ya Katavi kwenda Bandari ya Kalema ili kurahisisha usafiri kati yetu na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),”alisema Rais Magufuli.

Alisema huu ni uthibitisho kuwa Watanzania wanaweza na mradi huo utajenga uchumi kwa kiasi kikubwa.

Magufuli alisema mara  baada ya uchaguzi mkuu, Serikali yake imepanga kununua vichwa vipya 39 vya treni kwa njia kuu, vichwa 18 vya kusogezasogeza, mabehewa 800 ya mizigo na 37 ya abiria, mabehewa ya baridi kwa ajili ya kusafirishia mazoa ya bustani yakiwamo matunda, mboga, viungo na maua.

Alisema anataka TRC liwe mfano katika Afrika kwa mashirika yanayofanya biashara na kufanya kazi kwa kuhudumia wananchi wake wakiwamo wananchi wanyonge.

Alisema kufufuliwa kwa reli hiyo kutasaidia kutunza barabara ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa kutokana na kuharibiwa na magari makubwa ya mizigo.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Ujenzi, Elias Kwandikwa alimshukuru Rais kwa maelekezo yake yaliyowezesha kutungwa sheria iliyounganisha Kampuni ya Reli na Shirika la Reli Assets Holding Company Ltd (RAHCO) akisema matunda yake ni usafiri wa treni kuanza.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema  treni hiyo ni kutoka Dar es Salaam,Tanga, Moshi na Arusha na ilifika mkoani Arusha miaka 30 iliyopita ambapo Sh bilioni 14 zimetumika katika utengenezaji na ukarabati wa reli hiyo.

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi