loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tozo ya unyaufu korosho yamkera waziri mkuu

Tozo ya unyaufu korosho yamkera waziri mkuu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuna watu wanataka kuwaumiza wakulima wa korosho kwa kigezo cha tozo ya unyaufu, jambo ambalo hawezi kulikubali.

Alibainisha hayo juzi wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Boma katika mkutano uliofanyika viwanja vya Bomani vilivyopo Mji Mdogo wa Nachingwea, mkoani Lindi.

"Zao la korosho lilikuwa na tozo 12, tumeziondoa nyingi na kubakiza tano tu, lakini kuna watu wachache na hasa wenye maghala ambao bado wanarudisha kinyemela tozo ya unyaufu, sitaki kusikia hiyo kitu," amesema.

Alisema katika msimu unaoendelea wa ununuzi wa korosho, hataki kusikia habari ya tozo ya unyaufu kwa kuwa sheria ya unyaufu inaruhusu tozo hiyo ianze kutumika baada ya miezi sita na kwa maana hiyo, haimgusi mkulima wala mnunuzi.

"Hata mkulima akiokota korosho zake leo na akaziuza mwezi ujao, bado hawezi kukatwa tozo ya unyaufu kwa sababu kisheria tozo hiyo haimgusi. Ni marufuku kutoza makato ya unyaufu, sitaki kusikia kuanzia leo hii wakulima wanatozwa unyaufu, hii ni biashara ya wachache tu," alisema Majaliwa.

Wakati huohuo; Waziri Mkuu Majaliwa amesema Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani ni ukombozi kwa wakulima kwa kuwa ndio uliochangia kupandisha bei ya korosho kwa kutumia minada.

"Mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani si mnunuzi wa mazao kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai, bali ni mfumo wa kukusanya mazao ili yawekwe ghalani kusubiri bei iwe nzuri huku mkisubiri mnada," alisema.

Akaongeza: "Kabla ya mnada kufanyika, lazima kuwa na mahali ambapo hizo korosho zitahifadhiwa, ndiyo huko kwenye maghala. Ukifikisha mzigo wako, unapewa risiti ili kutambulisha kwamba mkulima mmoja ana kilo kadhaa, na mwingine ana kilo kadhaa.

Zikishakusanywa ni rahisi kuita wanunuzi na kuwaeleza mna tani ngapi au kilo ngapi ndipo wao watamke bei. Wakiwa na bei ya chini, mnawakatalia na mnapanga mnada kwa siku nyingine."

Alisema wataalamu walishafanya utafiti na kueleza kwamba gharama zote za mkulima wa korosho tangu kulima, kupanda, dawa hadi kuvuna, anakuwa ametumia Sh 1,700 kwa kilo. "Kwa hiyo, ukipata bei ya Sh 3,000 kwa kilo, ile ya juu inakuwa ni faida yako mkulima. Tatizo ni kwamba bei ya maisha inapangwa kwenye soko la dunia, na msimu huu tulianza na Sh 2,700, lakini sasa hivi imefika Sh 2,400 kwa kilo."

Akielezea tatizo lililosababisha kushuka kwa bei, Majaliwa alisema korosho si zao pekee lililoathiriwa na kushuka kwa bei mwaka huu, bali hata mazao mengine kama pamba, chai, kahawa na tumbaku.

"Kwa mfano, bei ya pamba imeshuka kutoka Sh 1, 200 hadi Sh 800 kwa kilo; kahawa imeshuka kutoka Sh 1,800 hadi Sh 1,200 kwa kilo, na tumbaku imeshuka kutoka Sh 1,700 hadi Sh 1,400."

"Korosho ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini yaliyokosa soko msimu uliopita baada ya mataifa ya Ulaya kufunga mipaka yao kutokana na ugonjwa wa corona na hivyo wanunuzi hawawezi kuja nchini. Wanunuzi wakubwa wa korosho wanatoka China, Vietnam na India. Hawa wenzetu bado wanahangaika na ugonjwa huu, hawawezi kutoka nje, hawawezi hata kusafiri kuja nchini mwetu," alisema.

Akaongeza: "Korosho, pamba, tumbaku, chai na kahawa hayakuwa na bei nzuri kutokana na corona si vinginevyo. Serikali hainunui mazao, kazi yake ni kutengeneza mazingira mazuri ya soko…”alisema.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Lindi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi