loader
Tambo za wagombea Tarime, Kisarawe kuelekea uchaguzi

Tambo za wagombea Tarime, Kisarawe kuelekea uchaguzi

KESHOKUTWA Watanzania wanapiga kura kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Wagombea waliokuwa madarakani wanaonesha waliyoyafanya katika kipindi kinachopita huku, wapya wakiweka hadharani sera na mipango waliyo nayo.

Mwandishi CHRISTOPHER GAMAINA wa TARIME amezungumza na wagombea Ubunge wa Tarime Mjini; MICHAEL KEMBAKI wa CCM na ESTHER MATIKO wa CHADEMA huku Mwandishi CLAUDIA KAYOMBO akiwa KISARAWE akizungumza na MOSHI MUGALU anayegombea udiwani katika Kata ya Chole, iliyopo Kisarawe mkoani Pwani. Ungana nao.

KEMBAKI MGOMBEA ubunge wa Tarime Mjini kupitia CCM, Michael Kembaki anasema kitendo cha kujitolea kuchangia uboreshaji wa elimu hata baada ya kutochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015, kinadhihirisha kuwa, atakuwa kiongozi sahihi kwa maendeleo ya wakazi wa jimbo hilo.

Anataja baadhi ya miradi aliyojitokeza kuunga mkono juhudi za wananchi kuitekeleza akiwa siyo mbunge kuwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Tagota Alipochangia mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya Sh milioni tatu na Sh milioni nne taslimu kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo vya shule hiyo.

Joyce Marwa, mkazi wa Tagota anasema: “Toka mwaka 2015 kura zake zilipopungua, Kembaki hakuwa na kinyongo wala kukata tamaa, aliendelea kutekeleza ahadi zake kwa wana-Tarime. Mfano, amesimamia ujenzi wa sekondari ya Tagota kwa misaada mbalimbali, tayari imejengwa na watoto wanasoma.”

Kwenye Shule ya Msingi Nyamwino, Kembaki alipeleka msaada wa saruji mifuko 30 kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na mifuko 10 ya saruji kuchangia uboreshaji wa miundombinu ya Shule ya Msingi Kemairi.

“Tumeona Kembaki ni mfano mzuri wa kuigwa, tunasikia kila sehemu anasaidia, huyu ni tofauti na wanasiasa walio wengi ambao wakishindwa katika uchaguzi huwa wanasusia kurudi nyumbani kuchangia maendeleo ya jamii,” anasema mkazi wa Kemairi, Lucy Marwa.

Kembaki alijitokeza pia, kuchangia uboreshaji wa miundombinu ya Shule ya Tambo za wagombea Tarime, Kisarawe kuelekea uchaguzi Msingi Azimio kwa kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa chenye thamani ya Sh milioni 19.7.

Aidha, alitoa msaada wa vigae vya Sh milioni 3.6 kuchangia ujenzi wa nyumba za askari polisi katika Kata ya Nyandoto.

Alijitolea pia kununua vyerehani 10 na kuvikabidhi kama msaada wake kwa kikundi cha Amani na Upendo kilichopo katani Turwa kuwasaidia wajasiriamali wadogo kujiinua kiuchumi kupitia ushonaji.

Kembaki anawaomba wakazi wa Jimbo la Tarime Mjini ridhaa ya kuwawakilisha bungeni ili kuchochea zaidi maendeleo ya kisekta jimboni humo. Mwenyewe anasema: “Nilirudi kuwa pamoja na ninyi… ahadi karibia zote nilizowaahidi nimeshazitekeleza.

Naombeni kura zenu tuchochee maendeleo ya jimbo letu. Ogopa mtu ambaye aliahidi na hakutekeleza.” Kembaki anasema ukosefu wa maji safi ya bomba katika mji wa Tarime na viunga vyake ni miongoni mwa vipaumbele atakavyoshughulikia haraka baada ya kuchaguliwa na anaahidi pia kuhakikisha ujenzi wa Soko Kuu la Tarime unaanza haraka ili wananchi wafanye biashara kwa ufanisi zaidi na kujiinua kiuchumi.

Akiwa jimboni Tarime Mjini hivi karibuni, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa anasema wakimchagua Kembaki watakuwa wameliweka jimbo hilo katika nafasi nzuri ya kupata maendeleo haraka kijamii na kiuchumi.

Majaliwa anasema: “Mleteni Kembaki bungeni, mchagueni Kembaki tulete maendeleo.”

MATIKO

Esther Matiko, mgombea anayetetea Ubunge Tarime Mjini kwa tiketi ya Chadema.

Anasema maendeleo ya kisekta aliyowaletea wakazi wa jimbo hilo yanatosha kuwashawishi kumwongezea kipindi kingine cha miaka mitano ya kuwawakilisha bungeni. Matiko anasema licha ya kukabiliwa na kesi kadhaa mahakamani jijini Dar es Salaam, muda wote alikuwa mwepesi wa kupokea na kushughulikia kwa mafanikio ufumbuzi wa matatizo jimboni humo.

Anasema katika kipindi chake cha miaka mitano ya ubunge Tarime Mjini alielekeza nguvu kubwa katika uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii, hasa miundombinu ya barabara, afya, Elimu, umeme na maji.

“Wakati nachaguliwa kuwa mbunge mwaka 2015 barabara nyingi katika jimbo hili zilikuwa hazipitiki, lakini sasa hivi barabara za mitaa yote 81 zimezibuliwa kwa kiwango cha changarawe, makaravati na madaraja yamejengwa.

Baadhi ya barabara zikiwemo za Bomani zimewekewa lami,” anasema. Kuhusu afya, Matiko anasema katika kipindi chake cha uongozi serikali imepeleka x-ray mbili mpya kwa ajili ya huduma za kitabiku katika Halmashauri ya Mji wa Tarime sambamba na ujenzi wa maabara za kisasa ingawa bado kuna changamoto za dawa, vifaa tiba, watumishi na huduma ya maji.

“Katika kipindi changu cha uongozi tumefanikiwa kujenga kituo cha afya eneo la Magena kwa Sh milioni 400 zilizotolewa na serikali na mimi mwenyewe nilipeleka magodoro 28 yenye thamani ya Sh milioni tano… Tumefanikisha ujenzi wa Zahanati ya Nkongore kutokana na msaada uliotolewa na Benki ya NMB, tumepeleka magodoro huko na tumeanzisha ujenzi wa kituo cha afya eneo la Kenyamanyori,” anasema Matiko.

Shule mpya za msingi zilizojengwa jimboni huko kwamiaka mitano inayopita sasa ni Mtingiro, Buguti, Mturu, Rembilwi, Taramroni na Nyamwino, ukiacha Regoro inayosubili usajili kutoka wizara yenye dhamana.

“Kwa sekondari tumeboresha miundombinu katika shule nyingi kutokana na fedha za mfuko wa jimbo na wangu binafsi.

Tumejenga shule mpya za sekondari za Iganana, Tagota na Nkongore,” anasema. Mafanikio mengine anasema ni ukarabati wa miundombinu inayohusisha majengo ya Chuo cha Ualimu Tarime (TTC), Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Tarime, shule za sekondari za Mogabiri na Nyamisangura.

Kwa mujibu wa Matiko, asilimia 50 ya mitaa 81 inayounda jimbo la Tarime Mjini imeshafikiwa na huduma ya umeme kupitia REA. “Ninaamini kabla ya mwaka 2021 asilimia zaidi ya 80 ya mitaa hiyo itakuwa imepata umeme,” anasema.

Matiko anasema tayari jimbo hilo limeingizwa kwenye mradi wa kupata maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria unaotarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa kutokana na mkopo wa Sh bilioni 14 kutoka nchini India.

Kuhusu uchumi, Matiko anasema katika kipindi cha uongozi wake mapato ya Halmashauri ya Mji wa Tarime yameongezeka kutoka Sh milioni 520 hadi bilioni 1.5 na akichaguliwa tena, ataelekeza msukumo zaidi kuboresha miradi ya maji, elimu, afya, uchumi na michezo.

“Ninatamani pia tujenge maktaba ya kisasa kwa ajili ya watu wote jimboni na bahati nzuri kuna mfadhili yuko tayari kutusaidia katika hili baada ya kupata eneo kwa ajili ya ujenzi huo,” anasema Matiko.

MGALU WA CHOLE, KISARAWE

Moshi Mugalu, ni mgombea udiwani katika Kata ya Chole iliyopo Kisarawe mkoani Pwani. Ubora wake katika utumishi wa umma ndio ulimfanya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, akubali kumnadi na kumwombea kura za udiwani katika hiyo.

Katika ufunguzi wa kampeni za kiwilaya kijijini Kwala, Jafo anasema: “Mchagueni Mgalu, ni mtendaji mzuri tena asiye na maneno mengi. Anasema changamoto ya maji kwa wakazi wa Kata ya Chole ndiyo hasa iliyomvuta katika siasa.

Mwaka 2015 aligombea udiwani na kushinda. Anasema amepania kumalizia kero ya uhaba wa maji, nishati ya umeme, miundombinu mibovu ya barabara katika kata hiyo na kuhakikisha unafanyika ukarabati na ujenzi wa shule.

Anasema: “Nikichaguliwa, nitahakikisha kero hizo zinafika mwisho na kukomesha migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji.” Kwa mujibu wa Mgalu Chole, ilikuwa kawaida akinamama kulindia maji visimani hadi usiku wa manane na wanapopata ndoo tatu, kipaumbele chao kinakuwa kupikia na kunywa.

Mkazi wa kata hiyo, Teopista Mtani anasema kabla ya kupata maji yaliyochimbwa na serikali, lilikuwa ja,no la kawaida klwa mtu kumaliza siku mbili mfululizo bila kuoga.

Anasema kwa kushirikiana na Mbunge wa Kisarawe aliyemaliza muda wake (Jafo), wamejenga bwawa la maji Chole lililogharimu Sh bilioni 1.6 na limeanza kunufaisha vijiji vya Kurui, Chole na Mafumbi.

Kuhusu shule, anasema zilizokuwa chakavu kabla ya 2015 zimekarabatiwa na nyingine mpya kujengwa, hivyo anatoa mwito kwa wapiga kura kumpa kura za kutosha yeye, Jafo na mgombea urais, John Magufuli ili waendeleza utumishi waliouanza.

“Shule ya Msingi Kwala imekarabatiwa na Yombo Lukingo wanafunzi walikuwa wanasomea chini ya miti, sasa wanasomea katika madarasa baada ya kujengewa madarasa yao… Uhaba wa walimu uliokuwa unazikabili shule, umepungua kwa kiwango kikubwa baada ya kuongezewa walimu na nikichaguliwa tena, nitahakikisha unakwisha,” anasema.

“Barabara ya kutoka Kurui hadi Kwala, ya kutoka Chole kwenda Gwata zimetengewa Sh milioni 90 kwa ajili ya matengenezo. Barabara kutoka Kurui hadi Chole ilikuwa mbovu, lakini sasa inapitika vizuri,” anasema na kuongeza: “… kati ya vijiji sita vya kata hii, vinne vina umeme na viwili mkandarasi anaendelea na kazi.”

Anasema akichaguliwa atahakikisha kila kijiji kinakuwa na kituo cha polisi ili kuwahakikishia wananchi ulinzi kwani tayari alishawaagiza viongozi wa vijiji vyote kutenga maeneo kwa ajili hiyo.

Kwa mujibu wa Mgalu, atahakikisha viwanda vingi zaidi vinajengwa na kuwa chachu ya ajira huku akishirikiana na diwani mwenzake kufufua utalii eneo la Pango la Mwingereza ambalo ni kivutio kizuri ya utalii kilichosahaulika.

Mintarafu afya anasema: “Hatukuwa na kituo cha afya, sasa tunacho kile cha Chole na tuna zahanati ya Kwala, Mafumbi na Yombo Lukingo.” Moshi Mugalu Esther Matiko Michael Kembaki

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/99aac8b2612caafc8e1a5235554fec82.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi