loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM atoa mwezi wananchi 4000 wapate umeme

JPM atoa mwezi wananchi 4000 wapate umeme

MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli amemuagiza Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani ahakikishe ndani ya mwezi wananchi 4000 mkoani Manyara wanaunganishiwa umeme.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana wakati wa mkutano wa kampeni mkoani Manyara. Alisema mkoa huo una changamaoto ya kuunganisha umeme kwa wananchi kwa wakati na Meneja wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Manyara Rehema Mashinji alimjulisha kuwa wananchi 4,000 wamelipa 27,000 za kuunganishiwa umeme lakini bado hawajaunganishiwa.

Rehema alimweleza Magufuli kuwa wananchi hawajaunganishiwa umeme kwa sababu ya upungufu wa fedha.

Akiwa jukwaani mgombea huyo alimpigia simu Waziri Kalemani kumjulisha hali hiyo na kiongozi huyo wa wizara akamuahidi kuwa kuanzia kesho changamoto hiyo itafanyiwa kazi.

“Ndani ya mwezi mmoja muwe tayari kutatua tatizo hilo, kama hakuna fedha kama ambavyo meneja amesema zungumza na Waziri wa Fedha au Katibu Mkuu ili kushughulikia suala hilo,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa Wizara ya Nishati imekuwa ikifanya vizuri lakini kwa mkoa huo hawajafanya vema.

Aliagiza Dk Kalemani awasiliane na viongozi hao ili apate Sh bilioni 1.5 za kufanyia kazi hiyo. Pia aliagiza kero mbalimbali kwenye mkoa huo zifanyiwe kazi zikiwemo barabara, na ujenzi wa kituo cha mabasi.

Alisema anatamani mkoa huo uwe na kiwanda kikubwa cha vitunguu ili wananchi wa eneo hilo wakue kichumi. “Miradi ya maji ni moja ya changamoto kwa eneo la Babati ndio maana ninaomba tena nafasi ili n ikamilishe miradi mbalimbali hata iliyoko katika sekta ya utalii,na madini,” alisema.

Kuhusu Muungano aliwataka wananchi kuwa macho na kutowapigia kura wagombea wasiojua thamani ya Muungano wa Tanzania na wanataka kuuvunja.

“Msiwachague wagombea wasiojua thamani ya Muungano, wanataka uvunjwe alafu wanagombea urais wa Tanzania, hawajui wanagombea nini kwa sababu huwezi kuuvunja Muungano alafu unataka urais wa Tanzania, hakuna Tanzania bila Zanzibar, huku ni kuharibu utulivu na amani ya nchi” alisema.

Magufuli alisema, biashara ya Zanzibar inategemea Tanzania bara na kwamba raia wa pande hizo mbili za Muungano wana historia ndefu na wako maeneo mbalimbali ya nchi.

“Tutengeneze amani, nimeingia madarakani nimekuta amani na hata sasa amani ipo nataka hata nikiondoka niiache nchi iendelee kuwa kisiwa cha amani” alisema.

Alisema mwaka 2015 alialikwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda kwenda nchini humo kujifunza madhara ya kuchezea amani na kwamba alimpeleka kwenye makumbusho kulikohifadhiwa mafuvu ya Warwanda zaidi ya milioni moja yaliyotokana na mauaji ya kimbari.

“Nampongeza rafiki yangu Kagame mwaka 2015 alinialika Kigali ameitunza sasa amani ipo,alinipeleka kujifunza kutunza amani,niliona mafuvu ya Warwanda zaidi ya milioni yakiwemo ya watoto, amani ilikosekana mauaji ya kimbari yakaharibu nchi,tuna mengi ya kujifunza,tusikubali kuichezea.

Wakati mwingine watanzania wanachonganishwa na watu wasiokaa hapa nchini,wana pasi za kusafiria za nchi nyingi”,alisema Magufuli.

Akizungumzia kero za Babati Mjini na Manyara kwa ujumla Magufuli alisema amesikia kero ya wananchi hao kuomba wataalamu kwenda kufanya utafiti ili kutibu maji yao yenye madini ya floraidi kwa wingi.

Katika mkutano huo Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye alisema hakuna chama cha siasa nchini kinachoweza kushindana na CCM kwa sasa hivyo hakuna mgombea anayeweza kumshinda Magufuli.

Alisema wapinzani wanaweza kufanikiwa miaka ijayo kama kitaundwa chama cha siasa cha upinzani na si vya sasa vya wanaharakati.

Awali akiwa Magugu, Magufuli aliupa hadhi eneo hilo kuwa Mji Mdogo wa Magugu. Kuhusu uchumi alisema, vita ya uchumi ni ngumu na kuwataka Watanzania kutochagua wagombea watakaowagawa.

Alisema Tanzania sasa ni taifa kubwa, wengine walizunguka nchi mbalimbali ikiwemo Ubeljiji na Ulaya kwamba Tanzania isipewe fedha yoyote ya misaada ikiwemo ule wa elimu na leo ni wagombea.

Awali Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliwashukuru Watanzania waliohudhuria mikutano ya CCM na kwamba imefanyika kwa utulivu na ustahimilivu.

Alisema zimefanyika kampeni za kisasa na kistaarabu ikiwa ni mikutano yenye kujali amani na upendo kwa kila mmoja, na kuwataka Watanzania kuendelea kulinda tunu ya taifa ambayo ni amani na ushindi wa CCM uwe na alama ya amani.

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi