loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waangalizi wasema uchaguzi ulikuwa huru, wa haki

Waangalizi wasema uchaguzi ulikuwa huru, wa haki

WAANGALIZI  wa Uchaguzi Mkuu wa kimataifa na wa kutoka ndani ya nchi wamesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na kwamba, mchakato huo uliotawaliwa na amani na utulivu.

Mwakilishi wa waangalizi wa kimataifa, Rais mstaafu wa Burundi, Sylvestre Ntibantunganya alitoa kauli hiyo jana Dodoma kabla ya Rais Mteule John Magufuli na mgombea mwenza wake Samia Suluhu Hassani kukabidhiwa vyeti vya ushindi kwa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais.

Ntibantunganya alisema wakati wa hotuba na katika mahojiano kuwa waangalizi wa kimataifa wanatoa maoni yao kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki na ulitawaliwa na utulivu na usalama wa kutosha kuanzia katika upigaji kura vituoni na katika kutoa matokeo.

“Sisi kama waangalizi wa kimataifa, tunatoa maoni kwamba uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa huru na haki kwani tume ilijitihidi kuandaa vizuri na wananchi wamepiga kura kwa amani na utulivu,” alisema.

Ntubantunganya alisema uchaguzi huo ulifanyika vizuri kwa kuwa kutokana na maandalizi mazuri ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema, NEC ilifanya kazi nzuri ya kuandaa uchaguzi na kuwawezesha Watanzania wafanye kazi ya kuchagua viongozi kwa amani na utulivu.

Ntubantunganya alisema waangalizi zaidi ya 196 walipita katika maeneo mbalimbali nchini na kuangalia wananchi namna walivyopiga kura na kubaini kuwa upigaji kura ulifanyika kwa amani na utulivu hivyo wao wanasema uchaguzi ulifanyika kwa utulivu na amani.

Kiongozi wa Watazamaji wa uchaguzi kutoka ndani ya nchi, Mwantumu Mahiza alisema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ulifanyika kwa amani na utulivu kutokana na maandalizi mazuri ya NEC kuanzia kwenye mchakato wa kampeni, upigaji kura hata utangazaji matokeo.

Mahiza alisema uchaguzi wa mwaka huu ulitaliwa na utulivu mzuri kuanzia kwenye vituo.

Alisema, NEC iliandaa vituo vya kutosha na hivyo kupunguza misongamano vituoni na hivyo wananchi hawakupoteza muda kwenye vituo kusubiri kupiga kura.

Akatoa maoni kuwa katika uchaguzi ujao 2025, elimu ya mpiga kura inahitajika  zaidi ili wananchi wengi waendele vituoni kupiga kura kuliko ilivyotokea katika uchaguzi huu kwa kuwa watu wengi hawakwenda kupiga kura.

Wakati huo huo, wagombea 10 wa urais waliofika kwenye halfa ya kukabidhi vyeti mshindi wa kiti ya urais wa Tanzania na mgombea mwenza wake, walimpongeza Magufuli kwa kushinda na wakaahidi kushirikiana naye kuijenga nchi.

Aliyekuwa mgombea kupitia chama cha ADC, Queen Sendiga alimpongeza Rais Mteule Magufuli kwa ushindi aliopata na akasema yupo tayari kushirikiana naye.

Sendiga alisema Watanzania wanatakiwa kuelewa kwamba uchaguzi ni kama wana masumbwi wanavyocheza ulingoni, lakini refa akipuliza kipenga kwamba mpambano umeisha basi wanakumbatiana kwamba mchezo umeisha.

Alisema wao wapo tayari kushirikiana na Rais Magufuli kuijenga nchi kama serikali ikiwahitaji ili kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi kwa maslahi ya Watanzania.

“Tunaahidi kukupa ushirikiano ukiona inafaa kukupa ushirikiano kwa ajili ya kusaidia Watanzania ambao wanajitaji maendeleo, lakini nawaomba wananchi waendeleze amani ili kupata maendeleo zaidi,” alisema Queen.

Aliviomba Rais mteule kuvifikiria vyama visivyo na wabunge ambavyo havipati ruzuku, ili kusaidia chochote kwa lengo la kuendelea na kuwafikia Watanzania kueleza sera zao.

Mgombea kwa tiketi ya NRA, Leopord Mahona mgombea mdogo kuliko wote alimpongeza Rais Magufuli ambaye ni mzee wake na baba yeke kwamba amepata ushindi mkubwa wa kishindi akamwomba sasa arudi kuchapa kazi na yeye yupo tayari kusaidiana naye.

Naye mgombea urais kwa tiketi ya ADA-TADEA, John Shibuda alisema wao wanampongeza Rais Magufuli kwa ushindi na hivyo watashirikiana naye na kuhakikisha nchi inasonga mbele.

Alisema kuvunjika kwa jembe si mwisho wa kilimo, hivyo wamekubali wameshindwa sasa wanajipanga upya kwa ajili ya uchaguzi ujao, asiwepo mtu wa kuharibu, sasa wamwache kiongozi aliyeshinda kufanya kazi.

Shibuda ambaye ni Mwenyekiti wa Vyama Vya Siasa alisema matokeo ya ushindi wa Magufuli si wa Tume ya Uchaguzi, bali ni matakwa ya wananchi wala si kutokana na kigezo cha kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya hadhara.

Alisema pamoja na wagombea kuzieleza sera majukwaani, wananchi baadaye walikuwa na muda wa kutafakari siasa safi na uongozi bora.

Aliwapongeza wanaanchi kwa uamuzi wao wa kuichagua CCM miongoni mwa vyama 15, ameshinda kwani anayeshindwa leo anaweza kushinda kesho akawaomba kuwa na uvumilivu wagombea walioshindwa kwani asiyekubali kushindwa si mshindani.

 “Kinachotakiwa wa wagombea wote na wanachama wao ni kuuenzi umoja na kudumisha tunu ya amani na usalama na jamii kuendelea kushikamana kwani kuna maisha baada ya uchaguzi.”alisema Shibuda.

Mgombea urais kwa tiketi ya AAFP, Seif Maalim Seif alimpongeza rais Magufuli kwa ushindi lakini akaomba kwamba walioshindwa wanatakiwa kumuunga mkono na kumsaidia mshindi kuijenga nchi.

Mgombea wa SAU, Muttamwenga Mgahywa alisema uchaguzi umeisha kinachotakiwa sasa ni kuingia katika awamu nyingine ya kuijenga nchi, aliyeshinda apewe nafasi ya kuongoza nao wapo tayari kushikiana naye katika kuijenga nchi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/17101cbe5585fb3ee912d6b384f4d455.jpg

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi