loader
Dstv Habarileo  Mobile
Basi lapinduka, laua 15, lajeruhi 20 :JPM atuma salamu za rambirambi

Basi lapinduka, laua 15, lajeruhi 20 :JPM atuma salamu za rambirambi

WATU 15 wamekufa na wengine 20 kujeruhiwa katika ajali ya barabara, baada ya basi la abiria kupinduka katika mteremko wa Kumnyange wilayani Ngara mkoa wa Kagera.

Rais John  Magufuli ametuma salamu za rambi rambi na kukumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva wa magari, kuzingatia sheria  za usalama barabarani  kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti kutokana na vifo hivyo na kutaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani, kuchukua hatua dhidi ya watumiaji wanaokiuka sheria za barabarani.

 “Nimesikitishwa na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, nawapa pole wafiwa wote na nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majozi,”alisema Rais Magufuli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alisema basi  lenye namba za usajili T670DKl aina ya  Tata, linalojulikana kama Fly Emirates linalofanya safari zake za Ngara – Bukoba, lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu 15 na majeruh 20.

Kamanda Malimi alisema ajali hiyo, ilitokana na kushindwa kwa mifumo ya breki katika eneo la Kumunyange; na kuwa pamoja na dereva kujitahidi kulimiki gari hilo, kona ya mwisho ilimshinda na kutumbukia katika korongo.

Alisema kati ya marehemu hao 15, watatu ndio wametambuliwa kupitia vitambulisho vyao na ni raia wa Burundi. Pia majeruhi wanane kati ya 20 wametambuliwa ni raia wa nchi hiyo.  

Alisema polisi inaendelea na uchunguzi, kujua sababu za ujio wa raia hao nchini. Majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali za Nyamihaga na Murugwanza wilayani Ngara.

Kamanda Malimi alisema polisi inamshikilia dereva wa gari hilo, Farasi Faustine ambaye ni miongoni kwa majeruhi kwa kusababisha ajali na vifo na anaendelea kupatiwa matibabu chini ya usimamizi wa polisi na hali yake ni mbaya .

Miili ya marehemu inaendelea kuhifadhiwa katika hospitali za Murugwanza na Nyamiaga hadi ndugu na jamaa wafike. Kamanda alisema hiyo ni ajali mbaya zaidi katika mkoa wa Kagera tangu mwaka huu uanze.

foto
Mwandishi: Diana Deus, Bukoba

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi