loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli azindua msikiti wa Chamwino,  ataka watanzania kudumisha amani

Magufuli azindua msikiti wa Chamwino, ataka watanzania kudumisha amani

RAIS John Magufuli amezindua msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally huku akiwasihi Watanzania kudumisha umoja na mshikamano na wasikubali kuvurugwa.

Pia aliwataka Watanzania watumie haki yao kupiga kura kwa utashi wao na kuamua mazuri ya kujenga umoja na mshikamano wa Watanzania.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wilayani Chamwino wakati wa uzinduzi wa msikiti wenye uwezo wa kuhudumia waumini 500 kwa wakati mmoja.

Alisema umoja na mshikamano ndio sifa ya Tanzania duniani ambayo imeasisiwa na waasisi wa Taifa.

“Watanzania tuendelee kudumisha tunu ya umoja na mshikamano iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili na kamwe tusikubali kuibomoa iwe kwa dini au kabila.”

Rais Magufuli aliongeza kuwa: “zimebakia siku moja ili Watanzania mkapige kura kwa kuamua mazuri, hivyo ni vizuri kuitumia siku hiyo katika kujenga umoja wa watanzania.”

“ Niwahimize ndugu zangu tusisahau kupiga kura na mimi ni mmoja wa wagombea sio vibaya nikitumia nafasi hii kuomba kura, tukapige  kura kulingana na utashi wa mioyo yetu. Mimi ni mwana CCM nitafurahi mkichagua mbunge, diwani  anayetokana na CCM na mimi ninayehusika na CCM.”alisema na kuongeza;

“Sina cha kusema ishara hii mliyoionyesha leo (jana) ni ya kipekee sio tu ya kitanzania na duniani pia, upendo huu na umoja huu ni wa maajabu sana, tuendelee kushikamana.”

Rais Magufuli alisema msikiti huo utumike kuwaweka pamoja kama ndugu, uwe fundisho kwa wana Chamwino na Watanzania katika kuwa wamoja na kutambua kuwa wana wajibu wa kumtanguliza Mungu maisha yote.

“Msikiti huu ukatoe mafunzo yatakayojenga umoja wa watanzania,ukaguse na mioyo yao ya kutekeleza maandiko matakatifu yaliyopo kwenye Quran na yakajenge umoja ndani ya watanzania wote.”

Aidha, Rais Magufuli aliagiza kiasi cha Sh milioni 1.133 kilichobaki kwenye ujenzi wa msikiti kiwe kianzio cha kujenga kanisa la Wasabato na kusisitiza kuwa endapo atarudi Ikulu atahakikisha madhehebu yote yanayozunguka Ikulu ya Chamwino yatajengwa na kuwa ya kisasa.

“Tulianza kujenga nyumba ya ibada kwa wanaosali Jumapili, na sasa tumekamilisha kwa wanaosali Ijumaa, sasa tunakwenda kujenga kwa wanaosali Jumamosi, nataka nyumba za ibada zote zinazozunguka Ikulu ziwe za hadhi.”alisema.

 

Mufti wa Tanzania Sheikh Zuberi alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea msikiti wenye hadhi na kumpongeza kwa uamuzi wake wa kurudisha mali za Waislamu na wanadini zilizopotea, chukuliwa au kubabaishwa.

"Umekuwa kiongozi  mwenye kipaji cha kupenda viongozi wa dini na mwenye kumtanguliza Mungu katika kila jambo. Quran inasema anayefanyia wema mlipeni na kama hauna cha kumlipa muombeeni."

Mufti Zuberi alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kujitokeza kupiga kura kwa utulivu na amani na kuchagua viongozi bora.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charles Mbuge alisema ujezi wa msikiti huo umekamilika kwa asilimia 100 na umejengwa kwa gharama ya Sh milioni 319.28 na kusaliwa na Sh milioni 1.133,388.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi