loader
Simba hali tete

Simba hali tete

BAADA ya Simba kupoteza michezo miwili mfululizo inadaiwa  hali si shwari ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake mtaa wa Msimbazi na Uhuru, Kariakoo, Dar es Salaam.

Simba juzi ilifungwa na Ruvu Shooting kwa bao 1-0 kwenye  uwanja wake wa nyumbani Uhuru, Dar es Salaam na mchezo uliopita ilifungwa na Tanzania Prisons kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga.

Baada ya mchezo wa juzi kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck alitoa kauli iliyotafsiriwa kama ni fumbo na inawezekana kukawa kuna kitu kinaendelea ndani ya timu hiyo.

 “Sifikiri kama tumefungwa kwa sababu ya ‘game fitness’ ni ngumu kwa wakati huu kutaja ni nini tatizo hususani kama utaeleza kila kitu katika vyombo vya habari,”  alisema Sven.

Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza kuwa Mbelgiji huyo haelewani na meneja wa timu, Patrick Rweyemamu na kwenye uongozi inadaiwa kuna mpasuko na timu ni kama wamesusiwa  Salim Abdallah ‘Try Again’ na Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez.

Inadaiwa kuwa hata kwenye nafasi ya nahodha kuna mgogoro na nahodha John Bocco amepokwa cheo hicho.

Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting nahodha alikuwa Jonas Mkude wakati nahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alikuwa katika kikosi kilichoanza na hata alipoingia John Bocco ambaye ndiye nahodha wa timu bado na yeye hakupewa kitambaa chake cha unahodha.

Viongozi wa juu wa Simba jana hawakuwa tayari kuzungumza hilo lakini habari za ndani zinadai wameitana vikao kuwekana sawa na Mtendaji Mkuu, Barbara alipopigiwa simu yake iliita bila kupokelewa.

Mwandishi habari za michezo kutoka Ghana, Nuhu Adam ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa uongozi wa Simba haufurahishwi na mwenendo wa timu yao chini ya Kocha mbelgiji, Sven Vanderbroeck na watakutana kuamua hatma yake katika mechi zijazo endapo matokeo yataendelea kuwa mabaya.

Jana  Bocco aliomba radhi wanachama viongozi pamoja wapenzi wote wa Simba na kumshukuru Mungu kwa kuwapa moyo wa upendo wana Simba  wa kuipenda timu yao na kuiunga mkono katika vipindi tofauti na kila mkoa wanaokwenda kucheza. 

 “Kwa niaba ya wachezaji tunaomba mtusamehe kwa matokeo tuliyopata katika michezo miwili iliyopita, tuliteleza na hatupaswi kuteleza tena na hii ndio ahadi yetu kwenu kurekebisha makosa yetu na kurudi wenye sura mpya na upambanaji kwa michezo yote ijayo,” alisema Bocco kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram. 

Alisema ili warudishe furaha kwa kupata matokeo mazuri kama walivyozoea halitajitokeza tena katika michezo ijayo.

Bocco ambaye alikosa penalti katika mchezo dhidi ya Ruvu, aliwaomba mashabiki, wanachama, viongozi na wapenzi wa klabu kuendelea kuwaunga mkono.

Katika msimamo Simba inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 13 huku Azam FC ikiongoza ikiwa na pointi 21 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 19 na Biashara inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 16.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/ce15a90279a50d13b74d8eaf2ff9a6eb.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi