loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Kutotumia vyoo kunavyohatarisha afya wakazi mwambao Ziwa Victoria

ZINAHITAJIKA jitihada za ziada kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyoko kandokando mwa Ziwa Victoria, pamoja na wale wanaoishi ama wanaofanya shughuli za uvuvi kwenye visiwa vilivyomo ndani ya ziwa hilo, ili kuwahamasisha wananchi kujenga vyoo bora na kuvitumia.

Hatua hii itasaidi kuepusha agonjwa ya milipuko kikiwemo kipindupindu.

Miaka zaidi ya 50 baada ya uhuru, bado baadhi ya wakazi wanaoishi kandokando mwa ziwa Victoria na visiwani vilivyo katika ziwa hilo wana tabia ya kujisaidia pembezoni mwa ziwa na pale mvua inaponyesha kinyesi chao kinasombwa na maji na kuingia ziwani.

Jambo hili limekuwa ni hatari kwani linachafua maji na kueneza magonjwa kikiwemo kipindupindu ambacho husababishwa na watu kula kinyesi cha binadamu mwenye vimelea vya ugonjwa huo.

Uchunguzi unaonesha kwamba watu wengi, hata wenye vyoo, wanapokwenda kuoga, kuchota maji au kufua nguo ziwani wanatumia pia mwanya huo kujisaidia pembezoni mwa ziwa na wengine wanajisaidia moja kwa moja majini haja kubwa au ndogo.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya unaonesha kwamba magonjwa ya matumbo na ya kuhara yamekuwa ni ya kawaida sana kwa wakazi wanaoishi kwenye vijiji vilivyo katika mwambao wa ziwa hilo na wale wa visiwani.

Ni kwa msingi huo, ni vyema wataalamu wa afya wakajipanga kuhakikisha wanashirikiana na viongozi maeneo husika katika kuelimisha wananchi, ili waweze kujenga vyoo bora na kuvitumia.

Katika wilaya ya Bunda mkuu wa wilaya hiyo, Lydia Bupilipili amekuwa mara kwa mara akikemea vitendo hivyo vya watu kujisaidia ziwani na hivyo kutumia muda mwingi kuwahamasisha wananchi ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na kukitumia.

Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda, amekuwa pia akipiga vita watu kuoga ziwani akiwataka wajenge mabafu katika miji yao. Hata hivyo, baadhi ya watu vichwa vyao ni vigumu na hivyo wamekuwa wakiendelea kuoga na kufua nguo zao katika ziwa hilo, hatua inayochangia watu hao kujisaidia ziwani ingawa utawaona wanachota maji hayo hayo na kwenda nayo nyumbani kwa ajili ya kunywa na kupikia!

Baadhi yao wanadhani kwamba kutokana na ziwa kuwa kubwa, kinyesi kikiingia ziwani kinachukuliwa na maji na kutupwa mbali na hivyo kutokuwa na athari, jambo ambalo si kweli.

Pamoja na serikali kutoa agizo kwamba kila kaya iwe na choo bora na kinachotumika, uchunguzi wa mwandishi wa makala haya unaonesha kwamba kaya nyingi wilayani Bunda, hususani zilizo kando kando mwa ziwa, hazina vyoo bora na nyingine hazina vyoo kabisa. Hali ni hiyo hiyo katika maeneo ya visiwani.

Kwa upande wa wavuvi, unaweza kuona wanajenga vibanda vya muda vya kujihifadhi ziwani lakini suala la vyoo huwatilii maanani. Kimsingi wavuvi katika ziwa hilo wamekuwa wakifanya shughuli zao za uvuvi kwa kuhamahama kwa ajili ya kutafuta maeneo mengine ambako samaki wanapatikana kwa wingi.

Endapo kumetokea ugonjwa wa kipindupindu au mwingine wa kuhara, wavuvi wanapohamia katika maeneo mengine huwa rahisi kwao kusababisha ugonjwa kulipuka katika maeneo hayo walikohamia.

Visiwa vya Sozia, Namuguma na Buyanza vilivyoko ndani ya Ziwa Victoria katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wakazi wake walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kunywa maji yasiyo safi na salama na hivyo mara kwa mara walikuwa wakiugua magonjwa ya kuhara na hivyo kukitokea mlipuko wa kipindupindu wengi walikuwa wakiugua n ahata vifo kutokea.

Licha ya kujisaidia kando ya ziwa na hivyo vinyesi vyao kuingia majini, mvua inaponyesha lakini wakichota maji ya ziwa walikuwa wakiyatumia kwa kunywa bila hata kuyachemsha.

Lakini kwa kuona changamoto hiyo inazidi kuwatesa wakazi wa visiwa hivyo, hivi karibuni shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) liliamua kutekeleza miradi mikubwa miwili ambayo ni ya umeme wa jua na pia uzalishaji maji safi na salama. Hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa ya kuhara kwa wakazi wa visiwa hivyo.

Mratibu wa miradi ya UNDP Tanzania, Amoni Manyama, pamoja na mwakilishi wa shirika hilo, wanasema sababu za kuanzisha miradi hiyo katika visiwa hivyo ni pamoja na kuokoa afya za wakazi wa visiwa hivyo kutokana na kuishi katika mazingira hatarishi.

Wanasema umeme uliowekwa katika visiwa hivyo huwasaidia wananchi kupata mwanga na pia kuchaji simu zao, lakini pia unasaidia kuchuja na kuchemsha maji na kisha kuyaweka kwenye chupa maalumu ili kuuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu tofauti na bei ya maji yanayouzwa madukani.

Hatua hiyo inawawezesha wananchi wa visiwa hivyo kumudu bei hiyo na kunywa maji salama, hatua inayowaepusha na milipuko ya magonjwa matumbo kikiwemo kipindupindu.

Wakishukuru baada ya utekelezaji wa miradi hiyo, wakazi wa visiwa hivyo wanasema miradi hiyo ni mkombozi mkubwa kwao, kwani sasa itawapunguzia tatizo la magonjwa ya kuhara, amiba au mlipuko wa kipindupindu.

Charles Musita, mkazi wa kisiwa cha Sozia anasema: “Sasa hivi tunakunywa maji safi na salama. Kwa kweli tunashukuru UNDP kwa kutuletea mradi huu wa maji. Sasa maji yanachujwa kwenye mtambo maalumu na kisha kuwekwa kwenye chupa. Kabla ya mradi huu magonjwa ya kuhara na mlipuko wa kipindupindu vilikuwa vitu vya kawaida hapa kisiwani.”

Mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Stephen Ochieng, anasema kabla ya mradi huo, magonjwa ya mlipuko yalikuwa yakitokea mara kwa mara katika visiwa hivyo kikiwemo kipindupindu.

Anasema kisiwa cha Sozia, kwa mfano, kina zaidi ya wakazi elfu kumi, hivyo ukitokea ugonjwa wa kipindupindu ilikiwa ni hatari sana.

“Ndiyo maana tunaishukuru sana UNDP kwa kuleta mradi wa maji safi na salama katika hivi visiwa,” anasema.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa mradi huo, elimu ya usafi wa mazingira inapaswa kuendelea kutolewa kwa wakazi wa maeneo hayo ili wasiendelee kujisaidia ndani ya ziwa hilo au pembezoni mwake ili kujikinga na kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara.

Kutokana na umuhimu wa kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya milipuko, umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) hivi karibuni ilitoa fedha kwa kilabu ya waandishi wa habari mkoa wa Mara (MRPC) kwa ajili ya kuendesha mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya kujikinga na magonjwa ya milipuko.

Lakini pia waandishi wa habari wanaoandika habari kuhusu magonjwa ya milipuko wanawezeshwa ili wawendelee kuandika na kuripoti habari za magonjwa hayo, ili jamii iweze kuchukua tahadhari ya kujikinga nayo. 

WILAYA ya Rungwe mkoani Mbeya ni moja kati ya wilaya ...

foto
Mwandishi: Ahmed Makongo, Bunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi